* Bei za vyakula nazo zapaa nchini
Waandishi Wetu, Dar na mikoani
OFISI ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Uratibu
wa Maafa, imesema kuna dalili za nchi kukabiliwa na ukame utakaoandamana na
kaya nyingi kukumbwa na njaa na magonjwa
ya mlipuko.
Kutokana na hali hiyo, imewataka
wananchi kuchukua hadhari kwa kuotesha mazao ya muda mfupi na kutumia kwa
uangalifu chakula walichonacho.
Akizungumza jana Dar es Salaam,
Mkurugenzi wa Idara hiyo, Brigedia Jenerali Mbaazi Msuya alisema hali hiyo inatokana
na upungufu wa mvua na ukame unaoweza kuiathiri nchi.
Alisema hali hiyo inatokana na taarifa
za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuonesha kwamba kutakuwa na ukame katika
kipindi cha mwezi huu hadi Desemba.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa TMA,
Dk Paschal Waniha kutakuwa na vipindi virefu vikavu ndani ya msimu wa mvua
zinazoweza kusababisha unyevunyevu mdogo kwenye udongo na hivyo kuathiri ustawi
wa mazao ya kilimo katika maeneo mengi nchini.
Kutokana na mtiririko huo mdogo wa maji,
vina vya mito na mabwawa vinatarajiwa kupungua katika msimu wa vuli mwaka huu.
"Mlipuko wa magonjwa unaweza
kujitokeza na uhaba wa maji salama na matumizi mabaya ya mifumo ya majitaka
katika miji,” alisema.
Alisema uhaba wa malisho kwa wafugaji na
wanyama unatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi kutokana na kupungua kwa maji kwenye
mabwawa na visima.
Uratibu
Msuya alisema Idara ya Maafa inatoa hadhari
kwa wizara, taasisi za Serikali, mamlaka za mikoa na wadau wengine wa usimamizi
wa maafa, kuchukua hatua muhimu kukabiliana na tatizo hilo.
Alisema wakulima wanatakiwa kulima mazao
ya muda mfupi na yanayostahimili ukame ikiwa ni pamoja na kuhifadhi.
"Pia nawasihi wananchi ili
kukabiliana na kipindi hiki kuna haja ya kuchimba au kukamilisha na kukarabati
mabwawa na malambo kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua," alisema.
Brigedia Jenerali Msuya alisema maofisa
ugani wote ambao wameajiriwa, sasa ni kipindi sahihi cha kufanya kazi rasmi ili
kutoa ushauri kwa wakati kuhusu mazao ya kupanda.
Aliwataka wafugaji kuhifadhi chakula kwa
ajili ya malisho ya mifugo na kuvuna mifugo, ikiwa katika hali nzuri kiafya,
ili kupunguza idadi kubwa ya mifugo katika kipindi cha uhaba wa malisho ambapo
inaweza ikafa kwa wingi na kupata hasara.
Pia alizitaka taasisi hizo kudhibiti
usafirishaji holela wa mazao ya chakula kwenda nje ya nchi.
Usalama
wa chakula
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya
Usalama wa Chakula, Marystela Mtalo alisema idara yake itahakikisha inafanya
kazi ya uratibu, ufuatiliaji, ukusanyaji na utoaji taarifa ya chakula nchini
kwa wakati.
Alisema Bodi ya Nafaka inaelekeza nguvu
kununua mazao ya wakulima kwa wingi ili kuongeza wigo wa biashara na soko la
mazao ya wakulima, sambamba na kuyaongeza thamani.
Mtalo alisema mikoa na halmashauri zake
zihamasishe na kufuatilia kwa karibu akiba ya chakula kwa wafanyabiashara ili
kuwezesha kupata takwimu sahihi za kiasi cha chakula kilichopo nchini.
Alibainisha kuwa taasisi husika
zihamasishe uwekezaji katika viwanda vya usindikaji mazao ili kuyaongeza
thamani.
Uchunguzi uliofanywa na JAMBO LEO katika
mikoa mbalimbali imeonekana kuwa hali ya upungufu wa chakula imeanza
kujitokeza.
Limebaini kuwa wakulima katika mikoa ya
kanda ya kati, Mashariki na Kaskazini hawakuvuna vyakula vya kutosha kutokana
na ukame kuathiri mazao mengi, hasa mahindi na maharage.
JAMBO LEO lilitembelea baadhi ya maeneo
ya Jiji la Dar es Salaam na kubaini kwamba bei ya mahindi imepanda kutoka Sh 650
kwa kilo mwezi uliopita hadi Sh 800 na Sh 1,000 mwezi huu.
Unga wa sembe umepanda kutoka Sh 24,000
kwa mfuko wa kilo 25 hadi kufikia Sh 27,000 na Sh 30,000. Unga wa sembe kwa bei ya rejareja nao
umepanda kutoka Sh 1,000 hadi kati ya Sh 1,200 na Sh 1,500.
Katika mkoa wa Ruvuma bei haijabadilika
sana. Mahindi kwa kilo ni Sh 520 kwa wafanyabiashara
wanaotoka nje, Sh 510 wafanyabiashara wa ndani na bei ya gunia la kilo 100 ni Sh
52,000.
Inasemekana bei hiyo inatokana na
mahitaji ya chakula kwa baadhi ya nchi jirani na kuwa bei ya unga kwa kilo ni Sh
1,000 na mchele kilo ni Sh 2,200.
Katika mkoa wa Morogoro bei ya mchele
inategemea ubora wake ambapo bei inaanzia
Sh 1,500 kwa kilo hadi Sh 1,000.
Mfanyabiashara Luth Kalikene wa Mbeya
alisema kipindi cha mwezi wa mavuno walikuwa wakiuza kilo 20 sawa na debe moja kwa
kati ya Sh 17,000 na Sh 18,000.
Kwa sasa alisema bei ya jumla ni kati ya
Sh 25,000 hadi Sh 28,000 kutegemea na aina ya mchele huku bei ya reja reja ikipanda
hadi Sh 32,000 kwa kilo 20.
Mkoani Kilimanjaro bei
ya mahindi imepanda kutoka Sh 50,000 kwa gunia la kilo 100 hadi Sh 65,000.
Aidha, alisema kutokana
na kupanda kwa bei ya zao hilo, unga wa mahindi umepanda kutoka Sh 1,000 hadi Sh
1,200 kwa kilo.
Mkoani Tanga mahindi
gunia ni kati ya Sh 68,000 na Sh 70,000 tofauti na miezi miwili iliyopita
ambapo liliuzwa chini ya Sh 60,000.
Kigoma mmiliki wa
mashine za kusagisha nafaka, Jiti Rubibi
alisema mwanzoni mwa Septemba debe la
mahindi liliuzwa Sh 11,000 lakini sasa limepanda hadi Sh 13,000.
0 comments:
Post a Comment