*Ni kwa msimamo wake kuhusu Katiba Mpya
Suleiman Msuya na Fidelis Butahe
Tundu Lissu |
SIKU tatu baada ya Rais John Magufuli kueleza
bayana kwamba suala la Katiba Mpya si kipaumbele chake kwa sasa akitaka aachwe
ili ainyooshe nchi kwanza, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema
kiongozi huyo hawezi kunyoosha nchi bila kuwa na Katiba Mpya iliyotokana na
maoni ya wananchi.
Wakati Lissu akisema hayo, Mwenyekiti wa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damiani Lubuva amesema atatolea
ufafanuzi suala hilo siku za karibuni.
Lubuva na Lissu walieleza hayo
walipotakiwa kuzungumzia kauli ya Rais Magufuli kwamba kipaumbele chake ni
kuchapa kazi ili kuinyoosha nchi na mengine yafuate ikiwamo Katiba Mpya.
Magufuli alitoa kauli hiyo Novemba nne,
alipozungumza na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari siku moja kabla ya
kutimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani.
Lakini, Lissu alisema nchi haiwezi
kunyooka bila kunyoosha kwanza Katiba inayoiongoza ambapo alipendekeza uwepo wa
Katiba Mpya badala ya kuifanyia marekebisho iliyopo sasa.
“Tulishaondoka kwenye mjadala wa kuziba
viraka kwenye Katiba, tumeshakubaliana kwamba tunahitaji mabadiliko ya Katiba
yote si sehemu tu. Rais asidhani mtu akikalia kiti hicho basi neno lake ni
sheria ya nchi. Haiwezekani,” alisema.
Alisema mchakato wa Katiba Mpya
hautakiwi kuendelea ulipoishia kwa maelezo kuwa ikiwa hivyo nchi haiwezi kufika
popote.
“Katiba Inayopendekezwa ni kama imepakwa
rangi ya Katiba ya sasa. Inaonekana mpya lakini misingi yake ni ya Katiba ya
sasa…, kama Rais Magufuli anataka kunyoosha nchi, anapaswa kuirejea Rasimu ya
Jaji Warioba. Tuanzie hapo, zaidi ya hivyo atajidanganya na kuwadanganya
Watanzania,” alisema.
Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida
Mashariki alisema nchi haiwezi kuongozwa kwa matamko ya kiongozi mkuu pekee
bila kuangalia matatizo ya kisheria.
“Anafikiri akiamua yeye kama Rais
unafuata utekelezaji? Kuna matatizo mengine ya kikatiba…, hayawezi kubadilika
bila kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba. Kuna mambo ili yanyooke ni lazima uwe
na Katiba nzuri. Usipoyashughulikia hayo mengine yote hayatawezekana,” alisema
Lissu.
Kauli
ya Jaji Lubuva
Hata hivyo, Jaji Lubuva alipoulizwa
kuhusu mchakato wa Katiba Mpya na kauli ya Rais Magufuli alisema suala hilo linahitaji
kukaa na kulizungumza vizuri.
“Naomba upokee kuwa nimekuelewa ila kwa
sasa ninachoweza kusema nitatoa ufafanuzi mzuri kuhusu suala hilo kwani ni
jukumu la ofisi yangu,” alisema.
Alisema ni kweli baada ya Katiba Inayopendekezwa
kupigiwa kura na Bunge hatua iliyokuwa inafuata ilikuwa ni kuitisha Kura ya Maoni,
lakini ilishindikana kutokana na kuingiliana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Kabla ya Rais Magufuli kutoa kauli yake
kuhusu Katiba Mpya, siku za karibuni NEC iliwahi kueleza kwamba ipo katika
hatua mbalimbali za kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa mujibu wa sheria.
Alichosema
Rais
Katika kauli yake ya Novemba nne, Rais
Magufuli alisema wakati anaomba kura hakuweza kuzungumzia Katiba hivyo kwa sasa
kilichopo mbele yake ni kunyoosha nchi kwanza na Katiba mpya itakuja baadaye.
Akizungumzia uamuzi huo Mwanasheria wa
Chama cha Wananchi (CUF), Hashim Mziray alisema suala la Katiba mpya si suala
la Rais kutaka kwani lipo kisheria na kinachohitajika ni NEC kusimamia sheria
hiyo.
Mziray alisema kwa mujibu wa sheria hiyo
ni lazima Watanzania wapige kura ya maoni kukubali au kukataa Katiba hiyo hivyo
Rais ataamua kuendelea na Katiba ya zamani.
Alisema Katiba hiyo mpya ikifanikiwa
kupita itamsaidia Rais katika jitihada zake za kupambana na rushwa, ufisadi na
uwajibikaji kazini kwani kila kitu kipo tofauti na sasa ambapo anatumia mtazamo
wake katika baadhi ya mambo.
”Napenda kumkumbusha Rais kuwa Katiba
Inayopendekezwa sio suala la utashi wake ila ilipofikia ni utashi wa Watanzania
kupiga kura. Rais kusema kuwa kwa sasa sio kipaumbele (Katiba Mpya) chake ni
sawa na kuingilia NEC ambayo kisheria inapaswa kutekeleza mchakato huo,”
alisema.
Mwanasheria huyo alisema iwapo Rais
anasema kuwa Katiba mpya si kipuambele chake atakuwa anapotosha umma kwa kile
alichodai kuwa suala la kuhamia Dodoma halipo katika ahadi zake wala Ilani ya
CCM ila ametangaza kuhamia huko.
Rais wa Chama cha APPT-Maendeleo, Peter
Mziray alisema ni wajibu wa tume kusimamia majukumu yake bila kuogopa na kwamba
kama haitachukua hatua za kuandaa upigaji kura ni wazi kuwa inavunja sheria.
“Kusema kweli hata mimi nimestuka sana
kwa kauli ya Rais kwani ameingilia madaraka ambayo si yake suala la kura ya
maoni lipo katika mamlaka nyingine na kutopigwa kura wakati ule mimi
nilishiriki kumuomba Lubuva aihirishe mpaka uchaguzi upite Rais hakuwa na
nafasi tena,” alisema.
Mchakato wa Katiba mpya ulianza mwaka
2012 ambapo Rais Jakaya Kikwete aliunda tume ya wajumbe 30 kati yao 15 walitoka
Tanzania Bara na 15 walitoka Zanzibar Mwenyekiti wake akiwa Jaji mstaafu Damian
Lubuva na Makamu Mwenyekiti Jaji mstaafu Agustino Ramadhan.
Tume hiyo ilifanikiwa kuzunguka nchi
nzima kupokea maoni ya Watanzania wa kada zote ambapo ilitengeneza rasimu ya
kwanza na kuiwasilisha kwa Rais ambapo ilipelekwa kwa mabaraza mbalimbali ngazi
ya wilaya na kujadili,
Baadae tume ya Jaji Warioba ilitengeneza
rasimu nyingine ya pili na kumkabidhi Rais Kikwete ambaye aliteuwa wajumbe wa
wabunge la Katiba kwa kushirikiana na wabunge wa kuchaguliwa kutoka Bunge la
Muungano na Baraza la Wawakilishi walijadiliana na kuja na Katiba pendekezwa
ambayo kwa sasa inasubiriwa kupigiwa kura ya maoni ya ndio au hapana.
0 comments:
Post a Comment