Dotto Mwaibale
Profesa Juma Assad |
KATIKA hali
inayotafsiriwa kuwa watendaji wa taasisi za umma sasa wapo kwenye mazingira
magumu, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), imeanza kuzifanyia kazi tuhuma dhidi ya Bodi ya
Michezo ya Kubahatisha (GBT).
Tuhuma hizo
zilizokuwa zikisambazwa kupitia mitandao ya kijamii kwa wiki mbili sasa,
zinaelezwa kuwa ni majungu yasiyo rasmi na yaliyoibuliwa na
watu wasiojulikana dhidi ya GBT na menejimenti yake.
Vyanzo mbalimbali
vya habari kutoka ofisi ya CAG zimedokeza kwamba uchunguzi huo ulitarajiwa
kuanza mapema wiki hii na utahusisha sekta kuu mbili ambazo ni ajira
na idara ya
fedha.
Kwa mujibu wa
chanzo hicho, CAG ameunda timu maalumu kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tuhuma
hizo zinazoikabili taasisi hiyo na menejimenti, baada ya kupokea kitu
kinachoitwa waraka wenye malalamiko kadhaa.
Taarifa zinadai
kuwa Mkurugenzi wa GBT Tarimba Abbas, ameidhinisha matumizi ya zaidi ya bilioni
3.8 kwa ajili ya ununuzi wa jengo la ofisi katika jingo la PSPF.
Pia watoa
taarifa wamedai kwamba, amehusika na kushirikiana na bodi yake kujiongezea
posho pamoja na kurekebisha mishahara yao bila kibali kutoka
katika mamlaka za nchi hususan wizara ya fedha.
Tarimba mwenyewe
jana alikiri kuwepo kwa taarifa hizo, lakini alikataa kuzungumzia kwa undani
akidai sio msemaji na akataka atafutwe GAG.
Taarifa zaidi zimedai
kwamba Tarimba, akiwa Mkurugenzi Mkuu wa GBT amewaajiri watumishi zaidi ya
watano, akiwamo mtu anayetajwa kama ndugu yake wa karibu pamoja na ndugu
wa baadhi ya watu waliowahi kuwa wajumbe wa bodi hiyo.
Inaelezwa pia
kwamba, Tarimba alishirikiana na TRA alikwepa ulipaji wa kodi inayotokana na
malipo yake ya kumalizika kwa mkataba wake wa kazi (gratuity), hatua ambayo
imeikosesha serikali mapato.
Watoa taarifa
walilalamikia hatua ya malipo ya milioni 4.3 kama posho ya mafuta kwa mmoja wa
wakurugenzi wa bodi hiyo, hatua ambayo wamedai inaifanya taasisi hiyo
kuwa katika
mazingira magumu kiutendaji.
Hata hivyo, CAG
Profesa Mussa Idrisa Assad, hakuweza kupatikana kulizungumzia suala hilo, baada
ya kuelezwa kwamba yupo nje ya nchi kwa majukumu maalum ya
kiserikali.
Uchunguzi zaidi
umebaini kwamba uamuzi huo wa CAG umekuja kipindi ambacho tayari kumekuwa na
waraka unaosambaa kwenye ofisi mbalimbali za Serikali na
vyombo vya
habari ikiwamo mitandao ya kijamii, unaoeleza tuhuma hizo dhidi ya menejimenti
ya taasisi hiyo iliyo chini ya Wizara ya Fedha.
0 comments:
Post a Comment