Frankius Cleophace, Tarime
MWANAMKE
mwenye umri wa miaka 60 ambaye ana ulemavu wa viungo mkazi wa kijiji cha
Kemakorere kata ya Nyarero wilayani hapa anadaiwa kubakwa Novemba 15 saa 5
usiku na Wambura Nyaraita ‘Oyesu’ mwenye umri wa miaka kati ya 25 na 30
mkazi wa kijiji hicho.
Baada ya
kitendo hicho, Oyesu alitokomea kusikojulikana na jamii kuiomba Serikali
kuingilia kati ili kijana huyo akamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria ili
liwe fundisho kwa wengine.
JAMBOLEO
ilizungumza na mwathirika huyo ambaye jina lake linahifadhiwa lakini mwenye
ulemavu wa miguu na mkono aliyedai kuwa siku hiyo akiwa amelala alisikia kijana
huyo anamfuata kitandani na kumtisha huku akimwomba fedha na kisha kumbaka.
“Nilikuwa
nimelala nikasikia kijana huyo anaingia chumbani mwangu ambamo nalala peke
yangu, akaniuliza kwa nini nalala na nguo na akaniuliza vitu vitatu; pesa, mwili
wangu na roho, kuwa nimpe kimojawapo, nilivua nguo akalala na mimi kuanzia saa
tano usiku mpaka saa tisa alfajiri … niliogopa kupiga kelele,” alisema bibi
huyo.
Alimwomba
Rais John Magufuli asikie kilio chake hicho na kumsaidia usafiri kwani pamoja
na kuwa mlemavu hana baiskeli ya magurudumu matatu kwa ajili ya kutembelea ili
kupata huduma za kijamii licha ya kutendewa unyama huo.
Motende
Marwa, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, alithibitisha tukio hilo huku akisema jamii
haina budi kulaani kitendo hicho, na kuomba Jeshi la Polisi kutofumbia macho suala
hilo, ili kuhakikisha kijana huyo anasakwa kokote aliko na kutiwa nguvuni.
Diwani
wa Nyarero, Marwa Mhabas alilaani kitendo hicho huku akisema katika kata yake
ni mara ya kwanza kutokea.
“Hiki
kitendo cha kinyama katika kata yangu ni cha kwanza nakilaani na kuahidi kutoa
ushirikiano kuhakikisha kijana huyu anatiwa nguvuni, kwa sababu anajulikana na
ni wa kijijini hapa,” alisema Diwani huyo.
Thomas
Joseph, Msaidizi wa Kisheria wa Kata hiyo kutoka shirika la North Mara
Paralegal pamoja na ndugu jamaa kwa ujumla wakizungumzia ukatili huo waliiomba
Serikali kuingilia kati.
0 comments:
Post a Comment