Mwandishi Wetu
Tundu Lissu |
MBUNGE wa Singida Mashariki na
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, amesema vitendo vya uminyaji
demokrasia na ubabe vinavyofanywa na watawala vinawamaliza.
Lissu alisema hayo kwenye waraka wake aliouandika
baada ya kudai kupokea ujumbe tofauti 297,576 kutoka kwa wananchi wakihoji sababu za vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Chadema kutochukua hatua kwa wanayotendewa.
Alitaka wananchi na wafuasi wa vyama
vyao kuvuta subira kwa kile anachoamini kuwa hakuna lisilo na mwisho katika
dunia.
“Mnakumbuka Rais wa zamani wa Ivory
Coast, Laurent Gbagbo alivyoshindwa uchaguzi akalazimisha tume ya uchaguzi imtangaze
ameshinda, na tume kwa sababu haikuwa huru, ikamtangaza mshindi badala ya Alassane
Ouattara na sasa ameshitakiwa kwenye Mahakama ya ICC, kwa hiyo haya ni mambo ya
muda tu,” alisema.
Alitolea mfano wa pili wa Samwel Doe wa
Liberia ambaye alipinduliwa na rafiki yake aliyekuwa na jeshi dogo lakini
wananchi walimwunga mkono kutokana na kupinga udhalimu uliotendewa na watu.
Lissu alisema wapinzani hawapendi kuingia
kwenye vurugu za kuhatarisha amani ya nchi ingawa wanabambikiziwa kesi za
uchochezi kila kukicha.
Alisema jambo la kusikitisha ni kusikia
kesi hizo wanazobambikiziwa kuwa ni maagizo kutoka juu, hivyo wao wanatimiza.
“Ila niwaambie neno moja tu kutokana na
utafiti huu wanajimaliza wenyewe, huku
wapiga vigelegele wao wakiwapoteza,” alisema.
Alisema si watu wote walio kwenye mfumo wanaofurahia
wanayofanyiwa hivyo wanawapa taarifa za mambo wanayotaka kuwafanyia.
Mbunge huyo aliwataka wafuasi wao
kutambua kuwa mambo hayo ni mazito na wasikimbilie hasira, kwani ni hasara.
“Waonevu wengi huwa na chuki na visasi
nyoyoni na vitu wanavyofanya ni kwa malengo yao maalumu,” alisema.
Mwanasheria huyo alisema watawala wanaweza
kuweka kikwazo fulani au kitu fulani vurugu itokee ili wapate sababu au
kisingizio cha kumpata mtu fulani na kulinda maslahi yao.
Lissu alisema watawala wanapanga kukamata
mtu na kumtia kizuizini ili lengo litimie kama ushindi wa uchaguzi, au
vinginevyo, na pia kuvipunguzia nguvu vyama au kuviua,” alisema.
Alisema hata vitendo vya kukwamisha
miradi ya maendeleo katika maeneo ambayo yanaongozwa na wapinzani ni moja ya
mikakati ya watawala kutengeneza migogoro baina yao ila wao wako makini.
“Napenda niwasihi makamanda wote na
wapenzi wa UKAWA tuwe na busara kwani Afrika tuko kwenye hali mbaya sana, na tufahamu
kuwe watawala wanajimaliza, ni suala la muda tu,” aliongeza.
Alisema kila kona na kila idara ni vilio
na kwa mujibu wa utafiti aliofanya ni wazi kuwa wanajimaliza kwa umma.
0 comments:
Post a Comment