Sharifa Marira
WAENDESHA bodaboda wa Mbezi, Dar es Salaam wamemwomba
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kuingilia kati suala la
askari Polisi kuwawinda na kuwanyang’anya pikipiki bila makosa ya kueleweka.
Mwakilishi wa madereva hao ambaye hakutaka jina lake
liandikwe gazetini akihofia usalama wake kutokana na kufahamiana na askari
wanaofanya vitendo hivyo, alisema wamechoka kutumiwa kama mashine za kutolea
fedha (ATM) na polisi.
Alisema kumekuwa na migogoro kati yao na polisi kwa
kipindi kirefu, jambo linalowafanya kuwaona kama maadui zao namba moja wa
maendeleo, kwani wanawakamata bila kuwa na makosa na kuwabambikia kesi.
‘’Tukikutana na polisi tunawaona kama maadui zetu, wametufanya
kama ATM zao unakuta mtu huna kosa lolote anakukamata, anakwambia umekatiza katikati
ya barabara ambayo si yako, ukijaribu kujitetea unakuta anataka umpe fedha, hawajali
kwamba hujafanya biashara,’’ alisema.
Alisema imefika hatua wanatamani kuachana na biashara
hiyo ili kuepuka kero wanayokutana nayo kwa askari hao kwani hakuna faida
wanayopata.
‘’Tumekuwa msaada mkubwa kwa polisi, lakini wao
hawatujali, tunaweza kukutana na tukio tukapeleka taarifa kituoni ila wao
wanatuchukulia kama vitega uchumi vyao, kama bodaboda kafanya kosa mkamate mwandikie
faini umwache afanye shughuli zake lakini si kumfuatafuata na kumbambika kesi,’’
alisema.
0 comments:
Post a Comment