Serikali yakana kutisha wafanyabiashara


Richard Mwangulube, Arusha

MKUU wa Mkoa, Mrisho Gambo amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali hazina maana ya kutisha wala kuonea wawekezaji na wafanyabiashara bali kuimarisha ukusanyaji mapato.

Gambo alisema hayo jana alipokutana na wafanyabiashara  na wawekezaji  wa mkoa akielezea umuhimu  wa kulipa kodi ya Serikali.

Aidha, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani hapa kutenda haki na kufuata sheria inapokusanya kodi na   isitumie vitisho kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Mkuu wa Mkoa alisisitiza, kwamba Serikali lazima ilinde wawekezaji na wafanyabishara, ili kupata kodi isaidie kukuza uchumi wa nchi na kuboresha huduma za jamii.

Gambo alisisitiza, kwamba  wafanyabiashara na wawekezaji ni kiungo muhimu kwa Serikali huku akionya dhidi ya tabia ya baadhi ya watendaji serikalini kuwa kikwazo kwa wafanyabiashara na wawekezaji katika kufanikisha ulipaji kodi.

Alisema baadhi ya watendaji wa taasisi za Serikali  wamejigeuza miungu watu na vikwazo huku wakiendesha shughuli kibabaishaji, hali ambayo inachangia Serikali kupoteza mapato.

Gambo alisema Serikali ikiwa mbali na wawekezaji na wafanyabiashara itakosa mapato, hivyo ni lazima ijenge mazingira ya kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara bila   vikwazo.

Wafanyabiashara  nao  waliitaka Serikali kuhahakisha inaondoa urasimu  ambao ni changamoto kwao.
  
Aidha, walieleza kukerwa na tabia ya baadhi ya watendaji serikalini kukithiri kwa rushwa wakati wakitimiza majukumu yao.

Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Watalii, Wilbrod Chambulo alisema utitiri wa kodi ambazo kwa sasa  ni  takribani 54 ni kero kwa wafanyabiashara  na wawekezaji.

Chambulo alisema hivi sasa wafanyabiashara  na wawekezaji wanafanya kazi kwa woga na hofu kutokana na changamoto   zilizopo.

Aliitaka Serikali itengeneze njia nzuri ya kukusanya kodi   na kuziweka kwenye mfumo mmoja badala ya kuendelea kuwa na utitiri wa kodi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo