Magendela Hamisi
Bondia Thomas Mashali |
KINONDONI makaburini ndiyo makazi ya
mwisho hapa duniani ya bondia Thomas Mashali, ambaye enzi za uhai wake alijipachika
jina la Simba Asiyefugika.
Vurugu zake zilianzia mtaani hadi kuwa
bingwa wa dunia wa masumbwi kwa mkanda wa UBO na kuiweka Tanzania katika ramani
nzuri ya mchezo huo.
Mashali naamini kwa kila ambaye alikuwa
akimfahamu atakuwa na mengi ya kusimulia na kufunga ukurasa wa maisha ya nyota
huyo wa ngumi za kulipwa nchini ambaye Oktoba 31, mwaka huu alipoteza maisha
baada ya kushambuliwa kwa mapanga na matofari Kimara jijini Dar es Salaam.
Hakika kifo cha Mashali ni pigo kwa
wadau wa michezo nchini, pia mazingira ya kifo chake yataendelea kuumiza vichwa
vya wadau wa michezo kwani kabla ya tukio inadaiwa alifuatwa na mmoja wa watu
aliokuwa akifahamiana naye ili akamsaidie kupata haki yake.
Kwa mujibu wa mashuhuda huo ndiyo ukawa
mwanzo wa safari yake ya mwisho bondia huyo ambaye Novemba 19, mwaka huu
alikuwa apigane pambano la kirafiki dhidi ya Denis Ronald nchini Ujerumani
lililokuwa la kirafiki kwa ajili ya kumweka sawa na pambano lake la kutetea
mkanda wake wa UBO dhidi ya Chimwemwe Desemba 26, mwaka huu.
Bondia huyo baada ya kuwa mtukutu uraiani
katika viunga vya Tandale, Promota wa ngumi za kulipwa nchini, Kaike Siraji
akamtoa mtaani na kumwingiza katika mapambano ya kulipwa na la kwanza
alilicheza Novemba 27, 2009 dhidi ya Hamadu Mwalimu katika ukumbi wa Texas
Manzese Dar es Salaam na kushinda kwa KO.
Waswahili wanamsemo unaosema nyota njema
huonekana asubuhi kwani baada ya kushinda pambano hilo kwa KO, Aprili 4, 2010
akapanda ulingoni kwenye ukumbi wa Magomeni Kondoa kuzichapa na Karama
Nyilawila ambaye kwa wakati huo alikuwa katika kiwango kizuri na kuogopwa na
mabondia lukuki ndani na nje ya nchi na kufanikiwa kutoka naye sare.
Pambano lake la tatu alicheza na Robert
Mrosso katika ukumbi wa DDC Kariakoo na kushinda kwa KO, Desemba 9, 2010 siku
ya sherehe za Uhuru wa Tanganyika alifanikiwa kushinda pambano lake la nne
dhidi ya George Dimosso.
Harakati za kujiweka sawa katika ramani
ya dunia ziliendelea ambapo Aprili 9, 2012 alimtwanga Selemani Said kwa pointi
na Juni 24, 2012 alimtwanga Maisha Samson kwa KO, Oktoba 14, 2012 alimtwanga
bondia Med Sebyala na kubeba ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati katika ukumbi
wa Friends Corner Manzese Dar es Salaam.
Januari 12, 2013 alitetea ubingwa huo
baada ya kumtwanga Bernard Mackoliech kwa KO katika ukumbi wa Friends Corner,
Manzese na baada ya hapo Mei Mosi 2013, akapanda ulingoni kuwania mkanda IBF
Afrika, uzito wa kati dhidi ya Francis Cheka na kupoteza kwa KO.
Julai 7, 2013 alipanda ulingoni katika
pambano lake la 10, tangu aingie katika ngumi za kulipwa na kufanikiwa
kumtwanga Patrick Amote wa Kenya katika pambano lisilo la ubingwa lililochezwa Uwanja
wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam.
Baada ya kushinda pambano hilo, Agosti
30 alipanda ulingoni kuzichapa na Mada Maugo 'Mbunge wa Rorya' na kushinda kwa
pointi na kupata nafasi ya kupanda ulingoni nchini Urusi Novemba 16, kuwania
mkanda wa Mabara wa UBO dhidi ya Arif Magomedov na kupoteza kwa KO.
Simba Asiyefugika alipanda tena ulingoni
Machi 29, 2014 dhidi ya Japhet Kaseba kuwania mkanda wa UBO Afrika uzito wa juu
na kufanikiwa kushinda kwa pointi, miezi mitano baadaye akapoteza pambano
lisilo la ubingwa dhidi ya Mada Maugo, ambaye alilipa kisasi kwa pointi.
Kutokana na kupoteza pambano hilo,
akaendelea kujipanga na Oktoba 5, mwaka huo huo katika Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga akafanikiwa kumtwanga Alibaba Ramadhani kwa TKO katika pambano
lisilo la mkanda. Novemba Mosi katika ukumbi wa Friends Corner akamtwanga kwa
TKO, Henry Wandera.
Machi 7, 2015 katika ukumbi wa Vijana,
Dar es Salaam alimtwanga kwa TKO katika pambano lisilo la ubingwa ambalo alijiweka
sawa dhidi ya Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’, kwa pointi kwenye Uwanja wa Ndani wa
Taifa.
Baada ya kushinda pambano hilo, bondia
Selemani Said akaamua kujiuliza tena na kupanda ulingoni Juni 6, na Mashali akashinda
kwa KO, Pia, Agosti 29 alipanda ulingoni kuzichapa na Ibrahim Tamba na kushinda
kwa alama.
Kutokana na kufanya vema, akaona
ajiulize tena dhidi ya Cheka akiwa chini ya Kocha Ramadhani Uhad 'Rama Jah'
katika pambano lililochezwa Desemba 25, mkoani Morogoro na kufanikiwa kushinda
kwa alama na kupata nafasi ya kuwania ubingwa wa mabara uzito wa super middle
nchini Urusi Machi 5, mwaka huu dhidi ya Apti Ustarkhanov na kupigwa kwa KO
raundi ya pili.
Mashali baada ya kupigwa katika pambano
hilo la uzito wa kati alirejea nchini kujipanga upya na Mei 14, akapanda
ulingoni ukumbi wa Uwanja wa Ndani wa Taifa dhidi ya raia wa Iran, Sajjad
Mehrabi na kuwania mkanda wa Dunia wa UBO uzito wa super na kufanikiwa kushinda
na kunyakua ubingwa huo.
Ushindi huo ulimpa kiburi Mashali enzi
za uhai wake na kusaka pambano lingine kwa maana nia yake ili kuidhihirishia
dunia kuwa yeye ni Mtanzania anayefanya vema katika ndondi na kufanikiwa
kupanda ulingoni Julai 9, nchini China dhidi ya Zulpikar Maimaitiali na
kupoteza kwa TKO.
Pambano lake la mwisho hadi mauti
yanamkuta alipigana Septemba 12, katika ukumbi wa Chee Kwa Chee Pub, Bagamoyo
mkoani Pwani na kumtwanga Shabani Kaoneka.
Siku chache Mashali alizungumza na
mwandishi wa makala haya na kuweka wazi mikakati yake ya kuhamia Bagamoyo akiamini
huko kutampa mafanikio zaidi.
Maneno
yake ya mwisho kwa JAMBO LEO
"Ndugu yangu nimeweka kambi
Bagamoyo kwa ajili ya pambano langu la Desemba 26, pia moja ya mikakati yangu
ni kuhakikisha nahamia Bagamoyo nimekutana na baadhi ya wadau ambao naamini
nikiwa nao maisha yangu yatafanikiwa zaidi.
Pia, mikakati yangu mingine ni
kuhakikisha nafanya vema katika masumbwi na ndiyo maana nimeamua kuingia mapema
kambini kwani nina muda wa miezi mitatu na lengo ni kuangalia je, nikifanya
mazoezi kwa kipindi kirefu hali inakuwaje kwani mara nyingi ninapokuwa na
pambano naingia kambini kwa mwezi mmoja."
Mashali alizikwa Novemba 2, mwaka huu
katika makaburi ya Kinondoni.
Mungu ailaze roho ya Mashali, mahali
pema peponi amen.
0 comments:
Post a Comment