Warioba Igombe
KUPATA elimu iliyo bora ni moja ya haki za
msingi za mtoto, ndio maana malengo ya Serikali yamejikita katika kuendeleza
elimu nchini kwa namna yoyote iliyo bora.
Kuwapatia wanafunzi elimu bora ndiyo
shabaha ya msingi ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014. Pia ni shabaha ya
Sera zilizokuwepo kabla ya hii tangu uhuru mpaka sasa.
Kusaidiana na Serikali, wadau wa elimu
mkoani Morogoro walianzisha Shule ya Sekondari ya Greencity kwa lengo la kuwapatia
wanafunzi elimu bora.
Sekondari ya Greencity ipo Mkundi
Manispaa ya Morogoro. Uongozi wa shule hii unasema umejipanga kuleta mapinduzi
kwenye sekta ya elimu nchini.
Shule hii ilianza rasmi mwaka 2013,
ikiwa na wanafunzi 51 wa kidato cha kwanza, ambao kuanzia Novemba mosi wanatarajia
kuanza mtihani wa taifa wa kumaliza elimu ya kidato cha nne.
Katika matokeo ya mtihani wa moko shule
hiyo imeshika nafasi ya 16 kati ya 47 kwa sekondari zilizopo Manispaa ya
Morogoro.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Greencity,
Jonathan Mwachipa, anabainisha kuwa lengo ya shule yake ni kuhakikisha wanafunzi
wake wanapata matokeo mazuri katika mitihani ya taifa.
Kutokana na lengo hilo, uongozi wa shule
hii umetenga muda wa jioni kila siku wanafunzi kujisomea kwa kupitia masomo
yote waliyofundishwa ili kupata uelewa zaidi.
Mwalimu Mwachipa anaeleza kuwa kitendo
cha wanafunzi kutumia muda wa jioni kujikumbusha masoma waliyofundishwa, kimekuwa
chachu ya matokeo mazuri katika mtihani wa moko ukilinganisha na shule nyingine
ambazo ni kongwe mkoani Morogoro.
“Pamoja na uchanga wa shule yetu, wanafunzi
wamefanya vizuri katika mtihani wa moko. Hii ni dalili nzuri kwa vijana wetu
kuelekea mtihani wao wa mwisho wa taifa kidato cha nne,” anasema.
Anasema kuwa wanafunzi 75 walifanya mtihani
wa moko, na kati yao wasichana ni 31 na wavulana 44, ambapo waliopata daraja la
kwanza walikuwa ni 13 wasichana wakiwa 11 na wavulana wawili.
Mkuu huyo anasema waliopata daraja la
pili ni wanafunzi 21, daraja la tatu 35 na daraja la nne wanafunzi sita, hakuna
aliyepata sifuri. Katika matokeo hayo wanafunzi wengi wamefanya vizuri masomo
ya sayansi hususani somo la baolojia na kemia.
Pamoja na elimu bora inayotolewa darasani,
mkuu huyo anasema mandhari nzuri ya shule na hewa safi inachangia wanafunzi wao
kufanya vizuri katika masomo yao.
“Kwa ujumla kwa sasa shule yetu ina wanafunzi
340 kati yao wasichana ni 239 na wavulana 10,” anasema.
Pia anasema mbali na kutumia njia
mbalimbali zinazofanywa na walimu ili kuhakikisha wanafunzi wanafaulu, wana wastani
ambao ni lazima mwanafunzi aufikie ili aendelee na darasa linalofuata.
“Mwanafunzi kuingia darasa linalofuata lazima
afikishe wastani wa alama 50. Utaratibu huu umewasaidia wanafunzi wengi kufanya
vizuri darasani. Hakuna mwanafunzi anayeingia darasa lingine kwa ‘huruma’ ni
alama tu tulizoziweka ndizo zinamvusha mwanafunzi,” anasema mkuu huyo.
Wastani huo humfanya mwanafunzi atumie
muda mwingi kusoma bila kusukumwa na mtu ili aweze kuvuka hicho kikwazo na
hivyo kufanya vizuri darasani.
Anasema wanafunzi wake wamepania
kuhakikisha wanafanya maajabu kwa kuwa na ufaulu mzuri utakaowawezesha wote
kwenda kidato cha tano.
Mwachipa anasema ili kuhakikisha
inafanya mapinduzi ya elimu nchini, shule tayari imeanzisha kidato cha tano na
cha sita.
Mbali na hayo, anasema ni ukweli ulio
wazi kuwa wamepata mafanikio ya kutia moyo ingawa bado wana kazi kubwa ya kuendeleza
mbele safari.
Wanafunzi wajivunia wastani
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Happiness
Jumanne, anayesoma kidato cha tatu anasema utaratibu wa shule kuweka wastani
ili kila mwanafunzi aufikishe ni mzuri kwani unasaidia kumfanya mwanafunzi
anapojiandaa na mitihani akumbuke kwamba anapaswa kuvuka alama 50 ambazo ni
wastani wa masomo yote.
“Wastani unamfanya mwanafunzi kusoma kwa
bidii kila wakati ili asishindwe kufikisha wastani uliowekwa na shule na hivyo
kwenda darasa linalofuata,” anasema Happiness.
Kwa upande wake, William Jonathan, anayesoma
kitado cha pili anasema wastani wa alama 50 huongeza ushawishi kwa wanafunzi
kusoma kwa bidii.
“Kwa mwanafunzi anayefikisha wastani
uliowekwa na shule humrahisishia mwanafunzi husika kufanya vizuri katika
mitihani ya taifa.
Huu utaratibu humjengea mwanafunzi
kujiamini na kujituma katika masomo yake hivyo kujibu mtihani wowote ule kwa
urahisi,” anasema.
Jina la Greencity lilivyopatikana
Mkuu huyo anasema kuwa shule hiyo
iliamua kutumia jina la Greencity baada ya mmiliki wake, Ramadhan Mrema, kuona
kuwa maeneo ya shule hiyo yana mimea iliyosheheni rangi za kijani.
Anasema mwaka 2013, wakati shule hiyo ikijengwa
kulikuwa na mimea iliyosheheni rangi ya kijani hali iliyomshawishi kutumia jina
la Greencity akiamini kuwa mazingira yao yatakuwa chachu ya maendeleo shuleni hapo.
Changamoto
Kuhusu changamoto, Mwachipa anasema
shule yake inakabiliwa na kutokuwa na uzio na kwamba mikakati yao kwa sasa ni
kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.
0 comments:
Post a Comment