Sharifa Marira, Dodoma
Felchesmi Mramba |
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco),
limeichongea Serikali mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
likieleza kuidai Sh bilioni 125 kutokana na taasisi zake kubwa kutumia umeme
bila kulipa.
Akizungumza mbele ya Kamati hiyo jana
mjini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba, alilitaja Shirika
la Umeme Zanzibar (ZECO) kuwa ndilo mdaiwa sugu wa Sh bilioni 85 huku
taasisi zingine zikidaiwa Sh bilioni 40.
Mramba alisema hayo wakati akijibu hoja
za wajumbe wa PAC kuhusu ripoti ya ukaguzi ya CAG iliyoishia Juni mwaka jana ya
hesabu za shirika hilo.
Alisema shirika hilo limeanza kufanya
mikutano kadhaa na ZECO kwa ajili ya mikakati itakayofanikisha kulipwa deni hilo
la tangu mwaka 2013.
Katika mikutano hiyo walibaini kuwa ZECO
inashindwa kulipa kwa sababu inatoza gharama ndogo kwa wateja wa umeme Zanzibar
tofauti na gharama za ununuaji umeme kutoka Tanesco.
Mramba alisema kwa taarifa za hivi
karibuni ambazo shirika hilo lilizipata kutoka ZECO ni kwamba limewasilisha
deni hilo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kusaidiwa kulipa.
Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru
alisema tayari amewasilisha ripoti ya madeni hayo ngazi za juu za uamuzi kwa
ajili ya kufanyiwa kazi,Tanesco imefanya jitihada kubwa sana katika kuhakikisha
inalipwa madeni haya.
Alisema katika kipindi cha wiki mbili
zilizopita, waliwasilisha suala hilo ngazi za juu za uamuzi na kueleza
changamoto zinazolikabili shirika hilo za kutokulipwa madeni yake hasa na
taasisi kubwa za Serikali.
Mafuru alieleza kuwa maelekezo ya ngazi
hizo za juu ni kwamba kuanzia sasa taasisi yoyote isiyotenga bajeti yake kwa
ajili ya umeme, isipolipa ichukuliwe hatua.
Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka
aliiagiza Serikali kuhakikisha inalipa madeni hayo ya Tanesco ndani ya
miezi sita.
Mbunge wa Morogoro Mashariki, Omary
Mgumba (CCM) alilitaka shirika hilo, pamoja na kufuatilia madeni hayo, liweke
mikakati ya kuhakikisha linaondokana na tatizo la mlundikano wa madeni, hali
inayosababisha liendelee kujiendesha kwa hasara.
Mramba alisema kwa sasa limeanza kuondoa
mita zote za kawaida na kuweka za mfumo wa Lipa Kadri Unavyotumia (LUKU).
0 comments:
Post a Comment