Suleiman Msuya
MWAKA mmoja tangu Uchaguzi Mkuu ufanyike nchini,
aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amesema
alishindwa kutokana na Tume ya Uchaguzi isiyo huru.
Aidha, Waziri Mkuu huyo wa zamani amesema pamoja na
mafanikio machache katika baadhi ya maeneo kwenye utawala wa sasa, maisha ya
Watanzania yamezidi kuwa magumu.
Lowassa alisema hayo kwenye taarifa yake aliyoitoa kwenye
vyombo vya habari jana, mwaka mmoja baada ya Watanzania kupiga kura Oktoba 25
mwaka jana, ambapo alisema anasononeshwa na hali ya sasa ya Watanzania na ingawa
bado ana ari, nguvu na hamasa katika mapambano ya kisiasa.
“Hatutaki kuendelea kulilia maziwa yaliyokwishamwagika
ambayo hayazoleki, lakini kile ambacho tulikisema wakati ule kwa nini tunataka
mabadiliko, hivi sasa kila mtu anakiona,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Ajira imeendelea kuwa bomu linalosubiri kulipuka, elimu
bure iliyoahidiwa sivyo inayotekelezwa, utumishi wa umma umekuwa kaa la moto.”
Alisema anakumbuka Oktoba 25 mwaka jana, akisema ilikuwa
siku muhimu kwa Watanzania na yeye binafsi, ambapo aliongoza wananchi kupiga
kura akiwa mgombea wa upinzani.
“Naamini nilileta sura na msisimko mpya katika siasa za
Tanzania,” alisema Lowassa.
Aliongeza:“Nilishirikiana na wenzangu kuionesha nchi
demokrasia maana yake ni nini na kuwa kukosekana kwa Tume ya Uchaguzi iliyo
huru ni sababu ya sisi kushindwa.
“Ninapogeuka nyuma kuingalia siku ile, nasikia faraja
kubwa sana hasa kwa jinsi Watanzania walivyotuunga mkono na kuonesha matumaini
makubwa kwetu.”
Alisema katika kipindi hicho, mkewe Regina naye alionesha
ujasiri na ushupavu wa hali ya juu ambao ulimpa nguvu kubwa.
Hata hivyo, alisema kwa hali ilivyo sasa, anasononeka kuona
viongozi wanavyoshindana kuweka ndani madiwani na viongozi wengine wa
kuchaguliwa hasa wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mbunge huyo mstaafu wa Monduli alishukuru wananchi kwa imani
waliyoonesha kwake na Ukawa na kwamba kumalizika kwa uchaguzi mmoja ndio mwanzo
wa uchaguzi mwingine.
“Mapambano ndiyo kwanza yameanza. Kwa kasi, nguvu, ari na
hamasa niliyonayo ni kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote,” alisema
Lowassa.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema alisema chini ya
Mwenyekiti Freeman Mbowe, waliendesha kampeni za kiungwana kama walivyoahidi.
“Upepo ule ulivuma kwa kasi mpaka visiwani ambako Maalim
Seif Sharif Hamad aliporwa dhahiri ushindi,” alisema.
Uchaguzi uliofanyika mwaka jana matokeo ambayo
yalitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Lowassa alipata kura zaidi ya milioni 6.7 huku Rais
John Magufuli akipata kura zaidi ya milioni 8.9.
0 comments:
Post a Comment