Fidelis Butahe
SAA
chache baada ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuanika nauli za ndege mpya za
Bombardier Dash 8 Q400 zilizonunuliwa hivi karibuni na Serikali, viongozi wa
vyama vya NCCR-Mageuzi na CUF wamesema haziendani na kauli ya Rais John
Magufuli aliyeahidi kuwa nauli itakuwa chini.
Wamesema
nauli hizo zinaonesha wazi kuwa Serikali inalenga zaidi kufanya biashara kuliko
huduma stahiki na kudai kuwa zinatofautiana kwa kiasi kikubwa na nauli za ndege
za mashirika mengine.
Wakati
Mwenyekiti wa NCCR, James Mbatia akiitaka Serikali kupitia upya nauli hizo kwa
madai kuwa ndege hizo zimenunuliwa kwa kodi za wananchi, Mwenyekiti wa Kamati
ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alisema lazima nauli hizo ziendane na ubora
wa huduma.
Kwa
mujibu wa taarifa katika tovuti ya Shirika hilo, nauli hizo zimegawanywa katika makundi mawili
ya daraja la kwanza na la pili, huku nauli ya juu kwa daraja la kwanza ikiwa ni
Sh 590,000 kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma, na iwapo abiria atakata tiketi
ya kwenda na kurudi atalazimika kulipa Sh 910,000.
Katika
daraja la pili, usafiri wa juu wa ndege hizo pia ni kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma ambao ni Sh
395,000 na kufuatiwa na Dar es Salaam kwenda Tabora, Sh 385,000.
Katika
mpangilio wa safari 14 za ndege hizo katika mikoa nchini, nauli ya chini kabisa
ni kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar ni Sh 85,000
huku kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Arusha, Mtwara, Dodoma, Tabora, Mbeya, Kilimanjaro
na Bukoba mkoani Kagera, nauli ni kati ya Sh180,000 na Sh 520,000 kwa madaraja
yote, mbali na kukata tiketi ya kwenda
na kurudi.
Kwa
mujibu wa maelezo ya watoa huduma wa Shirika hilo, nauli hizo zitatumika kwa
siku 14, kuanzia kesho hadi Oktoba 28 na baada ya hapo zitaongezwa kulingana na
eneo husika ambalo ndege hizo zitakwenda.
Septemba
28 wakati akizindua ndege hizo, Rais Magufuli alisema nauli hazitakuwa kubwa na
kila Mtanzania ‘ataonja’ ndege, kubainisha kuwa zinatumia mafuta kidogo na zinatua
katika viwanja vya mazingira yote nchini.
“Nauli
za ndege hizi ziko juu kuliko za Fastjet. Watanzania wanahitaji usafiri wa
uhakika na kama Serikali ikiweza kulisimamia hilo huenda watu wakasahau
machungu ya nauli za juu…ila nikiri wazi nauli hizi ni kubwa kwa kweli, inasikitisha
sababu zitaongezeka badala ya kupungua,” alisema Mtatiro.
Mbatia
alisema: “Wanapaswa kutazama mashirika mengine duniani yanafanyaje. Hii ni
biashara ya ushindani. Ninachokiona ni Serikali kujikita katika biashara bila
kuangalia hali halisi.
“Kabla
ya kuja na nauli hizi lazima ujiulize, je huduma zimezoeleka na watu? Na je,
wataweza kutoa ushindani kwa wengine?”
Alisema
kiwango hicho cha nauli kinaonesha kuwa ATCL imeanza kwa kushindwa na imeshindwa
kuanza kazi kwa kuzingatia misingi ya uzalishaji na ufanisi.
“Wangeweza
kufanya ushindani kwa kuanzisha safari za ndege katika nchi kama za Kongo,
Zimbabwe na Nigeria, ambako watu hulazimika kuunganisha ndege kuliko kuanza
kupambana hapa nyumbani,” alisema.
Alibainisha
kuwa tatizo analoliona ni siasa kuingizwa katika biashara na kushauri wanasiasa
kuacha watalaamu wa masuala ya anga kufanya kazi yao.
0 comments:
Post a Comment