Warioba Igombe, Morogoro
JESHI la Polisi mkoani hapa limemkamata
na kumfikisha mahakamani Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkinga (DED) mkoani Tanga,
Emmanuel Barnaba (41) kwa tuhuma ya kumtishia kifo askari wa kikosi cha usalama
barabarani.
Akithibitisha jana kutokea kwa tukio
hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Ulrich Matei alisema tukio hilo lilitokea Jumamosi
maeneo ya Mkambarani baada ya askari Koplo Tutindaga kumwamuru DED kusimama.
Kamanda Matei alisema baada ya mtuhumiwa
kusimamisha gari aina ya Prado, ilibainika
kuwa alikuwa anaendesha gari hilo kwa mwendo kasi ikiwa ni pamoja na kutokuwa
na leseni.
“Baada ya askari wa kikosi cha usalama
barabarani kulisimamisha gari hilo, dereva alikutwa na makosa mengi ikiwa ni
pamoja na kuendesha gari kwa mwendo kasi lakini pia kutokuwa na leseni,” alisema
Kamanda Matei.
Baada ya askari huyo kubaini makosa hayo,
mtuhumiwa alisema hakuwa na fedha za kulipa faini kwa kuwa alikuwa anaendesha
gari la Serikali.
Kwa maelezo hayo, ndipo alipomwamuru DED
huyo kwenda kituo cha Polisi cha Kingolwira, lakini wakiwa njiani mtuhumiwa
alitoa bastola na kumwamuru askari huyo kushuka vinginevyo atamuua.
Inadaiwa kuwa baada ya askari kuona ametishiwa
kuuawa, alishuka na kumwacha mtuhumiwa aendelee na safari yake na yeye kufanya
wawasiliano na askari wa kituo cha Mikese ambao walimtia nguvuni.
Baada ya Polisi kumkamata mtuhumiwa huyo
aliyekuwa anatoka Morogoro kwenda Dar es Salaam walimfikisha kituo kikuu cha
Polisi Morogoro na baadaye mahakamani.
Mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Agripina
Kimaze, Mwendesha Mashitaka, Sandy Hyela alidai kuwa mtuhumiwa anashitakiwa kwa
tuhuma mbili, kutishia kuua kwa silaha la kuvunja sheria za usalama barabarani.
Katika tuhuma ya pili mtuhumiwa anadaiwa
kuendesha bila leseni, kukosa bima, mwendo kasi, kukaidi amri halali ya askari
wa usalama barabarani na kusimamisha gari katikati ya barabara bila kujali
watumiaji wengine.
Baada ya kusomewa mashitaka, mtuhumiwa
alikana na Hakimu Kimaze kusema dhamana
kwa mtuhumia iko wazi na ndipo ndugu na jamaa walipomdhamini baada ya kukidhi
na kesi hiyo itasikilizwa Oktoba 30.
Hata hivyo wakati anatoka mahakamani
hapo ndugu na jamaa zake waliokuwa mahakamani hapo walimficha ili asionekane kwa waandishi wa habari na
kumpiga picha na kisha kumpandisha kwenye gari dogo namba T 830 ARP.
0 comments:
Post a Comment