* Wengi wadai kuwa na Shahada, bila kutaja fani
* Baadhi nao wabania viwango vyao vya kitaaluma
Mwandishi Wetu
UHAKIKI wa vyeti kwa watumishi wa umma, huenda ukaibua ‘madudu’
kuhusu aina ya viongozi waliochaguliwa na wananchi, ukifika kwa wabunge, baada
ya watafiti wa wasifu wa wabunge hao, kubaini kuwa wengi hawapendi kueleza
taaluma walizosomea.
Mbali na idadi kubwa ya wabunge hao kukataa kutaja
taaluma na fani walizosomea zaidi ya kudai kuwa wana Shahada ya chuo kikuu,
utafiti huo umebaini pia baadhi yao kukosa wasifu kabisa wa kitaaluma zaidi ya
jina, chama na aina ya ubunge.
Utafiti uliopewa jina la ‘Watawala Wetu’, uliofanyika
mwaka huu wakati Serikali ikifanya uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma,
umebaini taswira hiyo ya kukataa kutaja taaluma kwa wabunge 66, wakati watafiti
hao wakitafuta taarifa za mambo matatu; ikiwamo kama wabunge wanaakisi taswira
ya jamii ya Watanzania.
Mambo mengine ambayo watafiti hao kutoka Taasisi ya
Sayansi ya Jamii; Bituro Kazeri na Emmanuel Ndomondo walilenga kupata taarifa
zake; ni kama wabunge hao wanakidhi matarajio ya Watanzania katika zama hizi na
mwisho ni kama wana uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Madudu yaliyoibuka
“Ukusanyaji wa taarifa ulikutana na changamoto ya kukosekana
taarifa za kutosha. Kwa mfano wabunge wengi walionesha kuwa wana elimu ya
kiwango cha Shahada bila kutaja ni shahada ya taaluma ipi. Hii ilileta
changamoto ya kupanga ni ujuzi au stadi zipi walizonazo.
“Changamoto nyingine ni kutokuwepo kwa taarifa kabisa
kwenye wasifu wa wabunge zaidi ya jina, chama na aina ya ubunge,” imeelezwa
katika utafiti huo ambao pia umeonesha namna Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, linavyokabiliwa na nakisi ya wanataaluma mbalimbali.
Watafiti hao wameeleza kwamba, hapana shaka katika
mabadiliko hayo jamii imepanua vigezo vya wasifu wa wenzao wanaowachagua kuwa wabunge.
“Kwa mfano inawezekana kwa zama zilizopo kusoma na
kuandika katika Kiswahili na Kiingereza si sifa inayotosha kumpa mtu ubunge
pale anapokuwa anashindana na mwingine mwenye sifa zaidi ya hizo,” walieleza
wakijaribu kuoanisha sifa ambazo jamii itahitaji kutumia kama kigezo na
zilizopo katika Katiba.
Wenye shahada/diploma
Kati ya wabunge 389 waliofanyiwa utafiti kuhusu wasifu
wao, taarifa zinaonesha kuwa 105 wamedai kuwa na Shahada ya kwanza ya chuo
kikuu.
Kati yao, CCM ina wabunge 61 waliodai kuwa na Shahada
kati ya wabunge wake 275; Chadema
wabunge 32 kati ya wabunge wake 69 na CUF ina 11 tu waliodai kuwa na elimu hiyo
kati ya wabunge wake 42.
Wenye diploma ilidaiwa ni wabunge 51 na kati yao 34 ni wa
CCM; tisa Chadema na CUF wanane.
Uzamili/uzamivu
Wabunge 136 kati ya 389 walidai kuwa na elimu ya Shahada
ya Uzamili au Uzamivu ambapo kati yao, CCM ina 110; Chadema 17; CUF saba; NCCR-Mageuzi
na ACT-Wazalendo kila kimoja mbunge mmoja.
Msingi, sekondari, siri
Aidha, wabunge 18 walikiri kuwa wao elimu yao ni ya
msingi na kati yao CCM ni 16, Chadema mmoja na CUF mmoja.
Waliodai kuwa na elimu ya sekondari ni wabunge 73, kati
yao 49 wanatoka CCM; Chadema ni 10 na CUF wako 14.
Wabunge sita; watano kutoka CCM na mmoja CUF hawakutaka
kabisa kutaja elimu yao wakisema ni siri yao.
Nakisi ya taaluma
Kati ya wabunge 66 waliokataa kueleza taaluma au uzoefu
wao, utafiti huo umeonesha kuwa 33 ni waliosema awali kuwa na Shahada ya Kwanza.
Wako pia wabunge wanane waliodai kuwa na Shahada ya Uzamili au Uzamivu, na
walipotakiwa kuanisha taaluma walikataa.
Mbali na waliokataa kusema taaluma japokuwa wanadai kuwa na
Shahada ya Kwanza, Uzamili na Uzamivu, utafiti huo pia ulibaini Bunge
kukabiliwa na nakisi ya wanataaluma wengi.
Taaluma zilizosomewa na mbunge mmoja mmoja ndani ya Bunge
zima ni Jiolojia, urubani, usanifu majengo, uanadiplomasia, usanifu, mipango wa
uchumi, polisi, usafirishaji, utafiti na utalii.
Fani 10 zenye wabunge wengi ni ualimu (48); uhasibu na
fedha (35); ujasiriamali (33); sheria (26); utawala na biashara (17); uhandisi
(14); utawala (13); uhadhiri (12); habari na mawasiliano (11) na siasa na uchumi
kila moja wabunge tisa.
0 comments:
Post a Comment