Mwandishi Wetu
Samia Suluhu Hassan |
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia
Watanzania kwamba Serikali imeweka mipango na mikakati thabiti kukabiliana na
vifo vinavyosababishwa na saratani ya matiti na mlango wa kizazi kwa wanawake.
Samia ametoa kauli hiyo jana jijini Mwanza wakati akizindua
kampeni ya uchunguzi wa saratani ya matiti na mabadiliko ya awali ya saratani
ya mlango wa kizazi.
“Tanzania ikiwa ni nchi mojawapo Kusini mwa Jangwa la
Sahara, ina kiwango cha juu cha vifo vya saratani ya matiti na mlango wa
kizazi. Asilimia 60 ya vifo vyote vinavyotokea Kusini mwa Jangwa la Sahara
vinasababishwa na saratani hiyo,” alisema.
Alieleza kwamba vifo vingi vinatokana na uelewa mdogo,
imani potofu, gharama kubwa za matibabu, unyanyapaa na kuwepo kwa vituo
vichache wa kufanyia uchunguzi nchini ambapo kwa sasa tiba ya mionzi
inapatikana katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dar es Salaam pekee.
Makamu huyo wa rais alibainisha kuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, imepokea Sh. bilioni 5 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuviwezesha
vituo vitatu kwa kila halmashauri nchini ambavyo vitasaidia kuboresha huduma za
uchunguzi na matibabu ya mapema ili wanawake hasa wa vijijini waweze kupata
huduma hizo kwa urahisi na kwa ukaribu maeneo wanayoishi.
“Wote ni
mashuhuda wa namna saratani ya mlango wa kizazi inavyosababisha vifo vingi hali
ambayo hutokana na magonjwa wanaogundulika kuwa tayari wamefikia hatua
isiyotibika na kwa pamoja saratani hizi mbili husababisha zaidi ya asilimia 50
ya vifo vyote vya akinamama,” alisema.
Alisisitiza kwamba kwa sasa tayari kuna vituo takribani
300 vinavyotoa huduma za upimaji wa dalili za awali katika vituo vya afya kote
nchini na hivyo vituo vipya vitaongeza huduma endelevu ili kupunguza vifo
vitokanavyo na saratani.
Makamu wa Rais huyo pia ametoa wito maalumu kwa wanaume
kote nchini kuunga mkono kampeni hiyo kwa kuwaruhusu wanawake na wasichana
kwenda kupima saratani hiyo na amewapongeza na kuwashukuru wanaume wa mkoa wa
Mwanza kwa kuwasindikiza wake zao na watoto wao wa kike kwenda kwenye vituo vya
afya kwa ajili ya kupima saratani hiyo na kupatiwa tiba.
0 comments:
Post a Comment