Mkurugenzi wa J4 Express arudi mahabusu



Baltazar Mashaka, Mwanza

Basi la kampuni ya J4 Express
MKURUGENZI wa Kampuni ya Mabasi ya J4 Express, Jumanne Mahende (45) amerudishwa mahabusu katika Gereza Kuu la Butimba baada ya upande wa Jamhuri kuiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Mwanza, kuwa upelelezi wa shauri la mauaji linalomkabili haujakamilika.

Kesi hiyo ya jinai namba 19 ya mwaka jana ilitajwa na kuahirishwa juzi na Hakimu Mfawidhi, Wilbert Chuma baada ya Jamhuri kuomba ipangiwe tarehe nyingine.

Mwendesha Mashitaka, Wakili wa Serikali, Emmanuel Luvinga kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, alisema shauri hilo la mauaji linalomkabili Mahende lilikuja ili kutajwa lakini upelelezi bado haujakamilika na kuiomba Mahakama kupanga siku nyingine.

Kutokana na maombi ya upande wa Mashitaka, Hakimu Chuma aliahirisha shauri hilo hadi Novemba 28, litakapotajwa tena katika Mahakama hiyo na hivyo mshitakiwa alirudishwa mahabusu Butimba.

Mahende au J4, anakabiliwa na kesi ya mauaji akidaiwa kuua kwa kuwapiga risasi watu wawili eneo la Nyakato Boma, Nyamagana

Anadaiwa kuwa  Julai 13, mwaka jana, saa 4 usiku,  aliwaua kwa   risasi, Ali Mohamed, fundi ujenzi wa Igoma wilayani Nyamagana na Claude Steven, wa Nyasaka, Ilemela, Mwanza.

Baada ya tukio alikamatwa na polisi na kufikishwa mahakamani akishitakiwa kutenda kosa hilo na hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza mashauri ya mauaji.

Alisomewa mashtaka mara ya kwanza na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa Serikali, Subira Mwandambo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi,  Chuma.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo