Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Kamati ya Uongozi wa Chama cha Wananchi
(CUF), Julius Mtatiro, ameomba viongozi walio madarakani kutambua thamani ya
kuchaguliwa kwao na kuilipa thamani kwa kuwaletea maendeleo wapiga kura wao.
Mtatiro alisema hayo mbele ya wajumbe waliohudhuria
mkutano ulioshirikisha viongozi wa vyama vyenye mlengo wa kimapinduzi Afrika uliofanyika
Afrika Kusini hivi karibuni.
Katika hotuba yake iliyopatikana Dar es Salaam, huku
akitoa mifano, Mtatiro alisema viongozi wengi wa Afrika wanatumia nguvu kubwa
kutafuta madaraka na wakishayapata husahau wananchi kwa kutowapelekea
maendeleo.
“Wakati tunapambana kutengeneza demokrasia ya kweli
Afrika, ndugu zetu wa vyama tawala wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kutafuta
madaraka na kukandamiza vyama vya upinzani na wanapoyapata hawawakumbuki tena hata
wapiga kura,” alisema.
Mtatiro alisema wakati Waafrika wanapambana kukuza demokrasia
na kutafuta maendeleo kwa wananchi, hali imekuwa tofauti kwa vyama tawala
ambavyo vimekuwa vikijali sana madaraka bila kukumbuka wapiga kura.
Katika hotuba hiyo, Mtatiro alimnukuu Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Nyerere ambaye katika hotuba yake mwaka 1960 aliwaambia viongozi kuwa
wanapopewa dhamana na kuaminiwa na watu wanatakiwa kulipa uaminifu huo kwa
kuwaletea maendeleo.
Aliwataka wajumbe wa vyama vya upinzani waliohudhuria
mkutano huo kuunganisha nguvu na kushirikiana kuhakikisha demokrasia ya kweli
inapatikana Afrika pamoja na kuwaelekezea maendeleo wananchi ambao ndio wapiga
kura.
“Kwa pomaja tukishirikiana na kushikana mikono, tunaweza
tukapambana na madhila ambayo sisi vyama vya upinzani tumekuwa tukifanyiwa na
vyama tawala na pengine kwa miaka ijayo tutaweza kuonja matunda ya demokrasia
ya Afrika,” alisema.
Mkutano huo wa siku mbili uliofanyika Johannesburg,
ulihudhuriwa na viongozi wa vyama vya upinzani wa ukanda wa nchi za Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
0 comments:
Post a Comment