Waandishi Wetu
UCHAGUZI wa
mameya katika manispaa za Kinondoni na Ubungo jana ulizua mvutano kati ya CCM
na vyama vinavyounda Ukawa kuhusu uhalali wa baadhi ya wajumbe kupiga kura,
huku Benjamin Sitta aliyechaguliwa na madiwani wa CCM pekee, akitangazwa kuwa Meya
mpya wa Manispaa ya Kinondoni.
Katika mvutano
huo, madiwani wa Ukawa Kinondoni walisusia uchaguzi huo huku ule wa manispaa ya
Ubungo ukiahirishwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa madiwani wa Chadema
ambao ndio wengi kuliko wa CCM, kupinga baadhi ya madiwani wao wa Ubungo
kutakiwa kupiga kura Kinondoni, huku wale wa Kinondoni kuhamishiwa Ubungo.
Uchaguzi huo
ulipangwa baada ya kuvunjwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ambayo
iligawanywa katika maeneo mawili ya kiutawala na kuzaa wilaya na manispaa
mbili; Kinondoni na Kibamba.
Mvutano katika
chaguzi hizo ulianza kuonekana tangu juzi baada ya vyama vinavyounda Ukawa;
Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi kudai kuna ‘mkakati’ wa kuongezwa kwa wajumbe
ili CCM iibuke na ushindi.
Wakati Ukawa
ikipinga wabunge wake wa viti maalum, Susan Lyimo (Chadema) na Salma Mwasa
(CUF) kutakiwa kushiriki uchaguzi wa meya wa Ubungo badala ya Kinondoni,
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli alisema
wabunge hao wote wanaishi Ubungo, hivyo walipaswa kushiriki uchaguzi huo.
Ukawa pia
walipinga kitendo cha Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Spika,
Dk Tulia Ackson, Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga na Waziri wa
Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuongezwa kuwa wajumbe
halali wa uchaguzi wa meya wa Kinondoni, kwa maelezo kuwa ni kinyume na sheria za
Serikali za Mitaa.
Sakata hilo
lilisababisha Chadema kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza
kusudio la kwenda mahakamani kupinga chaguzi hizo wakibainisha kuwa hali hiyo
imeamsha upya mkakati wao wa operesheni Ukuta.
Wakati Ukawa
wakijipanga kwenda mahakamani, Kagulumjuli aliwatangazia vita, akieleza kuwa
iwapo madiwani wa Ukawa watashindwa kuhudhuria vikao vitatu mfululizo vya
Baraza la Madiwani, watakuwa wamejiondoa kwenye nafasi hizo na kwa mamlaka
aliyonayo ataitisha uchaguzi mwingine kwenye kata zao.
Hali ilivyokuwa Kinondoni
Uchaguzi huo
ulipangwa kuanza saa 2:30 asubuhi lakini mbali na Ukawa kuususia, waandishi wa habari
nao walibaguliwa kwa kuruhusiwa wachache kutoka vyombo vya habari vya Serikali,
chama tawala, Clouds televisheni na Star televisheni.
Kuhusu madiwani
na wabunge wa viti maalum wa Ukawa kuondolewa katika uchaguzi kwa madai kuwa si
wajumbe halali wa kikao, huku wale wa CCM wasio halali wakiruhusiwa kushiriki alisema
ni uhuni uliopitiliza.
“Wamemkata Lyimo
na Mwasa. Sheria inasema wajumbe halali wa vikao vya halmashauri ni wabunge wa
viti maalum ambao mchakato wao umeanzia katika halmashauri na hao waliowakata
michakato yao imeanzia Kawe na Kinondoni. Ni wajumbe halali na ndio maana
waliingia katika vikao vilivyopita,” alisema.
Alidai kuwa
madiwani wa viti maalumu wa Ukawa pia wamekatwa kushiriki uchaguzi, kufafanua
kwamba idadi ya madiwani hao katika halmashauri husika hutokana na idadi ya
kata ambayo chama kimeshinda katika halmashauri hizo.
Alibainisha kuwa
kutokana na idadi ya kata ambazo Ukawa wameshinda katikamajimbo ya Kawe na
Kinondoni, walipaswa kuwa na madiwani saba wa viti maalum.
“Baada ya
kupatikana kwa halmashauri mbili mkurugenzi wa kinondoni amechukua hatua ya
kukata madiwani wawili wa viti maalum wakati Tume ya Taifa ya Uhaguzi (NEC)
ndio ina mamlaka ya madiwani na wabunge,” alisema.
Kuhusu wateule
wa Rais walioshiriki uchaguzi huo alisema, “Ili aweze kuingia katika
halmashauri husika lazima awe mkazi wa halmashauri hiyo. Yupo Dk Tulia,
Ndalichako ambaye ni mpya na alishiriki uchaguzi wa meya wa Ilala ila leo kaletwa
Kinondoni.”
Alisisitiza,
“wateule wa rais hawawezi kuingia zaidi ya watatu katika halmashauri moja, ila
ndani kwenye uchaguzi (wa jana) wapowanne. Huu ni uhuni na kama amewatuma (Rais
John Magufuli) sawa, ila tutaenda kupambana mahakamani ili tupate tafsiri ya
sheria.”
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema, aliponda uchaguzi huo na
kubainisha kuwa ni mwendelezo wa Serikali ya Awamu ya Tano kuminya demokrasia.
“Serikali hii
haizingatii demokrasia wala kufuata sheria na katiba na polisi wamekuwa
mawakala wa CCM…, huyu meya wao ‘magumashi’ (Sitta) watakayefikiria wamempata
nina imani hana baraka za wananchi na Mungu na sisi hatuna sababu za kumpa baraka.”
Mbowe ambaye pia
ni mbunge wa Hai aliponda kitendo cha kuzuiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari kuripoti
uchaguzi huo, kuruhusiwa vile vya Serikali na CCM, kukifananisha kitendo hicho
na uhuni uliopitiliza. “Ndani (katika ukumbi) kuna askari wengi wenye sare na
wasio na sare.
Rais Magufuli
kwa utaratibu huu wa kuua demokrasia aliouanzisha katika utawala wake
ataliletea Taifa hili maafa makubwa,” alisema Mbowe.
Katibu Mkuu wa
Chadema, Vicent Mashinji, alisema kitendo kilichotokea katika chaguzi hizo
kitaamsha upya mkakati wa operesheni Ukuta ambayo Septemba 30 mwaka huu,
kilitangaza itafanywa kimya kimya.
Operesheni hiyo
ambayo awali ilipangwa kuandamana na mikutano ya hadhara na maandamano nchi
nzima inalenga kila kinachoelezwa kuwa ni kupinga maamuzi yanayofanywa na
Serikali bila kuzingatia sheria na Katiba ya nchi, likiwemo la kuzuia mikutano
ya hadhara.
Mashinji
alilalamikia kitendo cha madiwani kupewa barua za kushiriki uchaguzi huo juzi
saa mbili usiku na kubainisha kuwa watakwenda mahakamani kupinga uvunjwaji wa
sheria na kanuni zinazoweka haki ya madiwani kuchagua viongozi wao katika Halmashauri
husika.
Meya wa CCM alichaguliwaje?
Sitta aliibuka
mshindi kwa kupata kura 18, huku Naibu Meya akichaguliwa George Manyama naye
akishinda kwa idadi hiyo hiyo ya kura. Awali, Ukawa ilikuwa na wajumbe 17 na
CCM wakiwa 16 lakini baada ya chama hicho tawala kuongeza wajumbe kwa hoja
zilizotolewa na Kagurumjuli, CCM kilikuwa na wajumbe 18 huku Ukawa wakibaki 17.
Katika maelezo
yake ndani ya uchaguzi huo ambayo JAMBO LEO imeyanasa, Kagulumjuli alisema
taarifa za uchaguzi huo zilitolewa mapema na madiwani wote walipewa taarifa.
“Wajumbe wote
walipata barua ya wito na kuzipokea kupitia “dispatch” lakini baadhi yao,
wamefika na kugoma kuingia ndani. “Kukaa kwao nje hakutuzuii kuendelea na
uchaguzi kwa sababu taratibu zote zimefuatwa,” Mkurugenzi huyo alieleza.
Awajibu Ukawa
Akijibu suala la
Lyimo na Mwasa, alisema Lyimo si mkazi wa Kinondoni anaishi eneo la Chuo Kikuu
lililopo Ubungo, hivyo anapaswa kushiriki kwenye vikao vya baraza la madiwani
kwenye wilaya hiyo mpya.
Kuhusu Mwasa
alisema ni mkazi wa Kimara na kwa sababu hiyo alipaswa kushiriki vikao hivyo
kupitia manispaa ya Ubungo.
Katika maelezo
yake Kagurumjuli, alisema wajumbe ambao ni wateule wa rais wabunge hao
wanachaguliwa na rais kwa majukumu maalum na hawana mchakato kwani mchakato wao
unafanywa na rais mwenyewe.
Mkurugenzi huyo
aliagiza kusomwa barua iliyoandikwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilala,
ikifafanua kuhusu makazi ya Profesa Ndalichako kuwa ni mkazi wa Kinodnoni
ambaye kabla ya uchaguzi huo alikula kiapo cha kuwa diwani wa manispaa hiyo.
Hali Ubungo ilikuaje?
Katika manispaa
ya Ubungo, mgombea umeya wa manispaa hiyo, Boniface Jacob aliwaongoza wenzake
kugomea uchaguzi ulioitishwa na Mkurugenzi wa Wilaya hiyo, John Kayombo.
Katika maelezo
yake, Jacob alisema taarifa za mkutano wa uchaguzi wa meya walipewa juzi saa
sita usiku, huku kukiwa na sintofahamu ya idadi ya wajumbe.
Aliwataja
madiwani waliotolewa Ubungo kupelekwa Kinondoni na kutolewa Kinondoni kupelekwa
Ubungo ili kuiongezea CCM kura kuwa ni Lyimo, diwani wa Mabwepande (CUF), Leyla
Madibi.
Wengine ni
diwani wa Saranga (CCM) Florence Masunga aliyetolewa Ubungo kupelekwa Kinondoni
pamoja na Dk Tulia ambaye ni mkazi wa Kibamba, lakini kapiga kura Kinondoni.
Naye mbunge wa
Kibamba, John Mnyika alisema kilichotokea ni maelekezo ya Rais John Magufuli
kuhakikisha CCM kinashinda Kinondoni.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Husein
Ndubikile, Suleiman Msuya na Abraham Ntambara
0 comments:
Post a Comment