Sharifa Marira, Dodoma
Azimio Housing Estates |
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limekiri kuwapo
ubadhirifu kwenye mkataba wa ubia na Kampuni ya Azimio Housing Estates iliyotakiwa
kuendeleza ekari 20,000 za ardhi Kigamboni na kuna hatari ya kupoteza Sh bilioni
270.
NSSF pia imekiri ubadhirifu katika utoaji mikopo kwenye
Saccos mbalimbali nchini ikiwamo ya Bumbuli, inayoonekana kukopeshwa zaidi ya Sh
bilioni mbili, bila kuwa na sifa huku kukiwa pia hakuna kumbukumbu ya mwaka
mzima kama walirudisha mkopo wa awali.
Mwenyekiti wa Bodi ya NSSF, Profesa Samuel Wangwe
alieleza jana mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwamba Bodi yake
ilipoingia madarakani iligundua ubovu wa mkataba huo na kusitisha kutoa fedha
na sasa inaangalia namna ya kujitoa bila kupoteza fedha zilizowekezwa.
Alisema uwekezaji huo ambao ardhi ya mwekezaji ilipaswa
kuwa ekari 20,000, hatua ya awali ulipaswa kuanza na ekari 300, lakini
uchunguzi uliofanyika hivi karibuni ulionesha kuwa kuna ekari 3,500 pekee hali
inayoonesha udanganyifu uliofanyika tangu awali.
Pia mwekezaji huyo alidanganya uhalisia wa bei ya ardhi
hiyo, kwani alionesha kuwa thamani ya ekari ya moja ni Sh milioni 800 wakati kiuhalisia,
ardhi hiyo thamani yake ni Sh milioni 25 peke yake.
Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka alisema imekuwa
vigumu kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
kuthibitisha uwepo wa viwanja hivyo kwa kukosekana hatimiliki, umiliki wa
ekari 19,700 za ardhi ambazo ni sehemu ya mtaji wa Azimio Housing Estates kwa
asilimia 20, hivyo fedha za NSSF zinakuwa kwenye hatari ya kupotea.
Alisema NSSF ambayo inamiliki hisa ndogo kuliko Azimio,
imewekeza fedha nyingi, zaidi ya dola milioni 129 za Marekani wakati mbia huyo
aliwekeza dola milioni 5.5.
Akijibu hoja za Mwenyekiti huyo, Profesa Wangwe alisema mradi
huo ulisimama tangu Februari kutokana
na mbia kukosa fedha na kwamba hakopesheki kwani NSSF inamdai.
Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige alisema mradi huo wa Kigamboni ni mchafu na
katika mazingira hayo ambayo Bodi pia imeshituka kuwa mchafu hivyo
ni vema NSSF ingejitoa kuliko kuendelea na mkataba mbovu.
“Ni vema ukishagundua kuwa unachezea kitenesi kichafu
ambacho kilianza kuchezewa na watu ambao wameshaondolewa, usiendelee kucheza na
mtu yule yule ili asije kukuingiza katika matatizo makubwa zaidi,” alisema
Maige.
Profesa Wangwe alisema ni vigumu kujitoa haraka kwenye
mkataba huo, kutokana na fedha nyingi waliyowekeza ambayo iko hatarini kupotea
na kwamba ardhi yote ni ya mwekezaji huyo hivyo wanatafuta namna ya kurudisha
fedha waliyowekeza hata kama haitakuwa na faida.
Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aesh Hilaly alihoji kama
mkataba unaruhusu mwekezaji huyo kukopa ili kuendeleza mradi huo.
Mkurugenzi wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema
mwekezaji huyo alitaka kukopa NSSF ili aendeleze mradi huo ambao umesimama
lakini hakopesheki kwa kuwa anadaiwa.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge walihoji uhalali wa Saccos kukopeshwa
mara mbili kwa mwaka, huku zingine zikikosa mikopo na vigezo vilivyotukia
katika kutoa mikopo hiyo.
Kuhusu Saccos ya Bumbuli, Kaboyoka alisema mbunge wake
anafahamika, hivyo inashangaza ipewe fedha hizo kwa mwaka mmoja na kuhoji sifa
zilizotumika kuzitoa wakati Saccoss zingine hazijapata.
Alisema ni vema ufanyike ukaguzi maalumu kwenye Saccos
hiyo kwani fedha hizo ni mafao ya wafanyakazi ingawa pia inatia shaka katika
utoaji, kwani awali Saccos hiyo ilipewa zaidi ya Sh bilioni moja na kwamba
hesabu hazioneshi, kwamba fedha hizo zilirejeshwa, lakini ndani ya mwaka mmoja
ikapewa fedha zingine.
NSSF ilitoa mikopo kwa Saccos tisa kwa kiasi kinachozidi
asilimia 50 ya thamani ya mali za Saccos husika, kinyume na sera ya Shirika ya
kukopesha na ziliomba kiasi ambacho hazikustahili.
Katika ripoti ya CAG mbali na Bumbuli, Saccos zingine
zilizopewa fedha nyingi ni Korongo Amcos, UMMA, SBC, Hekima, Ukombozi, Uzinza,
Harbour na Umoja.
Akijibu hoja hizo, Profesa Wangwe alisema Saccos zilizopewa
fedha zaidi ya mara mbili kwa mwaka ikiwamo ya Bumbuli iliyopewa Sh bilioni
2.473 kwa mwaka 2014/15, wakati anaingia kwenye nafasi hiyo, aliliona hilo kama
tatizo hivyo kuagiza kufanyike ukaguzi maalumu.
Alisema waliokuwa wanasimamia Saccos hizo walisimamiswa
kazi tangu Bodi mpya ilipoingia na kwamba walisitisha kutoa mikopo ya aina
yoyote katika Saccos zote nchini, hadi uongozi wa Shirika utakapoanzisha
utaratibu mpya.
“Watu wote waliohusika na ubadhirifu wameshaondolewa
ofisini, tulishituka kuona namna fedha hizo zilivyotolewa, si zote zilizofika
kwa wahusika, zingine ziliishia kwenye mikono ya watu, tuliona ni vema ufanyike
ukaguzi maalumu,” alisema Profesa Wangwe.
0 comments:
Post a Comment