Dk Philip Mpango
|
MKUTANO wa Tano
wa Ushirikiano kati ya Afrika na Korea Kusini (KOAFEC), ulifunguliwa jana
jijini hapa, ajenda kuu ikiwa ni namna nchi za Afrika zinavyoweza kutumia kilimo
katika muktadha wa maendeleo ya viwanda ili kujikwamua kiuchumi.
Katika mkutano
huo unaohusisha nchi 54 za Afrika na Korea Kusini, Rais John Magufuli
anawakilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, ambaye aliuelezea
kuwa utaleta mapinduzi katika nchi za Afrika ikiwamo Tanzania kwa kuwekeza kwa
kiasi kikubwa kwenye kilimo, rasilimaliwatu na Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano-TEHAMA.
Dk Mpango
alisema licha ya Korea Kusini kupata uhuru mwaka mmoja na Ghana, mwaka 1954
miaka michache kabla ya Tanzania Bara, imepiga hatua kubwa kimaendeleo na kuwa
moja kati ya nchi za dunia ya kwanza kiuchumi, lakini Ghana na Tanzania bado ni
masikini.
“Ni jambo zuri,
tuimarishe ushirikiano na Korea Kusini ili njia walizotumia kupiga hatua kubwa
kimaendeleo, nasi tuweze kujifunza kwa haraka,” alisema Dk Mpango.
Alisema baadhi
ya mawaziri wa fedha aliozungumza nao walisema uongozi thabiti wa nchi na uwekezaji
mkubwa katika rasilimaliwatu na kilimo cha kisasa, vinaweza kukwamua nchi za Afrika
kuondokana na umasikini.
“Ni muhimu elimu
na ujuzi tuvisisitize tunapoanza hatua ya kujenga Tanzania mpya kwa nguvu
zaidi, lakini jambo lingine ni kwamba kilimo ndio msingi ambao watu wengi
wanaishi wakitegemea hivyo mkutano huu unaendana na mkakati wetu wa Mpango wa
Pili wa Maendeleo wa Taifa,” alisema Dk Mpango.
Mkuu wa Idara ya
Utafutaji Rasilimali kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Sabra Issa Machamo
alisema uhusiano wa Zanzibar na Korea Kusini ni wa kuigwa na nchi hiyo
inafadhili mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji unaotarajiwa kujengwa
visiwani humo.
Awali akifungua
mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu wa Korea Kusini, ambaye pia ni Waziri wa Fedha,
II Ho YOO, alisema Serikali yake imeamua kuwekeza kiasi kikubwa cha rasilimali
zake kuendeleza nchi za Afrika kupitia sekta za kilimo, rasilimali watu na
viwanda.
Alisema mkazo
mkubwa utakuwa kushirikisha sekta binafsi kusisimua uchumi wa nchi
zinazonufaika na mpango huo ili kuharakisha maendeleo yao.
0 comments:
Post a Comment