Waandishi Wetu
Japhet Elia Stephano |
KINARA wa matokeo ya darasa la saba,
Japhet Stephano wa Shule ya Msingi Kwema wilayani Kahama mkoani Shinyanga
ambaye ni mtoto wa mjasiriamali Elia Ntinyako ametaja siri ya mafanikio yake kuwa
ni kumwomba Mungu, kusoma kwa bidii na kusikiliza walimu na wazazi.
Stephano alisema hayo jana katika
mahojiano maalumu na JAMBO LEO muda mfupi baada ya matokeo ya Mtihani wa
Kumaliza Elimu ya Msingi kutangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA)
Dar es Salaam.
Alisema amelelewa katika maadili na
kanuni za imani ya dini yake, pamoja na kutojihusisha na michezo na makundi
yasiyo na sababu.
“Nilikuwa napenda masomo yote, ila siri
kubwa ya ushindi ni kumwomba Mungu na kufuata maelekezo mema ya wazazi wangu
ambao mara kwa mara walinisimamia katika masomo ya kawaida nay a ziada ili
kutimiza ndoto zangu. Nitahahikisha hata kidato cha nne naongoza pia,” alisema.
Alisema awali hakutarajia kuwa
angeongoza kutokana na ushindani ulivyokuwa mkubwa shuleni kwao ambapo kuanzia
darasa la kwanza walikuwa wakigombea nafasi ya kwanza hadi tano.
Stephano alisema malengo yake ya baadaye
ni kuwa Mhandisi wa Ujenzi wa Miundombinu na kwamba anajua hilo linahitaji
aongeze bidii na juhudi katika masomo.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa
aliyokumbana nayo katika kutafuta elimu hiyo kukosa kushiriki michezo na
wanafunzi wenzake, kwani muda mwingi aliutumia kujisomea.
Baba wa mwanafunzi huyo, Ntinyako
alisema siri ya mafanikio ya kijana wake ni kujisomea na kuwasikiliza kile
ambacho wanamwelekeza.
Alisema walichofanya ni kuhakikisha
wanafuatilia masomo kwa kuwasiliana na walimu na kukagua madaftari wakati wa
likizo na anaposoma masomo ya ziada.
“Kwanza alihakikisha hashiriki starehe
za kwenda fukweni, ingawa tunaishi karibu na Ziwa Tanganyika ambako kuna zaidi
ya fukwe tatu,” alisema.
Ntinyako alisema pamoja na ugumu wa
maisha alihakikisha anasomesha watoto wake kwenye shule nzuri akiamini kuwa
elimu ndiyo mkombozi wao na kutaka Watanzania wasiogope kusomesha watoto kwenye
shule hizo.
“Sisi ni wajasiriamali lakini tumejikaza
kisawasawa ili watoto wetu waweze kupata elimu bora ambayo itawasaidia na
matunda yake ndiyo kama leo (jana) mnatupigia simu kutupongeza,” alisema.
Jamal Athumani aliyeshika nafasi ya pili
kitaifa alisema siri ya mafanikio yake ni kusoma kwa bidii, kumwomba Mungu, ushirikiano
kati yake, walimu, wanafunzi wenzake na wazazi.
Jamal alisema walimu wamekuwa na mchango
mkubwa katika mafanikio yake kwa kufundisha vizuri na kuahidi kuwa ataendelea
kusoma kwa bidii ili afanye vizuri zaidi ngazi zinazofuata.
Mwanafunzi huyo alisema maisha ya
nyumbani kwao ni ya kawaida huku akimpongeza mzazi wake, Dk Asha Maneno kwa
kumlea vizuri na kuhakikisha anafaulu.
Mzazi huyo naye alisema amefurahishwa na
matokeo ya kijana wake kwani kila mara alikuwa akimsisitiza kusoma kwa bidii,
nidhamu na mnyenyekevu kwa Mungu na wanadamu.
Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya tatu kitaifa
ambaye pia anatoka Shule ya Msingi Kwema, Enock Bundala alisema malezi mazuri
kutoka kwa wazazi wake ambao muda mwingi walimsimamia kwa karibu katika masomo
yake ndiyo siri ya mafanikio yake.
“Napenda masomo ya Sayansi, Hisabati na
Jiografia, natamani niwe mhandisi, nawasihi watoto wenzangu wakiwa darasani
wazingatie anachofundisha mwalimu kwani ndiyo siri ya mafanikio, pia kumwabudu
na kumpa nafasi zaidi Mungu,” alisema.
Baba wa mwanafunzi huyo, Daud Bundala
alisema matokeo hayo aliyatarajia kutokana na mtoto wake kujisomea kwa bidii na
kumwabudu Mungu hivyo anajipanga zaidi kumwendeleza.
Mama wa Enock, Anastazia Shija alisema:
“Jina la Mungu lihidimiwe. Siri ni malezi bora kwa mtoto, hasa kuepuka makundi
rika maovu na kusimamia kwa umakini matendo yake kuanzia nyumbani hadi
matembezini kwa kubaini aina ya marafiki.”
Katika hatua nyingine, mama wa
mwanafunzi bora wa kike,Justina Gerald kutoka Shule ya Msingi Tusiime ya jijini
Dar es Salaam, Dk Edna Majaliwa alisema amefurahi binti yake kuongoza wasichana
wote wa Tanzania kwani alikuwa anajitahidi shuleni.
“Mwanangu alikuwa msikivu, alijituma na
alikuwa anafanya uamuzi mkubwa kama mtu mzima ila shangazi yake alimtabiria
kuwa atakuja kuwa wa kwanza siku moja,” alisema.
Dk Majaliwa ambaye ni bingwa wa magonjwa
ya watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alisema Justina anapenda
kusoma vitabu, kuangalia filamu na kusaidia watoto wa mitaani.
Akizungumzia shule yake kuwa ya kwanza
kitaifa, Mkurungezi wa Shule ya Msingi Kwema, Pauline Mathayo alisema siri
kubwa ya mafanikio yake ni kumtanguliza Mungu katika shughuli zake pia jitihada
za walimu wanaofundisha kwa weledi.
Alitoa mwito kwa walezi na wazazi
wasichanganywe na ukali wa maisha ya sasa na yajayo kwa kuwa jukumu lao ni kuongoza
watoto katika malezi bora na si bora malezi.
“Kwanza wawafundishe Neno la Mungu na
kudhibiti michezo isiyo na tija,” alisema.
Alitaja sababu nyingine ya watoto
kufanya vizuri kuwa ni ushirikiano wa wazazi, walimu na wanafunzi, akisema
wazazi wamekuwa wakiwafuatilia watoto wao kwa karibu.
Mathayo alisema shule hiyo ina walimu 31
ambao ni Watanzania wote na darasa hilo lilikuwa na wanafunzi 50.
Meneja wa Shule, Emanuel Ang’ulo alisema
ushindi huo umetokana na ukaribu wa Mkurugenzi wao kwa walimu wake kuwajali
kimaslahi hali inayowapa moyo wa kuwa na bidii ya kufundisha na kuwajenga
kisaikolojia.
Mkuu wa Shule, Michael Luhaga ambaye ni
mwalimu wa Sayansi, alisema alitarajia matokeo hayo kutokana na juhudi zilizokuwa
zikioneshwa na wanafunzi hao.
Mwalimu wa darasa la saba, Adili
Majogolo alisema Japhet alikuwa na uwezo mkubwa kitaaluma na alipenda zaidi
masomo ya Sayansi akiwa na ndoto za kuwa mwanasayansi siku zijazo.
“Amekuwa akishika nafasi ya kwanza na
wakati mwingine ya pili au ya tatu, hakuwahi kushuka zaidi ya hapo,” alisema.
Alisema Jamal na Enock wanapenda kusoma na
ni watulivu hali ambayo ilisababisha wasaidiane kwenye masomo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tusiime,
Philibert Simon alisema mwanafunzi huyo alikuwa akiongoza katika mitihani ya
ushindani iliyokuwa ikifanyika ambapo kati ya mitihani 32 alikuwa anaongoza 19.
Alisema mwanafunzi huyo amekuwa wa kipekee
kwenye usomaji na kuna wakati ukifika muda wa kupumzika na wanafunzi kuungana
kucheza alikuwa haendi na badala yake alijificha na kujisomea.
Mkurugenzi Mkuu wa Tusiime, Albert Katagira
aliishukuru Serikali kwa kubadili mfumo wa alama katika upangaji matokeo na
kwamba wangekuwa nafasi ya juu zaidi.
Habari
hii imeandikwa na Suleiman Msuya, Celina Mathew, Magreth Magoso na Neema Sawaka
0 comments:
Post a Comment