Bodi yasimamisha malipo ya miradi


Suleiman Msuya

Mwenyekiti wa RFB, Joseph Haule (kulia)
BODI ya Mfuko wa Barabara (RFB) nchini, imeagiza kusimamishwa mara moja kazi zote na malipo yanayogharamiwa na Mfuko huo katika Manispaa ya Kinondoni baada ya kubaini ‘madudu’ kwenye miradi ambayo imetoa fedha.

Aidha, maofisa wote waliohusika wachukuliwe hatua na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Bodi ya Usajili Wahandisi (ERB), Bodi ya Uhasibu (NBAA) na Bodi ya Ununuzi (PSPTB) zichukue hatua dhidi ya wahusika.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa RFB, Joseph Haule wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam akibainisha kuwa mradi wa barabara ya Masjid-Quba ambao ulipaswa kukamilika Juni mwaka jana hadi sasa umekamilika kwa asilimia 28 tu.

Mwenyekiti huyo alisema Bodi hiyo iligundua ‘madudu’ hayo baada ya kufanya ukaguzi wa kiufundi kwa lengo la kubaini ubora wa kazi, mwenendo mzima wa utekelezaji na changamoto zilizopo.

Alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 2.4 ingekamilika ingegharimu zaidi ya Sh bilioni 3.3, lakini hadi mwezi uliopita ni meta 700 tu ndizo zilizokamilika huku kukiwa na upungufu mwingi kwenye kipande hicho.

Haule alisema matokeo ya ukaguzi wa kiufundi katika kipande hicho ni tabaka la lami ambalo limewekwa kutokidhi viwango hivyo kuruhusu hewa na maji kupenya.

“Kitaalamu tabaka la lami linapaswa kuwa  asilimia 16 ila baada ya ukaguzi tulibaini lami iliyowekwa tabaka lake ni asilimia katio ya saba na nane na nguvu ya lami ni ndogo haijafikia kiwango cha chini kabisa kinachokubalika ambacho ni 800kPa,” alisema.

Aidha, alisema ukaguzi ulibaini ITS ilikuwa kati ya 156 hadi 580 kPa, tabaka la mchanga lilikuwa sentimeta tisa kinyume na taratibu ambayo inahitajika kuwa 20 na tabaka la mawe makubwa limewekwa sentimeta 32 badala ya 40 hivyo kupunjwa sentimeta nane.

Kasoro zingine ni taratibu za usanifu, ununuzi, mradi kuchelewa kukamilika, kukosekana kwa mpango kazi, dhamana ya kazi, malipo ya zaidi ya Sh milioni 201 kutohakikiwa, ukiukwaji wa mkataba kwa kulipa chini ya asilimia 25 ambayo inahusika na manispaa kushindwa kutoa nyaraka za ununuzi.

Haule alisema pamoja na mambo mengine, Bodi iliagiza zaidi ya Sh milioni 24 zilizolipwa kwenye cheti namba moja na zaidi Sh milioni 354 zilizotumika kujenga zege badala ya kuziba mashimo, zirejeshwe kwenye akaunti ya mfumo.

Kaimu Mhandisi wa Manispaa hiyo, Azack Kashangala alisema hawezi kuzungumzia mradi huo kwani bado uko katika utekelezaji na kuwa taarifa ya RFB kusitisha fedha bado hajazipata.

Kuhusu miradi mingine ambayo imeonekana kuwa chini ya kiwango, alisema ni vigumu kubainisha tafsiri hiyo kwa kile alichodai kuwa ujenzi wa barabara unategemea mkataba alioingia mkandarasi na Manispaa.

Alisema barabara ya Akachube ujenzi wake haukuwa chini ya kiwango, ila kilichotekea ni magari makubwa kutumia njia hiyo hivyo kuchangia uharibifu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo