Mariam Cyprian, Tanga
CHAMA cha Wananchi (CUF) wilayani hapa kimetoa tamko la
kutomtambua Mwenyekiti wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, na kwamba hakitampokea
katika ziara yake.
Lipumba anatarajia kuanza ziara mkoani hapa kesho huku uongozi wa chama hicho ukisisitiza
kutambua uamuzi wa Mkutano Mkuu uliomwondoa
madarakani na wa Baraza Kuu kumvua uanachama.
Mwenyekiti wa CUF wa Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe alitoa tamko
hilo jana akieleza kuwa hawatakuwa tayari kukaidi Katiba ya Chama chao na
kwamba hawatampokea na hakuna maandalizi yatakayofanyika kumpokea.
"Tumeambiwa Lipumba ana dhamira ya kufanya ziara mkoani hapa.
Sisi kwa uamuzi wa Baraza hatumtambui, wala hatujaandaa maandalizi ya kumpokea.
“Wilaya za Korogwe na Muheza ndizo zimesema atazitembelea, lakini
sisi hatuko pamoja nao na watakaompokea wataingia kwenye mgogoro mwingine kwa
sababu hatambuliki," alisema Jumbe.
Mwenyekiti huyo pia alizungumzia mgogoro baina yao na CCM kutokana
na sakata la umeya ambapo alisema hatima
ya mgogoro huo itajulikana baada ya mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba
29.
Alisema kutokana na sakata hilo walitoa malalamiko kwa viongozi
mbalimbali lakini hakuna hatua zozote zinazoendelea, hivyo Kamati ya
Utendaji iliwataka madiwani wa chama hicho kutohudhuria kikao chochote cha Halmashauri
hadi itakapotoa uamuzi.
"Tumetoa malalamiko yetu kwa viongozi wa CCMna lengo letu
ilikuwa tuonane na Rais lakini tulimpata
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa aliyetwambia kuwa atalifanyia kazi, lakini sasa
tumeamua kupeleka malalamiko yetu kwa wenye chama na wao ndio watakaotoa uamuzi
juu ya mgogoro huo.
“Hivyo tumeitisha mkutano ambao utakuwa na wajumbe 440 ambapo tuna
imani kuwa tatizo letu litakwisha Oktoba 29,” alisema Jumbe.
0 comments:
Post a Comment