Suleiman Msuya
KENYA imetangaza kwamba Tanzania
imejitoa katika mpango wa Viza ya pamoja wa Afrika Mashariki ikitaja moja ya
sababu zake kuwa ni kuhofia ushindani na nchi hiyo.
Katika taarifa yeke iliyonukuliwa na
vyombo vya habari nchini humo wiki iliyopita, Kenya kupitia Katibu wake wa
Baraza la Utalii, Najib Balala ilitangaza hatua hiyo ya Tanzania ikisema itapunguza idadi ya watalii
kwa nchi za EAC.
Hata hivyo, Serikali imekanusha taarifa hizo
ikieleza kwamba mchakato wa Viza ya pamoja unaratibiwa na Sekretarieti ya EAC
na kwamba imesikitishwa na shutuma hizo kuelekezwa kwa Tanzania moja kwa moja.
Kaimu Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji
na Sekta za Uzalishaji Wizara ya Mambo ya Nje na Afrika Mashariki, Bernard
Haule aliliambia JAMBO LEO mwishoni mwa wiki kwamba taarifa hizo ni za
upotoshaji.
“Ni jambo la kusikitisha kuona kiongozi
anatoka mbele ya vyombo vya habari anapotosha na kudanganya umma wa EAC kuwa
Tanzania imegoma kujiunga katika mpango huo,” alisema Haule.
Alibainisha kuwa hakuna maridhiano
yoyote yaliyokwishafanyika kuhusu mpango huo na kwamba hatua zilizofanyika ni
sekretarieti kufanya utafiti wa jinsi nchi hizo zitakavyoweza kunufaika na mpango
huo wa Viza moja utakapooanza.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema baada ya
hoja hiyo kutolewa Baraza la Mawaziri la EAC liliitaka sekretarieti ya jumuia hiyo
kuangalia maeneo yanayoweza kuwa na tija iwapo mpango huo utaanza kutekelezwa.
Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni
miundombinu sahihi ya kutoa Viza ya pamoja na kila nchi mwanachama kuweza
kunufaika, uwepo wa rasilimali watu wa kutosha na usalama wa Viza na nchi.
“Na sisi tumeiona taarifa hiyo kwenye
mitandao na vyombo vya habari vya huko Kenya eti tumejitoa katika mpango wa
Viza moja ya EAC. Ni jambo la kusikitisha kuhusishwa na suala hilo ambalo bado
lipo kwenye mchakato,” alisema.
Alisema ili mpango huo uanze kufanya
kazi ni jukumu la nchi wanachama kupitia EAC kukubaliana na si suala la nchi
nan chi kama ambavyo inavyosemwa na Balala.
Haule aliendelea kusema zipo njama za
kuichafua Tanzania katika mpango huu kwa kile alichodai kuwa nchi ya Burundi ni
mwanachama ila haikutajwa kuwa imejitoa au ipo hivyo kumtaka Katibu huyo wa
Baraza la Utalii Kenya kuwa muwazi ili aeleweke.
Alisema nchi ambazo zinatajwa kuingia
katika hiyo Viza ya pamoja hadi sasa ni zile za Ukanda wa Kaskazini ambazo ni
Kenya, Uganda na Rwanda na kwamba ili utekelezaji wake uanze ni lazima nchi
zote wanachama zishiriki.
“Unajua mambo mengi ni aibu mbona Kenya
imekataa kusaini mkataba wa soko la mitaji lanikini hakuna mtu ambaye
anaishambulia nadhani watafute mbinu nyingine za kutoa malalamiko yo,” alisema.
Kuhusu Tanzania kutoshiriki mkutano wa
masoko utakaofanyika jijini London, sababu ikiwa ni kutojiunga katika mpango
huo wa Viza ya pamoja alisema si kweli na kwamba mkutano huo hauhusiani na
suala hilo.
Awali, Balala alisema kama nchi tatu
zilizojiunga zinataka kupiga hatua katika utalii ni vema kuboresha umoja huo na
kuwa Tanzania itahyamasika kujiunga.
Alisema tatizo la nchi za Afrika
Mashariki ni kuishi kwa hofu katika mambo wasiyoyajua, hali inayosababisha kila
nchi kuangalia mwenzake badala ya kushindana.
0 comments:
Post a Comment