Peter Akaro
Dk. Ali Mohamed Shei |
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi (SMZ), Dk. Ali Mohamed Shein amesema Mahakama ya Kimataifa ya
Makosa ya Jinai (ICC), haina uwezo wa kuhoji uchaguzi wa visiwa hivyo.
Aliwataka wananchi wa Kisiwa cha Pemba
kupuuza taarifa kwamba kuna Serikali nyingine itaingia madarakani visiwni humo,
badala yake waendelee kufanya kazi kwa bidii kwa kushirikiana na SMZ.
Taarifa ya Ikulu ya Zanzibar iliyotolewa
jana kwa vyombo vya habari ilisema Dk. Shein amewaambia wananchi kisiwani humo
kwamba Serikali anayoiongoza iko madarakani kwa mujibu wa Katiba na inaendelea
kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM hadi mwaka 2020.
“Wanaisingizia ICC, wanadanganya tu
haina uwezo huo wa kuhoji uchaguzi wa Zanzibar ulioendeshwa kwa mujibu wa
Katiba yake,” alisema Dk. Shein ambaye yuko kisiwani Pemba kwa ziara ya kikazi.
Dk Shein alionyesha kukerwa na uzushi
huo. Aliwakumbusha wanasiasa wanaoeneza uvumi wa kuingia madarakani kwa
Serikali nyingine akisema kiongozi anayetaka ushindi ni lazima ashiriki
uchaguzi, achaguliwe na wananchi na atangazwe na Tume ya Uchaguzi kuwa ni
mshindi.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo
na mimi ndie Rais. Ni serikali halali kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1984,”
alisema.
Aliwahakikishia wananchi hao kwamba
hakuna nchi wala taasisi ya ndani au ya nje inayoweza kuiondoa Serikali iliyopo
sasa, wala hakuna wa kuhoji uhalali na uwepo wake.
“Hakuna nchi inayoapisha Rais mara
mbili, mimi sina wasiwasi na Serikali yenu haina wasiwasi na tuko hapa
kuwatumikia ili kuendeleza nchi yetu, maneno haya yanawapotezea muda wenu tu,”
alisema na kufafanua:
“Serikali hii ni ya wananchi
waliyoichagua na wasioichagua, waliopiga kura na wasiopiga kura. Wapo
wanayoitaka na wasiyoitaka, wote hao wanafanya kwa hiari yao, lakini mwisho wa
yote kwa kuwa tayari imewekwa madarakani na wananchi wenyewe kupitia uchaguzi
ulioendeshwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar hawana budi kuitii.”
Alibainisha kuwa ni tamaa za baadhi ya
wanasiasa waliowashawishi baadhi ya watu wasishiriki katika uchaguzi wa marudio
ambao uliitishwa kwa mujibu wa Katiba lakini sasa baada ya kuona
waliyoyatarajia hawakuyapata sasa wanawazubaisha wananchi kwa kupita mitaani na
maneno yasiyo na msingi.
Dk. Shein aliyewasili kisiwani Pemba juzi
na kuzungumza na wananchi wa Mji wa Chake Chake wakati wa uzinduzi wa jengo la
Mahakama Kuu na wananchi wa Kengeja wakati alipozindua dakhalia ya wasichana ya
skuli ya sekondari ya ufundi Kengeja.
Jana alizungumza na wananchi wa
Micheweni wakati wa kukagua ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya
wilaya hiyo na wananchi wa Gando wilaya ya Wete wakati akizindua madarasa ya
skuli ya Chekechea ya Gando.
Tangu kumalizika uchaguzi wa marudio
uliofanyika mwezi Machi mwaka huu, kumekuwepo na uvumi unaoenezwa na baadhi ya
viongozi wa upinzani kuwa kutafanyika mabadiliko ya uongozi kwa msaada wa
mataifa ya nje.
Dk. Shein yupo kisiwani Pemba kwa ziara
ya siku tano kukagua shughuli za maendeleo ambapo kesho anatarajiwa kukagua
ujenzi wa barabara kadhaa zinazoendelea kujengwa katika mkoa wa Kusini Pemba.
0 comments:
Post a Comment