*Waendana na matukio ya kupora silaha, kuua
*Polisi
yasema iko imara inaendelea kupambana
Mwandishi Wetu
Rais John Magufuli |
LICHA ya kazi nzuri inayofanywa na Jeshi
la Polisi kukabili uhalifu nchini, taarifa za uhakika kutoka Jeshi hilo zinaonesha
kwamba matukio ya uhalifu unaombatana na uporaji wa silaha hufanyika kwa
kupangwa na watu wenye malengo ya kufanikisha mambo yao.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Jeshi
hilo, watu hao hupanga na kutekeleza matukio hayo wakilenga kuitikisa nchi hata
Serikali ili kufanikisha mambo wanayoyataka kwa maslahi yao.
Habari zilizoifikia JAMBO LEO zinaeleza
kwamba majambazi wanaopora silaha hizo, hupanga kuzitumia kwenye matukio
yanayolenga kuvuruga amani na utulivu nchini, ili kujijengea uhalali wa kutekeleza
mipango yao inayokwenda kinyume na ile ya Serikali na Taifa kwa jumla.
Taarifa zinaonesha kuwa tangu Januari
mwaka juzi hadi jana matukio zaidi ya 10 ya ujambazi yaliyoambatana na uporaji
wa silaha na mali na watu kujeruhiwa pamoja na vifo kutokea yaliripotiwa.
Hata hivyo, baada ya matukio hayo, polisi
kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa taarifa ya kukamata silaha hizo.
“Haya si matukio ya kawaida, ingawa watu
wakiona yanatokea wanadhani kuwa ni ujambazi. Kuna watu wana mambo yao ili nchi
ionekane haijatulia,” alieleza mmoja wa maofisa wa Jeshi hilo mwenye cheo cha
Inspekta.
“Tuna kazi kubwa, lakini tunapambana kwa
nguvu zote kuhakikisha matukio hayo yanakoma. Haya matukio ni zaidi ya watu
wanavyoyafikiria.”
Kuhusu matukio ambayo askari walipoteza
maisha, mtoa taarifa huyo alisema ni jambo linalohuzunisha kwa kiasi kikubwa,
lakini inatokea katika mapambano yenye lengo la kukabili uhalifu huo.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu hakukiri wala kukanusha, lakini akasema
huenda taarifa hizo ni maoni ya watu ambayo mwandishi wa habari hizi ameyasikia.
“Matukio ya ujambazi yanayotokea ndiyo
hayo ambayo mnayasikia polisi wakiyatolea ufafanuzi…ujambazi tunashughulika nao
miaka nenda rudi na wala si ajabu Polisi kukabiliana na wahalifu na majambazi,”
alisema Mangu.
Aliongeza: “Tunapokamata majambazi
tunatoa taarifa na kwa sababu hilo unalonieleza huenda ikawa mtazamo ya mtu,
siwezi kuchangia mengi kuhusu jambo hilo.”
Katika maelezo yake, mpashaji habari wa
JAMBO LEO alisema watu hao wanalenga kuandaa kikundi kitakachokuwa kikishiriki
matukio ovu na kwamba polisi wanalijua hilo na kwamba kundi hilo haliwezi
kufika kokote.
“Kaka we acha tu watu wakiona haya mambo
(ujambazi) kila mmoja anasema lake, lakini ukweli ni kwamba kuna kitu nyuma ya
haya mambo,” alisema.
Mwananchi ambaye hakutaka kutajwa jina,
alisema anaamini kasi aliyonayo Rais John Magufuli ya kuwaletea wananchi
maendeleo haifurahishi baadhi ya watu waliodhani angeshindwa.
“Haya mambo yanawezekana kweli yakawa
yanahusishwa na siasa, kwa sababu kuna watu aliokuwa akipambana nao kwenye
uchaguzi walidhani atashindwa kukabiliana na uovu, lakini kasi hii inawatisha
wanajaribu kumvuta shati,” alisema.
Matukio
Septemba 5 katika tukio la Vikindu
mkoani Pwani ambako polisi walijibizana risasi na majambazi na askari mmoja
kuuawa, walikamata majambazi watatu waliohusika na tukio hilo ambao
waliwapeleka polisi eneo la Mbezi Chini kwenye
nyumba waliyokuwa wamekodi na askari kufanya upekuzi na walifanikiwa kupata
silaha, zikiwamo bunduki 23 na risasi zaidi ya 800 na vitu vingine.
Pia walikuta redio
za mawasiliano 12 na chaja zake tatu, darubini za kuonea mbali tatu, pingu za
plastiki 45, majaketi ya kuzuia risasi matatu, mkasi wa kukatia vyuma, mtaimbo,
risasi baridi za kutishia 37, kasha la kusafirishia silaha, nyundo kubwa moja,
pingu za chuma tatu, mashine ya kuhifadhia kumbukumbu na magari mawili.
Julai 12, watu walioaminika kuwa
majambazi walivamia kituo cha Polisi cha Stakishari, Ukonga, Dar es Salaam kuua
askari wanne na watatu wengine na kisha kupora silaha zinazosadikiwa kuwa ni
zaidi ya 20.
Septemba mbili, majambazi walivamia na
kuua mlinzi wa Chuo cha Sebastian Kolowa (Secomu) na kumpora silaha aliyokuwa
nayo.
Tukio hili lilishuhudiwa pia mmoja wa
majambazi hao akipigwa risasi na wenzake akihofiwa kuvujisha siri zao, baada ya
pikipiki aliyokuwa akitumia, kugoma kuwaka baada ya kukamilisha uhalifu huo.
Januari 21 mwaka jana, majambazi yaliojihami
kwa silaha walivamia Kituo cha Polisi cha Ikwiriri, Rufiji mkoani Pwani na kuua
askari wawili na kupora silaha zilizokuwa kituoni hapo.
Silaha zilizoporwa ni SMG mbili, SAR
mbili, shotgun moja, mabomu ya kutoa machozi na risasi 60 za SMG.
Siku sita baadaye, Januari 27, mkoani Tanga
watu wanaodhaniwa kuwa majambazi, walivamia na kujeruhi askari wakiwa doria ya
pikipiki na kuwanyang’anya silaha mbili aina ya SMG.
Februari 3 mwaka jana, kundi la watu wanaodhaniwa
kuwa majambazi, walivamia na kuvunja stoo ya Kituo Kidogo cha Polisi Mngeta,
Kilombero, Morogoro na kuiba SMG ikiwa na risasi 30, pia waliiba jenereta,
redio, viti, betri ya gari na spika ya redio.
Machi 30 mwaka jana, askari wawili
waliuawa na mmoja kujeruhiwa na majambazi Kongowe, Dar es Salaam na kuporwa SMG
mbili.
Mei 29 mwaka jana, Dar es Salaam, watu
wanaosadikiwa kuwa majambazi, walivamia lindo askari wa Kikosi cha Tazara, Dar
es Salaam na kupora SMG.
Juni 12 mwaka juzi, majambazi
wanaokadiriwa kuwa sita, wakiwa na pikipiki tatu, walivamia Kituo Kidogo cha
Polisi Mkamba Kimanzishana, Mkuranga, Pwani na kuua askari mmoja na mgambo
wawili na kupora bunduki tano na risasi 60.
0 comments:
Post a Comment