Suleiman Msuya
Makamu wa Rais, Samia Suluhu |
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amepiga marufuku
uharibifu wa mazingira unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini, akisema
unaweza kusababisha nchi kugeuka jangwa.
Samia alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na waandishi
wa habari baada ya kufungua mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi
unaokutanisha wanasayansi, watafiti na wadau wa mazingira chini ya usimamizi wa
Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Alisema jukumu la kuhifadhi mazingira si la Serikali peke
yake bali ni kila mwananchi na wadau wa mazingira kwa ujumla, hivyo wananchi ni
muhimu kwa umoja wao wakaongeza jitihada za kupanda miti katika maeneo yao ili
kukabiliana na hali uharibifu wa mazingira.
“Uharibifu wa
mazingira usimame leo na marekebisho ya uharibifu tulioufanya uanze leo na hili
ni jukumu la kila Mtanzania,” alisema.
Aidha, Makamu wa Rais alitoa mwito maalumu kwa viongozi
wa ngazi zote nchini kuchukua hatua za kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji
katika maeneo yao ili visitoweke.
Alisema mabadiliko ya tabianchi yameanza kuleta athari duniani,
hivyo jitihada za makusudi zinahitajika ili kuhakikisha changamoto
zinazojitokeza sasa zinakabiliwa ipasavyo.
Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Mabadiliko ya
Tabianchi wa UDSM, Profesa Pius Yanda alisema mkutano huo wa siku tano utakuwa
na jukumu la kujadili kwa kina, namna bora ya kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabianchi.
0 comments:
Post a Comment