MWENYEKITI wa
kupambana na ujangili bungeni, Riziki Lulida, amesikitishwa na kasi ya kuuawa
kwa wanyamapori kwenye hifadhi nchini
wakiwamo tembo na simba.
Akizungumza na
waandishi wa habari mjini hapa jana, Riziki alisema iwapo kasi hiyo
itaendelea, miaka 10 ijayo Tanzania itakuwa haina tembo hata mmoja na
kuifananisha na Ivory Coast.
Riziki ambaye
pia ni Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Lindi kupitia CUF,
alisema kuuawa kwa wanyama hao kunasababishwa na wawindaji haramu kuwinda
katika maeneo ya mapito ya wanyama lakini pia wafanyabiashara kuachwa muda
mrefu wakiwinda kwenye hifadhi hizo.
"Ivory Coast,
Rwanda na Burundi zilijulikana huko nyuma kuwa na tembo wengi lakini hivi
sasa, hazina tembo huku akisema waliobaki Tanzania wanaelekea kumalizwa, kwani
kasi ya kuwaua ni kubwa,” alisema na kuongeza:
“Tanzania tuna
Niassa Selous Corridor, ambayo ilikuwa ikipitishia tembo kama ilivyo ya
Serengeti Masai Mara ya kupitishia nyumbu na pundamilia na wanyama wengine,
lakini ile ushoroba wa Niassa tangu nchi ipate uhuru, haujawahi kutangazwa.”
Hata hivyo,
alisema lazima Serikali kwa kushirikiana na Bunge na wananchi wasimamie kidedea,
kuhakikisha wanatoa sauti ili kuhakikisha tembo wanalindwa ipasavyo kwa
manufaa ya Taifa na vizazi vijavyo.
Riziki alisema
Tanzania inaonekana imeacha utalii endelevu wa kuangalia ushoroba wa tembo kutoka
Selous kwani hautangazwi ambapo matokeo yake miti imekuwa ikikatwa na kuondoa uhalisia
wa awali.
“Kwa nini wa Serengeti
unatangazwa halafu zingine kama vile Niassa hazitangazwi, huku shoroba za
wanyama zimekuwa zikionekana kuharibiwa maana hazina hata miti,tunatakiwa
kuheshimu tulivyonavyo,” alisisitiza Mbunge huyo.
Kuhusu kuuawa
kwa samba, alisema mnyama huyo ni miongoni mwa wanaopotea kwa kasi kutokana na
uwindaji haramu.
Alisema hivi
sasa ni tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo simba walionekana hadharani tofauti
na kwenye hifadhi.
"Zamani
ilikuwa ukipita njiani kwenye Kipiri kidogo tu lazima ukutane na simba, lakini
sasa hivi hawapo na hata ukipita kwenye hifadhi ,bado kumwona simba ni
shida," alisema.
Mbunge huyo aliitaka
Serikali kuweka ulinzi wa kutosha kwenye hifadhi ili kuhakikisha wanyama wote
wanalindwa kikamilifu ili kukuza vivutio vya utalii na kuvifanya kuwa endelevu na
kuliingizia Taifa pato la kutosha.
0 comments:
Post a Comment