Sharifa Marira, Dodoma
MAMBO manne makubwa yanatajwa kuibuka katika Mkutano wa
Bunge la 11 utakaoanza vikao vyake kesho mjini Dodoma.
Mkutano huo wa Tano utakuwa wa wiki mbili, lakini uliojaa
matukio makubwa, yakiwamo uchunguzi wa mkataba wa Kampuni ya Lugumi Enterprises
na Jeshi la Polisi, mvutano wa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka
2016, sakata la ubio linaloihusisha Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)
na utekelezaji wa robo bajeti ya mwaka 2016/17.
Wakati wabunge waliozungumza na JAMBO LEO wakitaja mambo
hayo, tayari ripoti ya utekelezaji wa mkataba wa kampuni ya Lugumu iliyopewa
kandarasi ya kufunga vifaa vya utambuzi wa vidole katika vituo vyote vya Jeshi
la Polisi nchini, imekabidhiwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projestus
Rwegasira.
Pia, Muswada wa Habari unaopigiwa chapuo na Serikali kuwa
ni mzuri, umepingwa na wadau mbalimbali wa tasnia hiyo, likiwemo Jukwaa la
Wahariri (TEF), huku sakata la NSSF na utekelezaji wa bajeti vikiteka vichwa
vya habari takribani wiki tatu sasa.
Mbunge wa Kibamba na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John
Mnyika alisema, “kama kuna jambo litatikia Bunge basi ni huu Muswada. Una utata
mwingi na wengi wameupinga…, sijui itakuwaje kwa kweli.”
Alisema muswada huo una maudhui ambayo si rafiki kwa
wanahabari na vyombo vya habari, jambo ambalo wadau wa tasnia hiyo hawatakubali
kuona ukipita bila marekebisho au kuondolewa kabisa ili kutoa muda zaidi
kuujadili.
Kuhusu utkelezaji wa bajeti iliyopitishwa Julai Mosi
mwaka juu, Mnyika alisema Serikali itakapokuja na mipango na miongozo kuhusu
masuala mbalimbali huenda ikapingwa na wabunge ambao wamekuwa na utaratibu wa
kuhoji kwanza utekelezaji wa bajeti.
“Kuna hili suala la Lugumi. Hii kampuni ilipewa zabuni ya
kufunga mashine za utambuzi wa vidole katika vituo vya polisi. Mpaka hatua ya
mwisho ilipewa miezi mitatu kukamilisha kazi hiyo na tayari muda huo
umeshapita. Wabunge lazima wahoji ili kujua kama suala hilo limefanyika,”
alisema.
“Pia kuna hili suala la NSSF kuhusu mradi wa ubia baina
yake na Kampuni ya AHEL (Azimio Housing Estates) ambao umeonesha kuwa shirika linaweza kupoteza kiasi cha Sh bilioni 270.
Kama wabunge lazima tuhoji jambo hili ili kupata maelezo ya kina. Sidhani kama
kuna mbunge atakubali kufumbia macho.”
Mkataba huo unaonesha mbia huyo alipaswa kuwa na ekari
20,000 na ndizo alizotaja katika
mkataba huo lakini kiuhalisia baada ya kufanya tathmini zipo ekari zaidi ya
3,500.
Pia bei
iliyothaminiwa kwenye ekari hizo ni tofauti kwani mwekezaji huyo alithaminisha
ardhi hiyo kwa Sh milioni 800, lakini baada ya NSSF kufanya uchunguzi wake
ikabaini kuwa ekari moja thamani yake ni Sh milioni 25.
Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga alisema pamoja na
mambo mengine yatakayoletwa mbele ya Bunge, muswada wa habari ndio utakaotikisa
kwa kiasi kikubwa.
‘’Tumeshaona mshike mshike wa muswada huu kabla hata
haujaletwa bungeni hivyo naona ni jambo kubwa litakaloletwa mnyukano mkali
,nyie wenyewe waandishi mnajua’’ alisema.
Mbunge wa Jimbo la Bukombe (CCM), Doto Biteko, “ratiba
kamili ya vikao tutaipata kesho (leo) baada ya kikao cha kamati uongozi lakini
uhalisia mambo ambayo yameonekana kuzua mjadala ni muswada huo wa habari ambao
ukiletwa tunatarajia utakuwa na mchuano mkali lakini wenye mantiki na
namna ya kusaidia tasnia hii ya habari’’alisema Biteko
Mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa (CCM) naye
aliugusia muswada huo wa habari ndio utakaokuwa mwimba mchungu ndani ya wabunge
kwa maelezo kuwa katika vikao vya kamati za Bunge, ulizua mvutano mkali.
0 comments:
Post a Comment