'Makaburi' manne anayohofia Rais



Suleiman Msuya na Fidelis Butahe

Rais Magufuli akizungumza na wahariri Ikulu
WANASIASA na Wasomi wametaja makaburi manne ambayo Rais John Magufuli anapaswa kuyafukua, likiwemo la Katiba Mpya, wakipingana na kauli ya kiongozi huyo mkuu wa nchi kwamba hakuingia Ikulu kufukua makaburi.

“Katiba mpya ndio kaburi linalopaswa kufukuliwa na iwapo tunaamua basi ile rasimu ya Warioba (Jaji Joseph-Mwenyekiti wa Iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba) ndio inapaswa kuwa Katiba ya nchi. Itafaa kufufua makaburi mengine,” alisema Zitto Kabwe, Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo.

Wakati Zitto akieleza hayo, Katibu Mkuu wa Chadema, Vicent Mashinji alisema kauli ya Rais Magufuli kuhofia ‘kufua makaburi’, inaweza kuwa mwanzo wa kushindwa vita dhidi ya ufisadi, jambo ambalo lilipingwa na msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, aliyesema “Rais anafanya mambo aliyojipangia, sio kufukua ya nyuma.”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili waliyataja madudu mengine yanayohitaji kufukuliwa na Rais kuwa ni sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, ufisadi katika mifuko ya hifadhi za jamii pamoja na kashfa ya Meremeta.

Ijumaa iliyopita, siku moja kabla ya kutimiza mwaka mmoja madarakani, Rais Magufuli alizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini na kuwataka Watanzania wamwache anyooshe nchi kwanza ndio mengine yafuate, kutokana na kukutana na ‘madudu’ ambayo mengine hakuyatarajia, huku akitaja mfano wa mapya matatu aliyokutana nayo.

Alitaja madudu hayo kuwa ni kupotea kwa meli 60 bandarini, wanasiasa kukopa katika mabenki na kutishia kufilisika kwa taasisi hizo pamoja na mkopo wa dola za Marekani milioni 20, sawa na zaidi ya Sh bilioni 40, kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda mkoani Lindi, ambazo zimeyeyuka na kiwanda husika hakipo.

Wasomi na wanasiasa hao walilieleza JAMBO LEO kuwa makaburi hayo yaliyotajwa na Rais Magufuli si lolote si chochote mbele ya hayo manne waliyodai kuwa ndio msingi wa kuirejesha Tanzania katika mstari ulionyooka.

Katika maelezo yake Zitto alisema  maoni yaliyokuwemo katika rasimu ya Jaji Warioba yaliyoondolewa kwa kiasi na wabunge wa CCM na kuingiza maoni yao binafsi katika Katiba Inayopendekezwa,  ndio yaliyokuwa na majibu ya masuala yote yanayowasumbua viongozi kwa sasa katika kufanikisha majukumu yao.

Alibainisha kwamba nchi ilifanya makosa kuingia katika Uchaguzi Mkuu bila Katiba mpya, jambo alilodai huwafanya walioingia madarakani kwa Katiba iliyopo, kujisahau kuwa kuna kilio cha kudai Katiba Mpya.

Alisema iwapo Katiba Iliyopendekezwa ingepita pamoja na upungufu wake, ingesaidia kwa kiasi fulani kuleta mabadiliko nchini, tofauti na Katiba ya sasa ambayo inampa madaraka makubwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wake, Mashinji alisema kaburi ambalo lipo wazi ila limemshinda ni ufisadi wa zaidi ya Sh bilioni 205 unaodaiwa kufanywa kupitia kampuni ya Meremeta iliyokuwa ikimilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

“Meremeta imelalamikiwa miaka yote, lakini hakuna ufumbuzi wowote. Rais ameonesha dhahiri kuwa vita ya ufisadi imemshinda. Viatu alivyovaa vinampwaya…, alishaingia katika mfumo wa CCM wa ‘upigaji’ kwani makaburi yapo mengi ila amekiri kuwa hawezi kuyafukua.” alisema.

Alisema ndani ya CCM hakuna mtu ambaye atatokea na kufanya mabadiliko katika nchi, huku akijipigia chapuo kuwa wapinzani wanapaswa kuungwa mkono kwa maelezo kuwa wao ndio vigogo wa kupambana na ufisadi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Josia Kibira cha mjini Bukoba, Dk Azavel Lwaitama alisema kinachomsumbua Rais Magufuli ni kuingia madarakani na kukumbana na mfumo ambao ni zao la kuwa na Katiba iliyopitwa na wakati, inayokifanya chama kilichopo madarakani kung’ang’ania kutawala.

“Rais anapaswa kukaa meza moja na Jaji Warioba pamoja na wajumbe wa tume ili wamueleze nini maana ya msingi wa Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya wananchi.  Hapo ndio anaweza kufanya mabadiliko ya nchi,” alisema.

”Unajua hata wakati wa utawala wa Nyerere (Julius-Rais wa Awamu ya Kwanza) changamoto hizo zilikuwepo, lakini sababu kubwa ni mfumo uliongiza vyama tawala madarakani na njia ya kutatua changamoto hiyo ni kuviondoa madarakani au Katiba mpya.”

“Katiba ndio kaburi la kufufua. Rais kuzungumza kwa mafumbo si njia sahihi ya kusaidia Watanzania kwani ni wazi ameonesha kuanza kushindwa kutekeleza lengo la kusafisha nchi kwa mujibu wa Katiba,” alisema Profesa Abdallah Safari.

Katibu wa Habari na Uenezi Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila alitaja sakata la Escrow na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kusisitiza kuwa ni mambo ya msingi yanayopaswa kufukuliwa.

Alibainisha kuwa licha ya Rais kuitambua kiundani kashfa ya Escrow, ameonesha kushindwa mapema jambo ambalo linawakatisha tamaa wananchi walioanza kujenga imani naye.

“Mifuko ya hifadhi za jamii ina uchafu mwingi sana, lakini kwa kuwa CCM imekuwa ikiitumia mifuko hiyo ni ngumu kwake (rais) kuishukia na kuibua madudu yake,” alisema.

“Nadhani unaona hadi leo Tanesco linaendelea kuilipa IPTL na kati ya malipo hayo nusu zinaenda kampuni ya Simba Trust ambayo mpaka sasa hatujui wamiliki wake ni akina nani? Hakuna maelezo ya kutosheleza yanayotolewa kuhusu suala hilo.”

Kafulila ambaye aliibua sakata la Escrow, alibainisha kuwa kauli hiyo ya Rais inakatisha tamaa kwa sababu wananchi wamekuwa wakimuombea ili aweze kutekeleza majukumu yake vizuri, “kesi kubwa zitachinjwa maana mwenye nchi ameshaamua kutofukua makaburi.”

Alisema wakati mifuko ya hifadhi ikiwa na kashfa waliokuwa viongozi wake wanateuliwa kushika nafasi mbalimbali, huku wanaoshughulikiwa wakiwa watu wa ngazi za chini.

Akizungumzia kauli hiyo ya Rais Magufuli, Ole Sendeka alisema, “Rais anatakiwa aende mbele ili kunyoosha nchi na si kurudi nyuma kwani kunamchelewesha…, hakuna kashfa ambayo itaachwa kama kuna ushahidi kwa kisingizio cha kutofufua makaburi,” alisema.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo