* Za malaria zachangia asilimia 45 ya vifo
* Watengenezaji wafananishwa na magaidi
Leon Bahati
VIFO vya watu 200,000 hadi 450, 000 kati ya milioni moja kutokana
na malaria katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo, hutokana na matumizi ya
dawa bandia.
Hayo yamo katika utafiti uliofanyika nchini na taarifa
yake kutolewa Mei mwaka huu na jopo la watafiti.
Watafiti hao ni pamoja na Linus Mhando, Mary Jande,
Anthony Liwa, Stanley Mwita na Karol Marwa wa Chuo Kikuu cha Afya cha Kanisa
Katoliki mkoani Mwanza.
Watafiti hao wamebainisha kuwa hali hiyo inatokana na kusambaa
kwa dawa bandia za malaria na magonjwa mengine kwenye maeneo mengi nchini.
“Tunachoshauri ni wananchi kupewa elimu ya kutambua dawa
bandia ikiwa ni pamoja na kuweka mfumo utakaowakatisha tamaa watengenezaji wa
dawa hizo,” inaeleza sehemu ya hitimisho la utafiti huo.
Kwa mujibu wa utafiti huo, kati ya watu milioni moja
wanaokufa kwa malaria 200,000 hadi 450,000 hufa kutokana na dawa bandia.
Aidha, watafiti hao walieleza kuwa kwa mujibu wa utafiti katika
nchi zinazoendelea Tanzania ikiwamo, asilimia 10 hadi 15 ya dawa zinazouzwa humo
ni bandia.
Kwa sababu hiyo, kwenye ripoti yao walipendekeza moja ya
njia za kukabili watengenezaji dawa bandia ni kuwa na sheria zinazoidhinisha
adhabu kali.
Watafiti hao walipendekeza moja ya kanuni hizo iwe ni kuadhibu
kwa mujibu wa sheria ya ugaidi inayoonesha mauaji ya makusudi.
Kuhusu sababu za kupendekeza sheria kali zitumike
kuadhibu wahusika wa dawa bandia, watafiti hao walieleza ni kutokana na wanaotengeneza
dawa hizo kufanya hivyo huku wakijua zitakuwa hazitibu bali kuua.
Ripoti ya watafiti hao inaonesha kwamba utafiti
mbalimbali duniani unabainisha watengenezaji wa dawa bandia kuzitengeneza kwa
wingi na kuingizwa kwenye soko la Afrika.
Sababu kuu waliieleza kuwa ni kutokana na asilimia 90 ya
watu milioni tatu wanaougua malaria duniani kuwa Afrika.
Walitoa mfano wa Uganda, ambako asilimia 37 ya dawa bandia
ya artemisinin, ambayo ni maarufu zaidi nchini humo imekuwa ikiuzwa kwenye
maduka mengi ya rejareja.
“Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoendelea haiwezi
kamwe kujinasua kwenye janga hilo la dawa bandia,” inaeleza sehemu ya ripoti ya
utafiti huo, lakini ikisisitiza kuwa mikakati makini ndiyo itakayozuia dawa
hizo kuingia au kutengenezwa nchini.
Kuhusu tafsiri ya dawa bandia, taarifa hiyo ya utafiti ilieleza
kuwa zipo dawa za aina nyingi lakini zimegawanyika katika makundi matatu.
Walitaja kundi la kwanza kuwa ni la dawa zenye upungufu
wa viambata.
“Kwa mfano; kama dawa ina viambata vitatu, kimoja au
viwili hukosekana, hivyo tiba yake kutokuwa kamilifu,” ilieleza sehemu ya
utafiti.
Aina ya pili, ilielezwa ni dawa zenye viambata vyote,
lakini kuwa kwa kiwango hafifu, hivyo kushindwa kufanya kazi ya tiba kulingana
na viwango vya kitaalamu.
Watafiti hao walilielezea kundi la tatu, kuwa ni dawa iliyotengenezwa
vizuri, lakini ufungaji wake kutokidhi viwango au kufungwa katika makasha
yasiyo sahihi.
Kwa mujibu wa watafiti hao, utafiti uliofanywa na Shirika
la Afya Duniani (WHO) mwaka 1999, ulipendekeza kuwapo mkakakati makini wa
kuwezesha watu kuzitambua dawa bandia.
Hata hivyo, walipofanya uchunguzi nchini kuona kama
wananchi wana ufahamu kuhusu dawa bandia, ilionekana karibu nusu hawajui
viashiria vya dawa bandia.
Utafiti huo unaonesha kuwa kati ya watu 293 waliochunguzwa,
matokeo yalionesha watu 163 sawa na asilimia 55.6 walikuwa na uelewa, lakini
130 sawa na asilimia 44.4 hawakuwa na elimu hiyo.
0 comments:
Post a Comment