* Ikilazimika atahakiki mwenyewe waliokopeshwa
Salha Mohamed
Rais Magufuli UDSM |
RAIS John Magufuli ameionya Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Heslb), kuwa akibidi ataitisha orodha ya wanafunzi wote
waliopatiwa mikopo na kuhakiki mmoja baada ya mwingine yeye mwenyewe.
Akizungumza wakati katika Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM), wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa mabweni 20
yenye ghorofa nne ya chuo hicho, aliitaka Bodi hiyo, kuhakiki orodha ya
wanafunzi wanaostahili kupewa mikopo ili kuepusha uwezekano wa wanafunzi
wasiostahili hasa wa matajiri na mawaziri kupata mikopo hiyo.
“Sitaki siku nifike Bodi ya Mikopo
nichukue orodha ya wanafunzi wote niangalie shule walizosoma na taarifa
walizojaza, halafu nije nipewe majina ya watu ambao hawakustahili kupata
mikopo.
“Wanafunzi 25,000 wa mwaka huu siwezi
kushindwa kupitia kwa siku moja kwa kuangalia kurasa hadi kurasa kwani nitagawa
(majina hayo) kwa saa 12 ambazo nitajifungia…tusifikie huko,” alionya na
kuwataka wanafunzi kuwa wavumilivu katika kipindi wanachopitia sasa.
Alisema Serikali ilifuatilia Bodi hiyo
na kubaini uwepo wa wanafunzi hewa pamoja na wanafunzi waliomaliza elimu zao lakini
wakaomba mikopo upya, ili wapate fedha bila kuhudhuria darasani.
Alisisitiza kuwa Serikali haitatoa mkopo
kwa wanafunzi wenye wazazi matajiri na badala yake wanaostahili ni watoto wa
masikini, huku akiagiza Bodi hiyo kutumia sheria kudai walionufaika wa mikopo
hiyo, kwani hadi sasa deni limefikia Sh trilioni 2.6.
“Lengo la Serikali ni kutoa elimu bora
lakini haitatoa mikopo kwa wanafunzi wenye uwezo, mtoto wa Ndalichako (Profesa
Joyce, Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi) naye apate mkopo!
“Mtoto wa Katibu Mkuu Kiongozi Kijazi
(Balozi John naye apate mkopo! Haiwezekani! Mkopo huu umelenga kwa ajili ya
watoto masikini,”alisema Magufuli.
Alisema anafahamu na kusikia kuwa bodi
ya mikopo kuna upendeleo wa kutoa mikopo kwani wapo wanaostahili kupata mikopo,
lakini hawapati huku wasiostahili wakipata.
Alimtaka Profesa Ndalichako pamoja na Bodi
hiyo kusimamia changamoto hizo na kuhakikisha Sh trilioni 2.6 zilizokopeshwa
kwa wanafunzi zinarudishwa.
Katika hatua nyingine, Dk Magufuli
amesema kumekuwepo na utitiri wa vyuo vikuu vinavyogombania wanafunzi, wakati
baadhi ya vyuo hivyo vikiwa na wanafunzi
20 bila mabweni wala mahabara.
“Natoa mwito kwa TCU, hebu mpitie
vizuri…mnatoa vibali mno vya kuanzisha vyuo vikuu kila mahali wakati vyuo
vilivyopo havijaja watu na vyuo vikuu vingine havina walimu,”alisema na
kuongeza kuwa si lazima kila mahali kuwe
na chuo kwani vingine vipo uchochoroni.
“Mimi nasema kwa uwazi siogopi, lazima
tukae na tuchambue mwelekeo wa elimu…sisi serikali tumejipanga kutoa mikopo kwa
watoto wa masikini.
“Wanahaki ya kuomba mikopo katika vyuo
hivyo kwa sababu sisi ndiyo tumewapeleka huko, tumevuruga elimu tujirekebishe
ili kuipa nafasi Serikali kwenda katika mwelekeo mzuri,”alisema.
Alisema haoni sababu ya kuwepo kwa mafunzo
ya shahada ya udaktari katika Chuo Kikuu Dar es Salaam baada ya kuzinduliwa kwa
Chuo cha Tiba cha Mloganzila hivyo wanafunzi
hao wapelekwe huko.
Aliongeza kuwa anafahamu mazingira
wanayopitia wanafunzi hao kwa sasa kwani alisoma hapo, hivyo watimize wajibu
wao.
“Waziri (Profesa Ndalichako) yale ambayo
ni dosari, yamejitokeza yasijirudi tena, wanaostahili kupata mikopo wapate
haraka na naninajua awamu ya kwanza zinahitajika zaidi ya Sh bilioni 157,” alisema.
Alisema awamu ya kwanza imetolewa Sh
bilioni 80 na kuwataka wanafunzi hao kutumia fedha hizo kwa ajili ya kusoma.
Dk Magufuli alisema ni vema viongozi wa
vyuo na wanafunzi waivumilie Serikali katika kupitia mabadiliko, ili kuweka
utaratibu uliokuwa mzuri kwani anafahamu katika Bajeti ya Serikali ya 2016/2017
kulitenga Sh bilioni 340 zitakazotosheleza wanafunzi 90,000.
“Baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia
madarakani ili kutimiza yale iliyoahidi tuliongeza fedha za mkopo hadi kufikia
Sh bilioni 473 kutokana na makusanyo na kutoa mikopo kwa wanafunzi 124,358,”alisema.
Alisema mwaka huu zaidi ya Sh bilioni
480 zimetengwa ambapo wanafunzi wengi zaidi watapata mkopo huku akibainisha
anafahamu wanafunzi waliokuwa wakiendelea pamoja na wanaojiunga sasa ni zaidi
ya 25,000.
Magufuli alikiri kutokuwepo kwa
uangalizi kwani vyuo vya elimu ya juu vinapaswa kuwa na tarehe moja ya kufungua,
ili kuipa Bodi hiyo muda wa kutoa orodha ya wanafunzi wanaostahili kupewa
mikopo.
“Palitakiwa kuwepo na Wizara ya Elimu,
Wizara ya Fedha na Bodi ya Mikopo kwamba kuna wanafunzi watakaopata mkopo hawa,
majina na kiasi cha fedha.
“Hapakuwa na sababu ya kufungua mwezi
mzima kabla, wakati hawajui kama wanafunzi watapata mkopo au hawapati au asifanye
udahili kwa sababu hajapata mkopo. Hii inaleta usumbufu kwa vijana,” alisema.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribishwa
Rais Magufuli, Profesa Ndalichako aliwataka wanafunzi kusoma na kucha
kujiingiza kwenye siasa au kushabikia mambo yasiyokuwa na takwimu.
“Sasa hivi kumetokea upepo wa kusema vijana
hawasomeshwi, mambo haya yametokea wapi? Kwa taarifa yenu hadi sasa hivi katika
Sh bilioni 483 za Bajeti ya Serikali imeshatenga Sh bilioni 120,” alisema
Profesa Ndalichako.
Alisema mchakato wa kutoa mikopo kwa
wanafunzi unaendelea ambap hadi hadi sasa serikali imefanya malipo kwa
wanafunzi 11,332 wa mwaka wa kwanza na Sh bilioni 40 zimeshatolewa kwa ajili ya
ada vyuoni.
Alisema wanafunzi waliodahiliwa ni
58,000 huku akibainisha kuwa serikali haiwezi kutoa mkopo kwa mwanafunzi ambaye
anauwezo.
“Wale waliokuwa kwenye utaratibu
watapata fedha yao kama kawaida,tutafanya kazi kwa bidii bila kujali madongo
ambayo tunapigwa ” alisema.
0 comments:
Post a Comment