Maalim Seif Sharif Hamad |
KATIBU Mkuu wa CUF,
Maalim Seif Sharif Hamad, ameibuka na kutaja utatu unaojumuisha mwenyekiti wa
chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi na Jeshi la Polisi akieleza ndio unaoshirikiana kukihujumu chama hicho,
huku akibainisha mambo tisa anayoeleza kuwa ‘ushahidi wa ushirikiano’ na hujuma
hizo.
Akizungumza
katika mkutano na wahariri na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam
ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuibuka kwa mgogoro ndani ya chama hicho
baada ya Jaji Mutungi kumtambua profesa Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF, Maalim Seif alitumia
dakika 95 kueleza hujuma hizo na kudai zinalenga kukifanya chama hicho kutodai
haki ya kunyang’anywa ushindi wa Uchaguzi Mkuu Zanzibar.
Msemaji wa Jeshi la Polisi na Profesa Lipumba
walipotafutwa kujibu madai hayo ya Maalim Seif simu zao ziliita bila majibu,
hata walipotumiwa ujumbe mfupi kuhusu suala hilo na hadi gazeti hili linakwenda
mitamboni hawakujibu .
Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu na Msajili wa
Vyama vya Siasa walipotafutwa hawakupatikana.
Akiwa sambamba
na viongozi mbalimbali wa chama hicho, alisema hana ugomvi na Profesa Lipumba
na yupo tayari kukaa naye meza moja kueleza uongo wa mtaalamu huyo wa uchumi,
ikiwa ni pamoja na ukweli anaouficha kuhusu kujiuzulu kwake uenyekiti wa CUF
Agosti mwaka jana na uamuzi wake wa kutaka kurejea katika chama hicho.
Mbali na kukiri
CUF kupitia katika wakati mgumu kwa sasa, Maalim Seif alisema hujuma hizo zilizotokana
na ‘wakubwa’ kuchukizwa na kitendo cha chama hicho kuwasilisha vielelezo
Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC) vinavyowatuhumu viongozi wa Serikali
kutumia mamlaka yao vibaya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, zimesababisha chama hicho kutopata ruzuku ya
Sh milioni 117 kila mwezi, tangu Agosti mwaka huu.
“Mtiririko wa
matukio haya (tisa) yanaonesha wazi
hujuma hizi…, ni mambo
yanayoratibiwa kwa suhirikiano wa makusudi
kati ya msajili, polisi na Lipumba, “ alisema Maalim Seif.
Aliyataja mambo
hayo kuwa ni kuvamiwa kwa Mkutano Mkuu wa CUF iliofanyika Agosti 21, utekaji wa
wanachama na viongozi wa chama hicho, kuvamiwa kwa ofisi kuu iliyopo Buguruni,
kuvunjwa kwa ofisi za wilaya ya Bagamoyo na Mkuranga, wabunge na wajumbe wa
Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho kuzuiwa kufanya kikao cha ndani.
Mengine ni
kuzuiwa kufanyika kwa mkutano mkuu maalumu wilaya ya Tanga, utekaji wa mlinzi
wa chama hicho uliofanyika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuzuiwa kwa
kikao cha ndani mkoani Mtwara pamoja na walinzi wa Profesa Lipumba kutaka
kuzuia viongozi wa CUF kuingia chumba cha mahakama kuu hiyo.
Agosti 8 mwaka
jana Profesa Lipumba alitangaza kuachana na uongozi wa chama hicho, baada ya
CUF kukubaliana na Ukawa kumsimamisha Edward Lowassa kuwania urais.
Hata hivyo, Juni
mwaka huu Profesa huyo aliomba kwa barua kurejea kwenye wadhifa wake, ambao kwa
sasa unashikiliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro
aliyechaguliwa katika mkutano wa Baraza
Kuu la Uongozi la chama hicho.
Uamuzi wake huo
ulizua sintofahamu ndani ya CUF huku mkutano mkuu wa dharura wa chama hicho
uliofanyika Agosti 21 mwaka huu kumchagua mwenyekiti mpya ukivunjika baada ya
kundi la wafuasi wa chama hicho kuvamia na kufanikiwa kuzima mchakato wa kupiga
kura kumchagua mwenyekiti mpya, wakishinikiza Profesa Lipumba aruhusiwe kurejea
katika wadhifa huo.
Baada ya sakata
hilo Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho lilimvua uanachama Profesa Lipumba na
kuwasimamisha uanachama makada kadhaa wa CUF, jambo ambalo liliingiliwa kati na
Msajili wa Vyama vya Siasa aliyetoa waraka wa kumtambua Lipumba kuwa
mwenyekiti.
Kitendo cha
Lipumba kutambuliwa na kurejea katika chama hicho kilisababisha Baraza la
Wadhamini la CUF kufungua kesi Mahakama Kuu na kumshtaki profesa huyo Jaji Mutungi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), George Masaju.
Katika ufafanuzi
wake, Maalim Seif alisema Lipumba alivamia Mkutano Mkuu wa chama hicho
akiongozwa na polisi na kusababisha vurugu kubwa sambamba na uharibifu wa mali
lakini polisi haikuchukua hatua yoyote.
“Kumekuwa na
matukio kadha aya utekaji wa viongozi na wanachama wa CUF…, mkurugenzi wetu wa
fedha Joram Bashange alitekwa akiwa anatoka nyumbani kwake na walinzi wa
Lipumba, licha ya kukamatwa na kufikishwa polisi waliachiwa na gari walilotumia
nalo halipo kituo cha polisi buguruni,” alisema.
Alisema Septemba
24 mwaka huu, Lipumba na wafuasi wake walivamia ofisi kuu ya CUF iliyopo
Buguruni na kufanya uharibifu huku akipewa ulinzi mkali wa polisi.
“Polisi kazi yao
ni ulinzi wa raia na mali zao pamoja na kupambana na wahalifu lakini hivi sasa
wao ndio wanatetea wahalifu. Tunamuomba Mwigulu (Nchemba-Waziri wa Mambo ya
Ndani) kuingilia kati na kutizama watendaji walio chini ya wizara yake,”
alisema Maalim Seif.
Alisema tukio la
nne ambalo polisi imeshindwa kukamata wahusika licha ya kuwajua ni uvamizi
uliofanywa na wafuasi wa Lipumba wa kuvunja ofisi za chama hicho wilayani
Bagamoyo na Mkuranga.
“Wabunge na
wajumbe wa Baraza Kuu la uongozi la chama walizuiwa kufanya kikao cha ndani
Newala na kukamatwa walipokuwa Nachingwea,” alisema na kubainisha kuwa wakati
viongozi hao wakikamatwa, Lipumba anafanya vikao kama hivyo bila kukamatwa.
“Polisi walizuia
kufanyika kwa mkutano mkuu maalum wa wilaya ya Tanga kwa madai kuna pande mbili
zinavutana. Pia Novemba 10 mwaka huu mlinzi wa chama, Mohamed Said alitekwa
akiwa mahakama kuu na kupigwa sana na kunyang’anywa fedha na kupelekwa kuhojiwa
na Lipumba. Tukio hilo lilitokea mbele ya polisi,” alisema.
Alisema jeshi
hilo pia lilizuia kufanyika kwa kikao cha ndani mkoani Mtwara pamoja na walinzi
wa Lipumba kutaka kuzuia viongozi wa CUF kuingia ndani ya chumba cha mahakama
kufuatilia shauri lao, huku akimtaja mmoja wa walinzi hao kuwa ni Hassan
Kingwele.
Akijibu hoja
mbalimbali zilizoibuliwa na Lipumba, Maalim alisema msomi huyo anatumiwa na
dola na kubainisha kuwa anaficha ukweli
juu ya uamuzi wake wa kujiondoa CUF.
“Lipumba bado
hajasema sababu za kweli juu ya kujiuzulu kwake, yeye ndio alikuwa mwanzilishi
wa Ukawa katika Bunge Maalum la Katiba na ndio aliyemtafuta Lowassa na
kumshawishi awanie urais kupitia Ukawa,” alisema.
“Lowassa ilikuwa
ajiunge na NCCR kwa sababu ni chama kidogo ili CUF na Chadema tumuunge mkono
kwa mantiki hiyo iweje Lipumba aseme mimi sikumshirikisha ujio wa Lowassa ndani
ya Ukawa?”
Alisema yeye
hana ugomvi na Lipumba bali mtaalam huyo wa uchumi ana ugomvi na CUF, huku
akidai kuwa hivi sasa anatumia udini, ukabila na uzanzibari kukigawa chama
hicho.
“Hizi ni
jitihada za dola kunifanya nisidai haki kwa yaliyotokea Zanzibar…, hilo
halitawezekana nitaidai tu mpaka mwisho,” alisema.
0 comments:
Post a Comment