Hussein Ndubikile
MAWAZIRI wa mikopo wa serikali za
wanafunzi wa elimu ya juu, wameilalamikia Bodi ya Mikopo ya ELimu ya Juu
(HESLB) kwa kuyaondoa baadhi ya majina ya wanafunzi waliokuwamo awali kwenye
orodha ya wanaostahili kupata mikopo hiyo.
Wakizungumza na gazeti hili katika ofisi
za bodi hiyo jijini Dar es Salaam walisema baadhi ya majina yaliyoletwa vyuoni
mara ya kwanza yameondolewa kwenye orodha mpya iliyowasilishwa hivi karibuni na
hiyo imeleta usumbufu mkubwa.
Naibu Waziri wa mikopo wa Chuo Kikuu cha
Sayansi na Tiba cha Muhimbili (MUHAS), Abubakar Hassan alisema kati ya
wanafunzi 316 waliopata mikopo hiyo awali, wanafunzi 19 waliondolewa katika
orodha mpya ya wanafunzi 290 iliyoletwa chuoni hapo.
Alisema pia katika orodha hiyo mpya kuna
wanafunzi 77 wenye mzazi mmoja wameondolewa kwa mfumo.
"Wanafunzi 316 pekee ndio waliopata
mikopo kati ya 396 wanaostahiki hata waliopata kuna waliopewa viwango vidogo
vya fedha za ada," alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo wanafunzi
ambao hawajui hatima yao ya kupata mikopo wamelazimika kurudi nyumbani kwani
bila kulipa ada hawawezi kupewa usajili.
Waziri wa Mikopo wa Taasisi ya
Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Fredson
Makundi alisema kati ya majina 147 yaliyokuja awali kuna wanafunzi wameondolewa
kwenye orodha ya wanafunzi 167 ya awamu ya pili.
Alisema walipouliza waliambiwa kuwa
majina hayo yameondolewa kutokana na kuwapo wanafunzi wengine wenye vigezo
zaidi yao.
Waziri wa Mikopo wa Chuo Kikuu cha Ardhi
(ARUSO), Gaspa Temba alisema majina ya wanafunzi 268 yaliyoletwa chuoni hapo
awali yamekatwa. Katika orodha mpya ya majina 827, wanafunzi 127 wa awali
hawakuonekana.
Naye Waziri wa Mikopo wa Chuo Kikuu cha
Mwalimu Nyerere, Kihaka Adam alisema chuo kina wanafunzi 1606 waliosajiliwa.
Kati yao wanafunzi 151 ndiyo waliopata mikopo, lakini ilipokuja awamu ya pili
ya wanafunzi 147, wanafunzi kumi waliondolewa.
Pia, alisema yatima 46 wenye vigezo
hawajapewa mikopo na hali hiyo imewafanya wanafunzi wengi kuahirisha mwaka wa
masomo.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Meneja wa
Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Omega Ngole alisema bodi hiyo ipo katika
hatua za mwisho za kushughulikia changamoto hiyo na huenda wakawekwa katika
orodha ya majina yaliyobaki inayosuburiwa kutolewa.
Alisema kuwa vyuo vikuu vyenye wanafunzi
wanaoendelea na masomo ambavyo vilikuwa havijawasilisha matokeo ya wanafunzi,
vimeanza kuwasilisha, huku akibainisha kuwa bodi inaendelea kushughulikia
malalamiko ya wenye uhitaji maalum waliokosa mikopo.
Ngole alisema kuwa tangu Jumanne vyuo
hivyo vimeanza kuleta matokeo ya wanafunzi wao na kwamba mchakato wa malipo
unashughulikiwa ili kuhakikisha wanafunzi wanapata fedha zao kwa wakati.
"Baada ya tamko hilo mwitikio
umekuwa mkubwa juzi tulianza kupokea matokeo yao na sasa tupo katika mchakato
wa kuyatuma majina ya mikopo katika vyuo vyao ili wapewe fedha zao,"
alisema.
Aliongeza kuwa tayari bodi hiyo
imeshapeleka malipo ya fedha mikopo benki na kwamba wameshatoa taarifa kwa
maofisa mikopo wa vyuo ili waende kuchukua vitabu vya kuwasainisha wanafunzi.
Alisisitiza kuwa wanafunzi wenye uhitaji
maalumu wakiwamo walemavu, yatima na wanaotoka katika familia duni wamekosa
mikopo kutokana na kutowasilisha vielelezo na kukosea kujaza fomu za kuomba
mikopo hiyo, hivyo bodi inatoa nafasi tena kwa wanafunzi hao kuomba.
Miongoni mwa vyuo hivyo ni Chuo Kikuu
cha Mtaktifu Joseph cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Mtakatifu John cha
Dodoma, Chuo cha CBE cha Dar es Salaam na Dodoma.
0 comments:
Post a Comment