Celina Mathew
SERIKALI imewataka watanzania
wanaomiliki viwanda vidogo, vyakati na vikubwa kushiriki maonesho ya viwanda
vya Tanzania yanayotarajiwa kuanza Desemba 7 hadi 11 mwaka huu katika uwanja wa
maonesho wa Mwalimu Julius Nyerere.
Maonesho hayo yatakayoambatana na kauli
mbiu isemayo ‘Tanzania sasa tunajenga viwanda’ lengo lake ni kuwaaminisha wananchi juu ya falsafa na dhima
ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, na kuhamasisha watanzania kudhubutu kujenga
viwanda kwa kuwakutanisha walioanza siku nyingi na wa sasa.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri
wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema lengo la maonesho
hayo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda ifikapo 2025,pamoja na
kujenga jukwaa la wadau wa sekta ya viwanda kupata fursa ya kujadiliana,
kubadilishana uzoefu na kutangaza fursa zilizopo.
Alisema pia yatatoa fursa za kutoa
taswira ya juhudi za ujenzi wa viwanda kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita,
kutangaza bidhaa na huduma mbalimbali zinazozalishwa nchini ili kutoa hamasa
kwa watanzania kutumia bidhaa na huduma zinazozalishwa na viwanda vilivyopo
nchini.
Aidha alisema yatawaunganisha wenye
viwanda na wazalishaji mbalimbali wa malighafi na huduma nyingine zinazotumika
viwandani, kutoa semina na mijadala ya kitaalam ikihusiana na maendeleo ya
viwanda nchini, kutangaza fursa za masoko ya ndani na nje na kuwezesha watafiti
na wabunifu kujadiliana na wenye viwanda juu ya kuboresha teknolojia za
uzalishaji na Tehama.
Nyingine ni kuwezesha vijana na
wanafunzi kuchangamkia fursa za ajira na masomo ya masuala ya viwanda ikiwemo
kuwajengea tamaa ya kuanzisha viwanda,
kutoa fursa kwa wananchi kutambua viwanda vilivyopo na zaidi kuwajengea hamasa
ili kuwekeza katika ujenzi wa viwanda na mamlaka husika zinazotumia maonesho
hayo kutangaza fursa za uwekezaji katika mikoa yote ya Tanzania ikiwemo maeneo
ya kujenga viwanda.
Alisema katika maonesho hayo
wamelenga kuwakutanisha wadau wote wa
viwanda ambao ni pamoja na wazalishaji wa malighafi, taasisi zinazotoa huduma
kwa wenye viwanda na zinazowezesha bidhaa kutoka kiwandani mpaka mikononi mwa
watumiaji.
“Kama mnavyojua mpango wa pili wa miaka
mitano unatamka wazi kuwa sekta binafsi ndiyo mhimili wa ujenzi wa uchumi wa
viwanda, hivyo maonesho haya mhusika mkuu ni sekta binafsi na serikali sisi ni
wawezeshaji,”alisema.
Aliwataka watakaoshiriki kutembelea
ofisi za mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) zilizopo katika
uwanja wa maonesho wa Mwalimu Nyerere ambao waratibu wake na kusimamiwa na
Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara hiyo na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo
ya Viwanda (UNIDO).
0 comments:
Post a Comment