Celine Mathew
SERIKALI
za Tanzania na Morocco zimetiliana saini mikataba 21 ya kiuchumi na biashara,
huku Mfalme wa Nchi hiyo, Mohammed VI akikubali maombi ya Rais John Magufuli
kujenga Msikiti mkubwa Dar es Salaam na uwanja mkubwa wa mpira Dodoma,
vitakavyoanza kujengwa mara moja.
Utiaji
saini mikataba hiyo ulitangazwa jana Ikulu, Dar es Salaam katika siku ya pili
ya ziara ya siku sita ya Mfalme huyo, kati ya mikataba hiyo ukiwamo wa usafiri wa anga kutoka Rabat hadi Dar es Salaam na askari 150
kwenda nchini humo wiki ijayo kwa ajili ya mafunzo.
Akizungumza Ikulu, Rais Magufuli
alisema historia kati ya Tanzania na Morocco ilianza kujengwa miaka ya 1631 na
kwamba mikataba hiyo itaisaidia Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025.
“Namshukuru Mfalme kwa kuja na
wafanyabiashara, lakini katika maongezi yake ameniambia kuwa mwaka jana, nchi
hiyo ilipokea watalii zaidi ya milioni 10.5 na kwamba mwaka huu wanatarajia
kupokea milioni 14,” alisema.
Alisema Mfalme huyo alimhakikishia kuwa
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), litashirikiana na la Morocco kuhakikisha
usafiri unakuwa mzuri na ndege zinasafiri kutoka nchini humo hadi Dar es
Salaam.
Rais Magufuli alisema Mfalme huyo alimhakikishia
kuwa nchi hiyo itashirikiana na Tanzania, lengo likiwa ni kukuza uchumi
unaotarajiwa kufikia asilimia 7.9 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Aliongeza kuwa Tanzania ipo kwa ajili
ya kujenga uchumi wa kisasa kutokana na uwepo wa madini tofauti hivyo kumhakikishia
Mfalme huyo kuwa ni eneo zuri la kuweka wawekezaji.
Hata hivyo, Rais Magufuli alisema
Mfalme huyo alimwomba aongeze siku moja nchini ambapo alimruhusu na kumsisitiza
kuwa hata kama anataka tatu akae tu.
Mikataba
Mikataba hiyo ni pamoja na makubaliano
ya jumla katika ushirikiano wa kiuchumi, Sayansi, kiufundi na kitamaduni baina
ya Serikali ya Morocco na Tanzania ambao ulisainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga na Waziri wa Mambo ya
Nje wa Morocco, Alahddine Mezouar.
Mkataba mwingine ni wa kuanzishwa kwa
Jukwaa la Ushauriano wa Kisiasa baina ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania na
Morocco kati ya Dk Mahiga na Mezouar wa Morocco.
Mwingine ni wa sekta ya gesi, nishati,
madini, sayansi ya miamba kati ya Tanzania na Morocco ambao ulisainiwa na
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mezouar.
Aidha, mkataba wa usafiri wa anga baina
ya Tanzania na Morocco ambao ulisainiwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Mezouar.
Mkataba wa Mradi wa Mtangamano wa
kuwasaidia wakulima wadogo nchini ambao ulisainiwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi, Dk Charles Tizeba na Aziz Akhannouch wa Morocco.
Pia mkataba wa sekta ya uvuvi ambao
ulisainiwa na Dk Tizeba na Akhannouch, Mkataba wa Maendeleo ya Nishati mbadala
baina ya MASEN na Wizara ya Nishati na Madini ambao ulisainiwa na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa na Mwenyekiti wa MASEN, Moustapha
Bakkoury.
Mkataba kati ya Bodi ya Utalii nchini
pamoja na Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Ofisi ya Utalii ya Taifa la Morocco ambao
ulisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji, Devota Mdachi na Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya
Taifa ya Utalii Morocco, Abderrafie Zouiten.
Mingine ni kundi la utoaji mikopo la
Morocco na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, Shirika la Bima la Taifa
Tanzania (NIC), Shirika la Bima la Morocco (MAMDA) kwa ajili ya maendeleo ya
bima ya mazao nchini.
Aidha mkataba baina ya kundi la SNTL la
Morocco na Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji (EPZA), ya Tanzania katika
ubia wa uendelezaji na utangazaji wa nguzo za viwanda.
Pia mkataba baina ya Mamlaka ya
Usafirishaji ya Taifa ya Morocco na kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli
Tanzania (RAHCO), kwa ajili ya ubia ili kuendeleza reli ya Mtwara-Mchuchuma/
Liganga.
Mwingine ni kati ya Baraza la Bishara baina
ya Shirikisho la Wafanyabiashara wa Morocco (CGEM) na taasisi ya Sekta Binafsi
Tanzania (TPSF), baina ya Benki ya BOA na Hospitali ya CCBRT ili kuiwezesha
kujiendesha.
0 comments:
Post a Comment