Seif Mangwangi, Arusha
John Kahyoza |
MAMIA ya watu kutoka wilaya ya Longido na jijini hapa
jana walifurika kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kusikiliza uamuzi wa
rufani ya kesi ya ubunge wa jimbo la Longido.
Hata hivyo uamuzi huo ulisogezwa mbele baada ya kudaiwa kuwa
wakata rufaa walishindwa kuwajumuisha kwenye kesi hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG) na aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi jimboni humo.
Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Sauda Mjasiri, Mussa
Kipenka na Profesa Ibrahim Juma, waliokuwa wanasikiliza rufani hiyo, walitoa
uamuzi huo jana, ukisomwa na Msajili wa Mahakama ya Rufani nchini, John Kahyoza
Katika uamuzi huo, waliamua upande wa rufaa uliopinga
kutenguliwa matokeo ya ubunge wa Longido, uwaongeze AG na Msimamizi wa Uchaguzi
kwa walichodai ni muhimu katika kesi hiyo kazi inayotakiwa kufanyika ndani ya
siku 21 ili kuruhusu kuendelea kwa rufani ya msingi.
Msajili Kahyoza akisoma uamuzi wa majaji hao, alisema katika
rufani hiyo, Wakili wa wajibu rufaa, Masumbuko Lamwai na Edmund Ndemela
waliokuwa wanamtetea aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Steven Kiruswa waliwasilisha
hoja, kutaka rufani hiyo, itupwe kwa kuwa waliokata rufani hawajawajumuisha, AG
na Msimamizi wa Uchaguzi.
Hata hivyo, mawakili wa aliyekuwa Mbunge wa Longido,
Onesmo ole Nangole, Wakili Method Kimomogoro na John Materu, walipinga hoja
hiyo kwa maelezo wao tayari waliwapatia AG na Msimamizi Notisi ya kukata rufani
na hoja za rufani.
Kimomogoro alisema baada ya kukawabidhi, walitarajia kujumuika
kwenye rufaa ya kupinga mteja wao kuvuliwa ubunge, lakini awali walikuwapo na
baadaye wakajitoa.
Majaji walisema wameshindwa kuitupilia mbali rufani hiyo,
kwa kuwa ina hoja za msingi, lakini wakakubaliana na nusu ya baadhi za hoja za
Wakili Lamwai kuwa AG na Msimamizi ni watu muhimu katika kesi hiyo.
Walisema kwa kuwa sababu zote tatu za kutenguliwa
matokeo, zilitokana na Msimamizi wa Uchaguzi kushindwa kutimiza wajibu wake,
katika rufani alipaswa kushirikishwa.
"Kutoshirikishwa kwa AG na Msimamizi ni kuwanyima
haki yao ya msingi kusikilizwa na ndio sababu Mahakama ya Rufani imetumia
kifungu cha 111 cha kanuni za Mahakama hiyo, kuagiza waunganishwe katika shauri
hilo," alisema Kahyoza.
Majaji waliagiza nyaraka zipelekwa upya katika Mahakama
hiyo ndani ya siku 21 zikiwajumuisha maofisa hao na kuhusu gharama za rufani
hiyo, zitalipwa baada ya kutolewa uamuzi wa mwisho.
Katika uchaguzi uliopita, Nangole alitangazwa mshindi
baada ya kupata kura 20,076 dhidi ya 19,352 za Kiruswa.
0 comments:
Post a Comment