Grace Gurisha
HATIMAYE raia watatu wa China wamepandishwa kizimbani kwenye
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakidaiwa kumteka na kumjeruhi
mwenzao, Liu Hong na kumweka katika hatari ya kifo.
Watuhumiwa hao Chen Bao (34), dereva Wang Jian (37) na
Zheng Pa Jin ‘Mr Ping’ (40) ambaye ni mfanyabiashara. Bao na Jian walikiri mashitaka
huku Mr Ping akikana yote.
Akisoma hati ya mashitaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi
Hellen Moshi alidai jana mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Cyprian Mkeha kuwa washitakiwa wanadaiwa kuteka na kujeruhi.
Moshi alidai kuwa Oktoba 21 raia hao wakiwa eneo la Palm Beach,
Ilala walimteka Hong ambaye ni mwanamke kwa lengo la kumweka kumsababishia
kifo.
Katika mashitaka ya pili, Moshi alidai kuwa siku hiyo hiyo
na eneo hilo hilo, raia hao walimpiga Hong na kumsababishia majeraha mwilini.
Jian alikiri kumteka mwanamke huyo na kumjeruhi, huku Bao
akimweleza hakimu kuwa alimchukua na kumweka hotelini, ila hakumteka kama
inavyodaiwa na upande wa Jamhuri.
Mr Ping ambaye muda wote alionekana mkali, alikana
kuhusika huku akitaka kujua hatima yake kwenye kesi hiyo kutokana na kwamba
upelelezi haujakamilika.
Dhamana
Hata hivyo, kabla Mahakama haijapanga tarehe ya kutajwa kesi
hiyo, Moshi alidai kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Ilala (RCO) aliwasilisha kipo
kupinga dhamana ya raia hao kutokana na sababu maalumu saba.
Alidai kuwa kiapo hicho kiliapwa na Mrakibu Mwandamizi wa
Polisi, Salumu Ndalama, akieleza kuwa anajihusisha na upelelezi wa makosa ya
jinai.
Na kwamba washitakiwa ni raia wa China na hawana taarifa
za makazi yao nchini, hivyo hawastahili dhamana.
Moshi alidai kuwa Ndalama ana taarifa za kuaminika ambazo
walizikusanya kupitia upelelezi wa kesi hiyo, kwamba washitakiwa hao na
watuhumiwa wengine ambao hawajakamatwa, wanapanga kujihusisha na vitendo vya uhalifu
Dar es Salaam ukiwamo utekaji.
Pia kiapo hicho kiliendelea kueleza kuwa zipo taarifa za
kuaminika, kwamba washitakiwa na watuhumiwa ambao hawajakamatwa, wana mpango wa
kumdhuru Hong kwa lengo la kupoteza ushahidi.
"Upelelezi bado unaendelea, wakipewa dhamana
wanaweza kuingilia upelelezi na pia tuna taarifa za kuaminika kuwa Wachina
wengine ambao ndugu yao alitekwa nyara, wanapanga kulipiza kisasi.
“Kwa hiyo ni kwa maslahi ya Jamhuri washitakiwa wabaki
ndani hadi kesi itakapokwisha ili kulinda usalama wa Hong na raia hao,"
kilieleza kiapo hicho.
Washitakiwa hao ambao walikuwa wanatafsiriwa na mkalimani
kwa kutokujua Kiingereza na Kiswahili, walielezwa na kujikuta wakipatwa kiwewe cha
kutaka kujua hatima yao.
Hakimu Mkeha aliwauliza kama watawasilisha kiapo kinzani
kujibu kiapo cha RCO, wakadai kuwa na mawakili wao kwa hiyo watalishugulikia
hilo, lakini baadaye walionekana kukosa mwelekeo baada ya kukosekana mtu mwenye
aarifa zao.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 14 siku ambayo upande
wa washitakiwa utajibu hoja za RCO kupinga dhamana yao.
0 comments:
Post a Comment