Hussein Ndubikile
Peter Kakamba |
KAMANDA wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Peter Kakamba, amefariki dunia katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikokuwa akipata matibabu.
Taarifa iliyotumwa jana kwenye vyombo
vya habari na Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Bulimba, ilieza kuwa Kamanda huyo
alifariki dunia alfajiri ya kuamkia juzi.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Kakamba
alijiunga na Jeshi hilo mwaka 1988 na kupanda vyeo mbalimbali vikiwamo vya
konstebo (1988), Sajini (1991), Mkaguzi Msaidizi (1997) na Mkaguzi (2003).
Alipanda kuwa Mrakibu wa Msaidizi
(2006), Mrakibu (2008), Mrakibu Mwandamizi (2011) na Kamishna Msaidizi (2015).
Alisema Kakamba aliwahi kushika nyadhifa
mbalimbali zikiwamo za Mwendesha Mashitaka wa Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Polisi wa
Wilaya ya Mufindi, Ofisa Mnadhimu wa Polisi mikoa ya Iringa na Geita na Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Iringa.
Alizaliwa mwaka 1963 katika kijiji cha
Kawajense, Mpanda mkoani Katavi na kupata elimu ya msingi kwenye shule ya
Shanwe, Kawajense (1973-1980) na kidato cha kwanza hadi cha nne sekondari ya Kantalamba
(1981-1984).
Alipata elimu ya vidato vya tano na sita
sekondari ya Umbwe, Kilimanjaro (1985-1987) na Astashahada ya Sheria ya Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (1992-1994).
Mkuu wa Jeshi Polisi nchini (IGP),
Ernest Mangu alitoa pole kwa maofisa, wakaguzi, askari, ndugu, jamaa na
marafiki waliofikwa na msiba huo.
0 comments:
Post a Comment