Abraham Ntambara
Viongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania |
JUKWAA la
Wahariri Tanzania (TEF)
limemwomba Rais John Magufuli kumshughulikia Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba kwa maelezo kuwa ni ‘jipu’
ambalo limevuruga mjadala wa Muswada wa Huduma za Habari.
Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam wakati wahariri wa
vyombo vya habari walipokuwa wakijadili vipengele vya Muswada huo ambavyo
vinatakiwa kufanyiwa mabadiliko kabla ya kupitishwa kuwa sheria kwa kuwa si
rafiki kwa tasnia ya habari nchini.
Mhariri Mtendaji Mkuu
wa Kampuni ya New Habari Limited,
Absalom Kibanda alisema Serukamba
ni ‘jipu’ na kumwomba Rais aamini hivyo, akibainisha kwamba kipindi cha
aliyekuwa Waziri wa Habari, Fenella Mukangara walipeleka hati ya dharura kutaka
Muswada huo ujadiliwe vizuri, lakini alikataa huku akiunga mkono kama ulivyo.
“Kuna sauti ilisikika ikitembea katika mitandao,
nikajiuliza ameongea kama Waziri, Ofisa Habari wa Serikali au mtu binafsi?” Alihoji
Kibanda.
Kibanda alimwomba Rais aangalie ni nani wasemao ukweli
kati ya wadau wa habari (wahariri na waandishiwa habari) na mamlaka nyingine za
Serikali kuhusu namna nzuri ambayo Muswada huo unaweza kujadiliwa na kuwa sheria
kwa maslahi ya Taifa bila kukwaza upande.
Aidha, alibainisha kuwa kuna watendaji wa Serikali ambao wamekuwa
wakimsukuma Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, ili aridhie
mahitaji yao kwa maslahi binafsi.
Alisema kwa sasa waandishi wa habari wanafananishwa na
wahalifu na kusema hivi karibuni walichapisha habari kwenye gazeti lao na
walikuja kuomba radhi baada ya kupokea vitisho.
Aliongeza kuwa Muswada huo ulitakiwa uwekwe vipengele
vinavyowachukulia hatua watu wanaoingilia kazi za vyombo vya habari, kwa kuwa
makosa mengi vinayotupiwa vyombo vya habari vyanzo huwa ni wanasiasa.
Mjumbe wa TEF, Jesse Kwayu alisema wana wasiwasi na
msimamo wa Serukamba, kwa kuwa anashindwa kutimiza majukumu yake ya kuisimamia
Serikali na badala yake anakuwa kama ni ofisa wa Serikali.
“Wakati akiusoma Muswada huu kwenye Kamati, akihitimisha
alisema hakuna uhuru usio na mipaka,” alisema Kwayu.
Alibainisha kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo aliyepita,
alisikiliza vizuri mapendekezo ya wadau wa habari na kuyafikisha bungeni yajadiliwe
tofauti na wa sasa ambaye si msikivu.
Alisema wakati wakiujadili hivi karibuni Dodoma ilifika
mahali kukawa na mvutano mkali kati ya Serukamba na Zitto Kabwe kwa kuwa
alikuwa hajaridhishwa na namna Muswada huo ulivyojadiliwa, kwa sababu wadau wa habari
wahusika hawajahusishwa kikamilifu.
Alisema asilimia 80 ya waandishi wa habari wako mikoani
ambako waandishi hao pia hawajajadili na kupata mwafaka wa Muswada huo.
Naibu Mhariri Mtendaji wa Jamhuri, Manyerere Jackton aliwataka
Serukamba na Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO, Hassan Abbas wasijisahau na kupitisha Muswada
huo eti kwa kuwa wako serikalini, bali wajue kuwa kuna wakati watarudi na
kukabiliwa na sheria hiyo.
Mwenyekiti wa TEF,
Theophil Makunga alisema Muswada huo usipobadilishwa vipengele hivyo na
ukapitishwa kuwa sheria, waandishi wa habari watakuwa kwenye shida kubwa kwa
kuwa watakuwa wakipambana na kitu kibaya sana.
0 comments:
Post a Comment