UCHAMBUZI HURU
Mashaka Mgeta
Mashaka Mgeta |
DUNIANI hakuna nchi inayoweza kufanya
chaguzi zake pasipo malumbano miongoni mwa wagombea, wanachama ama wafuasi wa
vyama vinavyoshiriki. Hali hiyo inatokea katika nchi za Afrika, Asia, Pacific,
Ulaya na kwingineko duniani.
Kuna tofauti ya namna malumbano
yanavyotokea, vyanzo na mfumo thabiti ya utatuzi wake.
Kwa sehemu kubwa, nchi kadhaa hususani
zilizoendelea na chache kati ya zinazoendelea, zimefanikiwa kuendesha chaguzi
zao kwa kufuata mfumo chanya, ambao malumbano na mbinu zinazotumika kupata
ushindi, haviathiri umoja wa taifa husika.
Kwa bahati mbaya, nchi nyingi za Afrika iliyowahi
kuitwa ‘bara la giza’, na pengine kutokana na matendo ya baadhi ya watawala
wake, inaweza kustahili kuitwa hivyo hali inazidi kuwa mbaya.
Malumbano na mbinu zinazohusiana na
uchaguzi vimekuwa sababu ya machafuko, kutoweka kwa umoja wa kitaifa na wakati
mwingine vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mifumo ya chaguzi nyingi katika Afrika
ni mizuri kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo ushirikishi mpana wa wananchi
kuwachagua viongozi katika ngazi za tawala za mikoa na serikali za mitaa.
Lakini utekelezaji hasi wa sheria za
uchaguzi ili kulinda maslahi ya kisiasa hasa kwa watawala, matumizi ya nguvu kubwa
katika kuutafuta na ‘kuumiliki’ ushindi na rushwa, vinachangia kuzivuruga jamii
za Afrika, hivyo kuzidisha wigo wa mafarakano.
Jamii zinazofarakana haziwezi kushiriki
katika ubunifu bora wa miradi, mikakati na mipango ya kuwaondoa watu katika
umasikini.
Kwa mafarakano yanayotokana na chaguzi
barani Afrika, jamii zinaendelea kuishi kimasikini, kuendeleza ujinga na
kushindwa kuyadhibiti maradhi kwa kadri ilivyokuwa kusudio la kumuondoa
mkoloni.
Tawala nyingi za Afrika zinashutumiwa
kwa kukiuka sheria na kanuni za uchaguzi, kisha kutumia dola kuwadhibiti
wanaotafuta haki na usawa kwa maslahi ya umma mpana.
Kwa namna hiyo, miongoni mwa malengo ya
kuwaondoa wakoloni na kuifanya Afrika kuwa huru, hayajafikiwa na huenda
yakachukua muda mrefu kufikiwa kutokana na ukiukwaji wa sheria na kanuni za
chaguzi.
Chaguzi zinapohujumiwa, michakato yake
‘ikachakachuliwa’ ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutafuta na kumiliki utawala,
mataifa yakabaki katika mafarakano ya ndani, wanavurugana wenyewe kwa wenyewe.
Wanaoratibu mbinu zinazoathiri mchakato
wa chaguzi, wamekuwa wakitumia ‘nyenzo’ kama vyombo vya dola, mamlaka za
kusimamia uchaguzi husika na rushwa hasa ya vyeo, ili kufanikisha nia ya kupata
ushindi.
Matukio hayo yanatumika kwa kizazi
kilichopo na kinachokuja. Tangu kuondoka kwa waasisi wa uhuru wa mataifa
mbalimbali Afrika, waliowafuata, kidogokidogo, wakaanza kushiriki njama na
mbinu chafu zinazowatenganisha na kuwafarakanisha raia wao.
Wenye mamlaka wanawateuwa wasaidizi wao
wakiwamo wa mamlaka za kusimamia uchaguzi ama taasisi kama mahakama za Katiba,
ili kuhalalisha `uovu’ unaowaweka madarakani.
Jambo lililo dhahiri ni kwamba mbinu
hizo zinafanikiwa katika maeneo mengi ya Afrika.
Watawala wanaendelea kubaki madarakani,
wakimiliki dola na tawala za mikoa na serikali za mitaa ambazo baada ya
ugatuzi, mataifa mengine yameibua Kaunti kama sehemu ya maeneo ya utawala.
Lakini hatua hiyo inakuwa yenye kulinda
maslahi binafsi na yanayohusu chama cha siasa. Kamwe hatua hizo hazigusi
maslahi ya umma.
Ndio maana kwa watawala wa aina hiyo
barani Afrika, hawajali umma unataka nini, umeamua nini na unaelekea wapi.
Inawezekana wananchi wakafanya uamuzi wa
kuwachagua viongozi katika ngazi tofauti, wakiwaamini kwamba ‘wanatosha’
kuwaongoza au kuwawakilisha.
Licha ya ukweli huo, kikundi cha watu
hasa walio na nguvu na mamlaka za utawala, kinaweza kuchukua hatua za udhibiti
wa matakwa ya umma, kikageuza nia za raia walio wengi na kuzielekeza mahali
panapowafaa.
Hali hiyo haiwezi kuleta umoja, haiwezi
kuyafanya mataifa yakapata utulivu wa kisiasa, raia wake wakajikita katika
kuwatambua na kuwashughulikia maadui wakiwamo wa kijamii.
Ndio maana mwenendo wa uchumi, maendeleo
na ustawi wa mataifa mengi ya Afrika vimebaki vilipo, ama vimedidimia katika
vipindi vya kutoka mwaka mmoja hadi mwingine.
Mataifa husika yameshindwa kutoka kwenye
orodha ya nchi masikini, licha ya miongoni mwao kuwa na rasilimali nyingi za
kuwezesha kukuza uwekezaji, uzalishaji wa bidhaa na huduma zinazohitajika kwa
mataifa ya nje.
Wanasiasa hasa watawala wengi katika Afrika
wanajali kuwapo kwao madarakani, hawaitazami jamii inayopaswa kujengwa katika
misingi ya umoja utakaoyaweka kando maslahi ya kisiasa, kwamba kila raia
anakuwa huru kuitumia ipasavyo haki ya kuchagua na kuchaguliwa.
Ikiwa mifumo, fikra na utashi wa wanasiasa
katika Afrika utajikita huko, ni dhahiri kwamba kizazi kitarithishwa ushindani
wenye tija, kwa kila anayechaguliwa kupimwa kwa misingi ya sera za kitaifa na
ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Haiwezekani kwa taifa linaloendeleza
mafarakano, kutanua wigo kati ya watawala na watawaliwa, likafikiria kwamba ipo
siku litavuka hatua kuyaelekea maendeleo endelevu na ustawi bora wa watu wake.
Matumizi ya hoja zinazojenga chuki
yanaendeleza chuki, ubaguzi unarithisha ubaguzi, mabavu yanazalisha wababe,
hila ovu zinaeneza uovu na mengine mengi kama hayo.
Afrika inapaswa kutoka huko. Mataifa na
tawala zao wasipokuwa na utashi thabiti katika kujenga umoja wa kitaifa,
wakashindwa kuondokana na maslahi ya binafsi na yale ya kisiasa, jamii zake
zikiwamo kizazi cha wanaosababisha kadhia hizo, hakitabaki salama kisiasa,
kiuchumi na kijamii. Afrika itatafunwa kwa matendo hayo.
Mungu ibariki Afrika.
0754691540
0 comments:
Post a Comment