Fidelis Butahe
Joseph Warioba |
WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba,
amesema kuteuliwa kwake na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (Sua) kusihusishwe na siasa wala msimamo wake, ukiwamo wa mchakato wa Katiba Mpya.
Alisema alishangazwa na wanaohoji uteuzi
huo bila kujiuliza umuhimu wa chuo hicho kwa Taifa wakati inafahamika kuwa
Watanzania wengi wanaendesha maisha yao kwa kutegemea kilimo, ufugaji na uvuvi.
“Hivi watu wanaelewa maana ya mkuu wa
chuo kweli? Hiki ni cheo cha heshima tu. Mtu anateuliwa aweze kusaidia mawazo.
Hii si kazi ya kulipwa mshahara, hakuna kitu kama hicho,” alisema Jaji Warioba
jana katika mahojiano na JAMBO LEO.
Alisema chuo hicho kinafundisha kilimo,
ufugaji na uvuvi, shughuli ambazo kwa kiasi kikubwa ndio zinaendesha maisha ya
Watanzania wengi.
“Nakwenda kusaidia ili chuo kitoe wataalamu
wa kusaidia sekta muhimu nchini. Sipendi kuona kila jambo likihusishwa na
Katiba, ina maana mimi sina mambo muhimu zaidi ya Katiba?” Alihoji.
Jaji Warioba ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa
na gazeti hili mikakati ya kusaidia chuo hicho na habari zinazoenezwa kupitia
mitandaoni kuwa uteuzi huo utamfanya ashindwe kusimamia mambo anayoamini,
likiwamo la Katiba inayotokana na maoni ya wananchi.
Baada ya Bunge Maalumu la Katiba
kumaliza kazi yake ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa huku baadhi ya maoni ya
wananchi yakiondolewa, Jaji Warioba alikuwa miongoni mwa waliokosoa uamuzi huo,
huku akihoji zaidi sababu za kuondolewa kwa miiko na maadili ya viongozi.
Mara ya mwisho kuzungumza na gazeti
hili, Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema atazungumzia mchakato wa Katiba-uliosimama
mwaka jana-kupisha Uchaguzi Mkuu, baada ya Serikali kueleza hatua ambazo zitakazofuata.
Hata hivyo, Novemba 4 Rais Magufuli kwenye
mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari alisema hakuna mahali alikoahidi kuendeleza
mchakato wa Katiba Mpya.
Msimamo wake kuhusu Katiba ndio uliibua
sintofahamu hiyo baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli takribani siku tano
zilizopita.
Alisema ni ajabu kuona baadhi ya wanahabari
wakimhoji kuhusu msimamo wake na uteuzi huo badala ya kumwuliza atakisaidiaje
chuo hicho.
Jaji Warioba ambaye alisisitiza
kuzungumzia uteuzi huo kiundani baada ya taratibu kukamilika, alisema chuo kina
umuhimu mkubwa kwa Taifa na kubainisha kuwa atahakikisha kinatoa wataalamu wa
kutosha.
0 comments:
Post a Comment