Hussein Ndubikile
MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Rais mstaafu
Jakaya Kiwete, ameahidi kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wanafunzi chuoni hapo likiwamo
suala la mikopo kwa kuwasiliana na Serikali kuhakikisha changamoto hiyo, elimu
na ujenzi wa mabweni.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini katika maadhimisho ya
miaka 55 ya chuo hicho yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Nkrumah chuoni hapo.
Alisema baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuongoza
chuo hicho, aliwasiliana na viongozi wa chuo na Serikali ili kuona miundombinu
inaimarishwa huku akisisitiza kuwa mazungumzo hayo yalichangia kwa kiasi
kikubwa ujenzi wa mabweni unaoendelea chuoni hapo.
"Naahidi nitaendelea kufanya kazi na Baraza la Chuo,
Serikali na wadau kutafuta njia ya kutatua matatizo ya mikopo, mahali pa kulala
wanafunzi na miundombinu mingine, yote ni kukifanya kiendelee kuwa na hadhi
yake," alisema.
Dk Kikwete alisema jamii inatakiwa kutambua mchango wa
chuo hicho katika nyanja mbalimbali ikiwamo kuzalisha viongozi wa Serikali,
wachumi, wakuu wa idara taasisi za umma na binafsi na wanasheria na kuongeza kuwa
utafiti wa wanafunzi wa chuo hicho umesaidia kuleta matokeo chanya kwenye
jamii.
Alitaka viongozi na wanafunzi wa Udsm kuendeleza juhudi
ili kiendelee kuongoza huku vingine vikifuatia ambapo pia alimpongeza Baba wa
Taifa, marehemu Mwalimu Julius Nyerere kwa mchango mkubwa uliofanikisha
kuanzishwa chuo hicho.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala,
alimpongeza Dk Kikwete kwa jitihada zake za kuboresha miundombinu hasa ujenzi
wa mabweni unaoendelea na kusisitiza kuwa chuo hicho ni miongoni mwa vyuo bora kwenye
ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alifafanua sababu zinazofanya kiwe bora ndani na nje ya
nchi kuwa ni mchango wake wa kuzalisha marais wa nchi, viongozi na bado kinakabiliwa
na changamoto za vitendea kazi vya maabara, ukosefu wa wafanyakazi hali
inayosababisha utekelezaji wa shughuli chuoni hapo kushindwa kufanyika
ipasavyo.
Mhadhiri mwalikwa ambaye pia ni mteule wa mkuu wa chuo,
Profesa Tade Aina alivishauri vyuo vikuu vya Afrika kuendeleza misingi, mipango
na malengo yaliyofanya vianzishwe ikiwamo kutoa viongozi waliopigania uhuru wa
nchi zao.
Aliwataka viongozi wa Afrika kuendeleza mawazo ya
kuanzisha Chuo Kikuu cha Kiswahili ambacho kitatumiwa na wasomi wa ndani na nje
kujifunza lugha hiyo hali itakayochangia kuondoa mawazo na fikra za kikoloni.
Alishauri viongozi wa chuo kuboresha ufundishaji kwa kutilia
mkazo ufanyaji utafiti mbalimbali utakaotoa wahitimu bora watakaoleta tija.
0 comments:
Post a Comment