Mariam Cyprian, Handeni
WANAWAKE wa Wilaya
ya Handeni mkoani hapa wamesema hujisikia amani na furaha wanapozalishwa na
wauguzi wa kiume waendapo kujifungua hospitali, kwani huwabembeleza wakati wote
kuliko ilivyo kwa wanawake wenzao.
Kinamama hao
walisema hayo kwenye mikutano ya uhamasishaji wa jamii kuhusu afya na
haki ya uzazi na mila hatarishi iliyofanyika wilayani humo ikiendeshwa na Shirika
la Amref Health Africa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni
kupitia mradi wa Kijana Wa Leo.
Katika mikutano
hiyo ya uhamasishaji iliyofanikiwa kuwafikia na kuwavutia maelfu ya
wakazi wa wilaya ya hiyo, mada mbalimbali zilifundishwa na kutolewa ufafanuzi
na wawezeshaji tofauti zikijumuisha magonjwa ya ngono na Ukimwi, ukeketaji,
uzazi wa mpango, umuhimu wa kuhudhuria kliniki na kujifungulia kwenye vituo vya
kutolea huduma za afya, athari za mimba na ndoa za utotoni.
Wananchi
walipata nafasi ya kuuliza maswali na kuelezea uzoefu wao kuhusu maswala mbalimbali
ya Afya ya uzazi katika maeneo wanaoishi.
Moja ya swali
lililojitokeza ni muuguzi gani wa kike au wakiume wakina mama wanapenda
awahudumie wakati wa kujifungua na kutoa majibu kwamba wanapenda kuhudumiwa na
wanaume.
Akiuliza swali
kwa watalaamu wa afya, mkazi wa Kwachaga, Abdallah Mkorogwe alitaka kujua
sababu za wake zao kupenda kuhudumiwa na wauguzi wa kiume licha ya kuwapo pia
wa kike kwenye hospitali na sehemu nyingine za kutoa huduma za afya.
Mwelimishaji
ambaye ni muuguzi wa kitengo cha afya ya mama na mtoto, Hospitali ya Wilaya
Handeni Neema Kombo aliwataka wanawake kujibu swali hilo ni muuguzi yupi
wanapenda kuhudumiwa naye wanapokwenda kujifungua?
"Mwanaume
ndio anafaa kwa sababu wanajua kubembeleza, wanajali na kutoa maneno ya
faraja hadi mtu anapojifungua lakini hawa wenzetu(wanawake) anakufokea na
kukutolea lugha chafu hadi unajutia kubeba mimba," walijibu kina mama hao.
Meneja mradi wa
afya na haki ya uzazi na ujinsia(Kijana Wa Leo) kutoka Amref Wilaya
ya Handeni, Dk. Aisha Byanaku alisema ni haki ya mgonjwa pia kuamua anapenda
kuhudumiwa na mtaalamu wa kiume au wa kike anapokwenda kupatiwa huduma hivyo
kuwataka wanaume kutokuwa na wasi wasi.
Alisisitiza kuwa
Amref kwa kushirikiana na halmashauri ,wataendelea kutoa elimu ya afya na
haki ya uzazi kwa wananchi wa wilaya ya handeni na kuwaomba wananchi kuendelee
kushirikiana na shirika kwani, Amref inaamini kuwa wananchi wenyewe ndio kiini
cha mabadiliko, kwani wao ndio wanayafahamu vizuri matatizo na changamoto za
Afya ya uzazi zinazowakabili, Amref ni muwezeshaji tu.
0 comments:
Post a Comment