Celina Mathew
BARAZA la Vijana la Chadema (Bavicha)
limetaja moja ya sababu za wanafunzi wa elimu ya juu kukosa mikopo kuwa ni
Serikali kushindwa kulipa deni la Sh60 Bilioni inayodaiwa na Bodi ya Mikopo ya
Elimu ya Juu.
Mwenyekiti wa Bavicha, Protrobas Katambi,
alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakipiga simu na kueleza kuwa wengi
wao wameshindwa kupata mikopo katika mwaka huu wa masomo.
Alitaja baadhi ya vyuo ambavyo wanafunzi
wake walikuwa wakiipigia simu na kueleza tatizo hilo kuwa ni Chuo Kikuu cha
Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu Huria (OUT), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), na
vinginevyo.
Alisema kutokana na changamoto hiyo ni dhahiri
kuwa kuna vyuo vipo hatarini kufungwa hivyo ni vyema serikali ikafanyia kazi
ili wanafunzi hao wapewe mikopo na kuondokana na adha hiyo.
Alisema kutokana na changamoto hiyo
Bavicha limetoa siku saba na kumtaka
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako atoe
ufafanuzi kuhusu suala hilo ili kuwezesha wanafunzi hao kupata mikopo na waweze
kurudi vyuoni kuendelea na masomo yao.
“Hali ya elimu kwa wanafunzi wa elimu ya
juu, vyuo vipo hatarini kufungwa hivyo tunamtaka Ndalichako aseme kuwa suala
hilo litafanywaje ili wanafunzi hao waweze kupewa mikopo na kama atashindwa
amwambie waziri mkuu atoe tamko na yeye akishindwa basi Rais apewe jukumu
hilo,” alisema.
Aliongeza kuwa kuna baadhi ya wakuu wa
vyuo wanatamani kujitokeza hadharani kuzungumzia suala hilo lakini wanaogopa
kutumbuliwa na Rais kutokana na kuwa wataonekana wanaichongea serikali.
Aidha alisema Bavicha limepokea kwa
mshtuko mkubwa taarifa ya kuwa kupitia utawala uliopo sasa zaidi ya nusu ya
wanafunzi waliodahiliwa kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo
2016/17 wako katika hatari ya kukosa fursa ya kupata elimu hiyo kwa sababu
ambazo hazieleweki hadi sasa.
Alisema kwa mujibu wa taarifa za vyombo
vya habari na vyanzo vingine Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) imeweza kudahili
wanafunzi wapya 58,000 kwa ajili ya elimu ya juu katika vyuo mbalimbali nchini
kwa mwaka huu.
Alisema katika hali ambayo inajulikana
itaumiza wanafunzi wengi na kuwasikitisha watanzania taarifa zilizothibitishwa
na serikali kupitia Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo zaidi ya nusu ya wanafunzi
waliodahiliwa na TCU kusoma elimu ya juu hawatapata mikopo.
“Hili ni jambo kubwa na zito kwa sababu
linagusa moja ya misingi muhimu ya taifa lolote lenye ndoto ya kutaka
kuendelea, achilia mbali kuwa taifa lenye uchumi wa kati unaotegemea
viwanda,”alisema.
Alisema hali hiyo inaonesha kuwa
Mkurugenzi huyo anajaribu kuficha jambo fulani na kwamba hadi sasa bodi hiyo
imetoa mikopo kwa wanafunzi 3,966 tu ambapo ni sawa na asilimia 6 tu kati ya
wanafunzi wote waliopata udahili wa kusoma elimu ya juu kwa mwaka huu.
Alisema maana yake ni kwamba kuwakopesha
vijana 24,000 ili wasome bado ni ahadi ya maneno, lakini uhalisia uliopo kwa
vitendo ni kwamba serikali ina uwezo wa kuwakopesha vijana 3,966 pekee nchi nzima.
Alieleza kuwa idadi hiyo ambayo serikali
imeweza kuwakopesha mikopo haifiki hata nusu ya jumla ya wanafunzi wanaopaswa
kudahiliwa na mojawapo ya vyuo vikuu vikubwa kikiwemo cha UDSM.
Aidha alisema utafiri huo umeendelea
kuonesha kuwa tangu HESLB imeanza utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanafunzo
wamekuwa wakipewa matumizi ya vitu vitatu tu ambavyo ni ada, malazi na chakula.
Alisema kinachozidi kushangaza na kuibua
maswali mengi ambalo limejificha ni kuwa hata asilimia sita ambao bodi
imeshawapa katika vyuo vingi wamepata fedha kwa ajili ya chakula na kulala tu
hawajalipwa ada.
Alifafanua kuwa hali hiyo inaonesha
kwamba serikali hadi sasa wiki tatu tangu vyuo vifunguliwe sio tu kwamba
imeshindwa kuwakopesha wanafunzi wote wanaostahili kupata mikopo kwa ajili ya
elimu ya juu, bali hata kulipa fedha za ada kwa wanafunzi hao ambao tayari
imeshawakopesha.
Alisema hali hiyo ikiendelea wazazi
watarajie kuona vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu vikifungwa kwa
sababu vitakuwa haviwezi kujiendesha vyenyewe.
Katambi aliongeza kuwa taarifa za
wanafunzi kukosa mikopo zinzonesha kuwa serikali iko katika hali mbaya ya
kifedha na hivyo inahitaji msaada wa fikra nje ya chama tawala kuikwamua
vinginevyo wajiandae kwa mwendelezo wa janga kubwa zaidi kwenye sekta ya elimu.
Alisema ni vyema Rais akarejea kwenye
ahadi yake aliyoahidi wananchi kipindi cha kampeni kwa kujitokeza hadharani na kueleza hatma ya
wanafunzi hao waliokosa mikopo.
“Rais Magufuli anapaswa kuwaeleza
watanzania ikiwa ameshindwa utekelezaji wa ahadi yake ya elimu bora au akubali
kuwa yeye ni muongo kwa sababu wakati wa kampeni alimnukuu kuwa ‘Eti niwe rais
halafu nisikie wanachuo wamekosa mikopo au wamecheleweshewa mikopo yao,
watanijua mimi ni nani, kitu chenyewe kinaitwa mikopo halafu unachelewesha’.
Alisema kuwa endapo suala hilo
halitafanyiwa kazi wataungana na viongozi wa serikali za wanafunzi katika vyuo
vikuu vyote nchini ili kudai haki ya wanafunzi hao.
Aliahidi kuwa watafanya hata maandamano
na kuwaomba wazazi nchi nzima wenye wanafunzi katika vyuo hivyo kuungana na
watoto wao kudai haki kwani umoja wao ni muhimu.
Aidha alizitaka taasisi mbalimbali za
kutetea haki za vijana, asasi za vijana na mtandao wa wanafunzi Tanzania
kujitokeza hadharani na kuwapigania vijana hao katika kuhakikisha wanapata haki
yao ya msingi ya elimu.
Aliishauri serikali kutumia misaada
inayotolewa na wafandhili na wadau mbalimbali kwa ajili ya maafa yaliyotokea
Bukoba zikatumika kuwalipa wanafunzi hao waliokosa mikopo.
Katika hatua nyingine Bavicha kimeitaka
Ikulu kupunguza matumizi yasiyo na msingi ili kuepuka matumizi mabaya ya fedha
jambo lililosababisha matumizi hadi Septemba kufikia zaidi ya sh. Bilioni
1.246,837,833.
Alisema kuwa taarifa anazo na kwamba
endepo zitahitajika kuthibitisha wapo tayari kwa ajili ya kuziweka hadharani
ili wanachi wazione.
Gazeti hili lilimtafuta viongozi wa
wizara husika kutole ufafanuzi suala hilo
simu zao ziliita bila kupokelewa.
0 comments:
Post a Comment