Grace Gurisha
Josephat Gwajima |
MPELELEZI wa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Sajini Abogasti ameieleza Mahakama kuwa wasaidizi
wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima walimpelekea
bastola saa nane usiku akiwa hospitali ya TMJ alikolazwa baada ya kuanguka Polisi
akihojiwa.
Sajini Abogasti alieleza hayo jana mbele
ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Cyprian Mkeha wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, Dar es Salaam wakati akitoa ushahidi dhidi ya Gwajima na wenzake
wanaokabiliwa na tuhuma za kushindwa kuhifadhi silaha sehemu salama.
Shahidi huyo alitaja wasaidizi hao kuwa
ni Yekonia Bihagaze, George Mzava na Geofrey Milulu, ambao wanadaiwa kutenda
kosa hilo kinyume cha sheria kwa sababu kwa hali ya kawaida mgonjwa hapalekewi
silaha.
Alidai wasaidizi hao walikutwa na begi
ambalo ndani lilikuwa na silaha na vitu vingine, baada ya askari kulifungua wakihisi
kuwapo jambo linaloendelea.
Alidai kuwa Mkuu wa Upelelezi Kinondoni
alimuunganisha na Mkuu wa Kituo cha Kawe, Pamphil ambaye alimkabidhi begi lenye
bastola namba CAT 5802, risasi tatu kwenye magazine, CD mbili, risasi 17 za SMG,
kitabu cha umiliki silaha, nguo ya ndani na hati ya kusafiria ya Mchungaji
huyo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Shedrack Kimaro, alimtaka shahidi wa upande wa mashitaka kuionesha Mahakama
kitabu cha umiliki wa silaha ambapo shahidi huyo alikitafuta zaidi ya dakika mbili
bila mafanikio.
Hata hivyo, alidai kitabu cha umiliki wa
silaha na cha hundi alimshampa Gwajima.
Alidai kuwa baada ya kukabidhiwa begi
hilo kwenye kituo cha Polisi Oysterbay alianza upelelezi na kubaini kuwa Machi
25 mwaka jana, Gwajima alikwenda Arusha kwenye mkutano wa maaskofu na washitakiwa
wenzake.
“Machi 26 mwaka jana, Gwajima aliambiwa
anaihitajika Polisi Dar es Salaam, Machi 27 alifika na kuacha silaha yake mikononi
mwa Bihagaze, Mzava na Milulu ambao walikaa nayo kwa siku mbili kitu ambacho ni
kinyume cha utaratibu,” alidai shahidi huyo.
Alidai pia kwamba Gwajima aliitwa polisi
kwa tuhuma za kumdhihaki Askofu Mkuu wa Jimbvo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama
Polycarp Kadinali Pengo.
Sajini Abogasti alidai mahojiano ya polisi
na Gwajima yaliisha baada ya Gwajima kupata maradhi ya ghafla ambapo
aliondolewa kituoni hapo na kupelekwa kwa mara ya kwanza hospitali ya Temeke,
kisha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mwishowe TMJ kutokana na hali yake
ilivyokuwa.
Hata hivyo, Wakili Peter Kibatala alimhoji,
shahidi huyo kuwa Gwajima alipofika kituo kikuu cha Polisi, upelelezi wake
ulibaini kuwa maungoni alikuwa na silaha.
Akijibu hoja hiyo, Sajini Abogasti
aligundua kuwa Gwajima alishaitekeleza na kuwa yeye si aliyemfundisha Gwajima
taratibu za kumiliki silaha. Kesi iliahirishwa hadi Novemba 24.
0 comments:
Post a Comment