Mwandishi Wetu
WAATHIRIKA wa Ukimwi wanakabiliwa na hatari ya kuugua
magonjwa yasiyoambukiza ya saratani na kupata matatizo ya misuli ya moyo,
kutokana na athari za matumizi ya Dawa za Kupunguza Makali ya Virusi vya Ukimwi
(ARV).
Utafiti mpya uliochapishwa juzi na Taasisi Utafiti wa
Saratani na Virusi Vinavyosababisha Ukimwi (VVU) ya Chuo Kikuu cha Califonia,
San Francisco (UCSF), umeeleza kuwa saratani hutokea katika tishu za mwili,
ambako virusi hivyo hukimbilia kujificha ili visifikiwe na ARV.
Taarifa ya Mtaalamu wa Maabara, Profesa Michael McGrath
wa UCSF iliyochapishwa katika jarida la
Virology la mwezi huu, imeeleza imependekeza
utafiti wa haraka ufanyike ili kutafuta muafaka wa tatizo hilo.
Wanasayansi hao wameelezwa kuwa walifanya utafiti huo
baada ya kubaini kuwa baadhi ya waathirika wa VVU wanaotumia ARV na kuwa na
afya nzuri, hujikuta wakifa ghafla.
“Baada ya kuchunguza tukabaini kuwa vifo hivi
vinasababishwa na saratani pamoja na matatizo ya misuli ya moyo,” alisema
Profesa McGrath.
Hali hiyo, anasema iliwafanya waendelee na utafiti ambao
matokeo yake wameyapata mwezi huu kwa kubaini kuwa virusi vinavyojiviche kwenye
tishu za mwili ambako havifikiwi na ARV ndivyo vinasababisha tatizo hilo.
Tangu dawa za ARV zianze kutumika zimeonekana kuzuia VVU
kuathiri seli nyeupe za binadamu maarufu kama CD4.
Matumizi hayo yameweza kuwafanya baadhi ya waathirika
kupima na kutoonekana tena kuwa na VVU kwenye mfumo wao wa damu lakini wakiacha
kutumia ARV huzuka ghafla na kuanza kuonekana vikishambulia CD4.
Profesa McGrath anasema kuwa katika utafiti wao wamebaini
kuwa kwenye tishu za mwili wa binadamu ambako VVU hujificha vinasababisha
tatizo la saratani na matatizo ya moyo.
“Hivi vifo vya wagonjwa walio katika matumizi ya ARV
vinaelekea vinatokana na uwapo wa virusi hawa waliojificha kwenye tishu baada
ya kushindikana kufikiwa na dawa ya kuwaangamiza,” alisema Profesa McGrath na
akifafanua:
“Utafiti wetu unashauri juhudi zifanyike ili ipatikane
dawa ambayo licha ya kuwaangamiza virusi kwenye damu, pia iweze kufika maeneo
ambayo virusi hawa hijificha.”
Kwa mujibu wa watafiti wa VVU na Ukimwi, iwapo
itapatikana dawa ambayo inawafikia virusi kwenye tishu wanakojificha itakuwa
imepatikana dawa kamili.
Kulingana na maelekezo ya matumizi ya ARV kwa sasa,
mwathirika wa VVU anapaswa kutumia dawa hizo maisha yake yote.
Hii ni kwa sababu anapoacha virusi hutoka walikojificha
na kuanza kusambaa mwilini kwa kuzaliana kwa kutumia CD4 na hii inakuwa rahisi
mwathirika kushambuliwa na magonjwa nyemelezi na kuanza kuugua Ukimwi.
Kwa sasa waathirika wanahimizwa kutumia ARV kikamilifu na
huu ni mpango endelevu kwa maisha yao yote.
Kutumia kikamilifu kunaweza kufanya hata akipimwa
asionekane na VVU kwenye damu na wakati huu huweza kuendelea na maisha ya kawaida ikiwa ni pamoja na kuoa
na kuzaa watoto wasio na maambukizi ya VVU.
Matumizi ya ARV yamewezesha kuwepo na matumaini kwamba
VVU ambavyo viligundulika mwanzoni mwa miaka ya 1980, huenda vikavikia ukomo
mwaka 2030, iwapo zitatumika vizuri.
Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonyesha kwamba
matumizi ya ARV yamepunguza kasi ya maambukizi ya VVU duniani.
Kwa sababu hiyo, mpango wa WHO ni kwamba dunia iwe na
maambukizi sifuri ifikapo mwaka 2030, miaka 14 ijayo.
0 comments:
Post a Comment