Fidelis Butahe na Sharifa Marira
MENGI yametokea saa 24 baada ya kuibuka
kwa mvutano kati ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema na Mkuu wa
Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kwenye uzinduzi wa mradi wa Sh bilioni 9, ikiwemo taarifa feki ya Ikulu
kuwa Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa mteule wake huyo.
Lema na mkuu huyo wa mkoa walizua
tafrani hiyo juzi mjini Arusha katika hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa hospitali
itakayohudumia bure kina mama na watoto, mbele ya wafadhili wa mradi huo, taasisi
ya Martenity Africa.
Sakata hilo liibuka baada ya Gambo kutoa
historia ya mradi huo, akimtaja wakili Nyanga Mawalla kuwa ndiye aliyetoa eneo
kwa ajili ya ujenzi huo, jambo ambalo Lema alilipinga akisema mteule huyo wa
Rais anapotosha ukweli.
Sakata hilo lilizua sintofahamu na
kusababisha polisi kuingilia kati na kuwatawanya wananchi waliokuwa wakimzomea
mkuu huyo wa mkoa, huku wafadhili hao wakishikwa na butwaa.
Mwendeleo wa mvutano wa viongozi hao
wawili ambao wameanza uhasama siku nyingi jana ulichukua sura mpya baada ya
kuiteka mitandao ya kijamii huku watu wa kada mbalimbali, wakiwemo wanasiasa,
wakimshambulia Gambo na wengine kumlaumu Lema kuwa alipaswa kuwa mtulivu.
Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo),
Zitto Kabwe alisema, “Nakasirishwa sana kuona viongozi vijana wanafanya mambo
ya hovyo. Mkuu wa mkoa wa Arusha mdogo wangu Mrisho Gambo una dhamana zaidi kwa
vijana. Mnapofanya mambo ya kijinga mnaharibu nafasi ya vijana kuaminiwa
zaidi.’’
“Kaa na Lema mnywe kahawa pale New
Arusha na muanze upya. Ndugu yangu Lema nashauri punguza munkari. Juhudi zako
Arusha haziwezi kufutika kirahisi. Nakushauri kaa chini na mkuu wa mkoa wako
mpige mstari muanze Kazi upya kwa pamoja. Viongozi jiepusheni kuonyesha hasira
zenu hadharani sio hekima’’
Mbunge wa Momba (Chadema),David Silinde
aliandika katika ukurasa wake wa Facebook ‘’Hii ni edited leter (barua ya
kughushi) yenye lengo la kum-prempty mhe rais asichukue hatua aliyoopanga
kuichukua hii haijatengenezwa kwa lengo zuri ,kwa hili mmeharibu kila kitu’’.
Aliyekuwa Meya wa Kinondoni,Boniface
Jacob,alisema hajaona jipya juu ya kilichotokea kutokana na kwamba wakuu wa
mikoa na wilaya wamepewa maagizo maalum ya kukwamisha wapinzani katika
maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano.
Kwa nyakati tofauti aliyekuwa Katibu
Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza na Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi
walimpongeza Rais Magufuli kwa kutengua uteuzi wa Gambo, jambo lililoonyesha
wazi kuwa walisoma taarifa feki ya Ikulu, kuiamini na kutoa maoni yao.
Akizungumzia taarifa hiyo feki ya Ikulu,
mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde katika ukurasa wake wa facebook
alisema, “hii ni barua ya kughushi yenye lengo la kum-prempty Rais ili asichukue
hatua aliyopanga kuichukua. Hii haijatengenezwa kwa lengo zuri. Kwa hili
mmeharibu kila kitu.”
Aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni,
Boniface Jacob alisema,“atakayekwamisha vizuri anapewa promotion, hao wakuu wa
mikoa na wilaya wanapewa mafunzo maalum ya kukwamisha wapinzani katika maendeleo
,atakayeonekana anawapa ushirikiano atahamishwa eneo hilo ili aletwe
mvurugaji’’
Jacob ambaye ni diwani wa Kata ya
Ubungo, alisema Serikali haijali juu ya kukosa au kupoteza mradi wa mabilioni
ya fedha kutoka kwa wahisani hao na
kudai aliwahi kushuhudia wafadhili wakielezwa kuondoa Sh bilioni 3.2 katika
manispaa aliyokuwa anaiongoza.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment