Mariam Cyprian, Tanga
Balozi wa EU, Roealand Van der Greer |
MABALOZI wa Jumuia ya Ulaya (EU) wamevutiwa
kuwekeza viwanda mkoani hapa na kuboresha bandari ya Tanga ili kukuza uchumi
wake.
Akizungumza jana, Balozi wa EU, Roealand
Van der Greer alieleza azma hiyo alipoongoza ujumbe wa mabalozi wa nchi hizo kufanya
ziara ya siku moja ya kukagua bandari hiyo.
"Tumewasili hapa kuangalia
uwezekano wa kukuza sekta ya viwanda, tunaamini ukiwapo uwekezaji mkubwa wa viwanda,
uchumi wa nchi utakua lakini pia kuna umuhimu wa kuboresha bandari ya Tanga na
sisi tuko tayari kushirikiana nanyi ili kukamilisha azma hii," alisema
Rowland.
Mkuu wa Mkoa Tanga, Martine Shigela
alisema Serikali imejipanga kukaribisha uwekezaji mkubwa ili kuhakikisha mkoa
unapiga hatua kimaendeleo, ikiwamo kuimarisha ulinzi na usalama ili mkoa
uendelee kuwa na amani.
"Tuko tayari kupokea wawekezaji na
maeneo yapo ya kutosha, kwani mkoa wetu ni sehemu nzuri ya uwekezaji kutokana
na hali ya amani na utulivu iliyopo, Serikali inajitahidi kuimarisha ulinzi na
usalama, ili kuwahakikishia usalama wananchi na wawekezaji," alisema
Shigela.
Shigela aliwaeleza mabalozi hao kuhusu
mradi mkubwa wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda unaotarajiwa kuanza
mwakani, huku pia kukiwa na uwekezaji wa viwanda vikubwa vikiwamo vya saruji.
Mabalozi hao walitembelea pia ghala la
kupokea mafuta la GBP na sehemu litakakoishia bomba la mafuta.
Akisoma taarifa kwa mabalozi hao, Kaimu
Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Andrew Arika alisema
changamoto inayoikabili ni kina kifupi jambo linalosababisha meli kubwa kutia
nanga mbali.
Hata hivyo, alisema ipo mikakati ya
kujenga bandari mpya ya Ndumi ambayo ina kina kirefu.
Mabalozi waliokuwa kwenye ujumbe huo ni kutoka
Ufaransa, Italia, Uingereza, Hispania, Ujerumani na Finland wakati Ireland na
Sweden zikituma wawakilishi.
0 comments:
Post a Comment