Jemah Makamba
MAMIA ya watu waliofurika katika
Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, jana walipigwa na butwaa baada
ya kushuhudia mshtakiwa wa utoboaji macho na uporaji, Salum Njewete maarufu kwa
jina la Scorpion akiachiwa huru.
Tukio hilo lilitokea baada ya upande wa
mashtaka mbele ya hakimu Adelf Sachore wa mahakama hiyo kuamua kuiondoa kesi
hiyo katika hali ambayo sababu zake hazikuweza kufahamika mara moja.
Awali, Mwendesha Mashtaka SP Munde
Kalombora aliomba mahakama kuliondoa shtaka hilo chini ya kifungu cha sheria
91(1) cha kanuni ya adhabu na hakimu Sachore kukubali akitumia kifungu hicho.
Hata hivyo, baada ya hakimu Sachore
kumaliza kuondoa shtaka hilo akieleza haliwezi kuendelea tena kwenye chemba
yake, Scorpion alitoka nje.
Lakini wakati watu waliofurika
kusikiliza kesi hiyo wakiendelea kushangaa, polisi walimkamata tena na
kumpeleka katika mahabusu ya mahakama hiyo.
Scorpion alikaa kwenye mahabusu hiyo kwa
takriban takika tano, kisha alitolewa akiwa kwenye ulinzi mkali akiwa amefungwa
pingu mikononi na kufikishwa tena mahakamani kwa hakimu mwingine na kusomewa upya
mashtaka hayo.
Safari hii, mashtaka hayo yalisomwa
mbele ya Hakimu Flora Haule.
Katika shtaka hilo jipya, mwendesha mashtaka,
Chesensi Gavyole alidai mbele ya hakimu huyo kuwa Septemba 6 mwaka huu, maeneo
ya Buguruni Sheli, Scorpion alifanya kosa la wizi wa kutumia silaha.
Alidai kuwa kabla ya kufanikisha wizi
huo alimjeruhi kwa kumchoma kisu malalamikaji sehemu ya mabega na tumboni, kisha
kumchoma macho yote mawili kwa kutumia kisu na kumuibia cheni ya fedha, kidani
na pesa taslimu, vyote vikiwa na thamani ya Sh. 476,000.
Baada ya usomewa mashtaka hayo,
mshtakiwa huyo alisema halitambui jina la Scorpion akidai si jina lake huku
akikana mashtaka aliyosomewa.
Mwendesha mashtaka alisema upelelezi wa
kesi hiyo haujakamilika na Hakimu Haule alinukuu kifungu cha cha sheria namba
148 (5) (a)(i) kinachozuia watuhumiwa wa makosa kama hayo kupata dhamana na
kuamua kuwa ataendelea kukaa rumande hadi Novemba 2 mwaka huu kesi hiyo
itakapotajwa tena.
NJE YA MAHAKAMA
Watu walioonekana kujaa shauku ya kumjua
mtuhumiwa huyo walijaa nje ya mahakama kusubiri kinachoendelea. Wingi huo wa
watu uliwalazimu Polisi kutumia nguvu ya ziada kuwadhibiti.
Ndugu wa mlalamikaji akiwemo mama mzazi walifika
mahakamani hapo mapema na walionekana wenye huzuni pale walipomuona mshtakiwa huyo
alipofika mahakamani hapo na kushuka kwenye gari la magereza.
Hata hivyo wakati ndugu hao wa mlalakaji
wakionekana kuhudhunika, ndugu wa Scorpioni walisikika wakisema kuwa hawaamini
kama ndugu yao huyo anaweza kufanya unyama kama huo.
Mmoja wa wadogo wa mlalamikaji alimwambia
mwandishi wa habari hii kuwa alifika mahakamani hapo ili kuona mwisho wa kesi
hiyo.
“Lazima nije ni kama namwakilisha ndugu
yangu ambaye sasa hawezi kufanya chochote. Hawezi hata kufuatilia kesi hiyo na
kuona mwisho wake,” alisema ndugu huyo.
0 comments:
Post a Comment